Header Ads

MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 02


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Akiwa njiani aliwaza sana uhusu vifo vyote hasa vinavyoihusu familia yake kama wameuawa wote aliyebaki ni yeye na kama asipomuwahi muuaji basi atamuua yeye.
“Hivi Malaika Mweusi anaweza kuwa muuaji?.....inawezekana maana nimemuona eneo la tukio sasa hivi, kwani ana siri gani inayomfanya afanye hivyo?” Mr. Anderson alijikuta akizungumza peke yake. Hakuamini mtu aliyemuamini na kumbatiza jina la Malaika Mweusi awe muuaji, kama ni kweli alihusika hakuwa Malaika Mweusi bali Shetani Mweusi.
SASAA ENDELEA...
*******
Alianza kukumbuka siku ya kwanza walipoanza kufahamiana na Malaika Mweusi ilikuwa ni siku ambayo alikuwa amechanganyikiwa kutokana na zaidi ya miezi miwili kutokutulia nyumbani kutokana na mfululizo wa matukio ya vifo vya watu kila kukicha watu waliuawa na muuaji hakuonekana.
Kwanza yalikuwa mauaji ya mzungu mmoja aliyekuwa msimamizi wa uchimbaji wa madini. Kabla hajajua kinachoendelea vikatokea vifo vya kutisha vya wazungu wengine sita ambao waliuawa kinyama kwa kupigwa risasi nyingi miilini. Hali ile ilitishia jiji na kufanya kikosi cha upelelezi na jeshi zima la polisi uwa katika wakati mgumu wa kuhangaika huku na huko kuwasaka wauaji wenye mbinu za kijasusi.
Kutokana na kuwa bize katika suala la kutafuta muuaji usiku na mchana bila mafanikio hali ilimfanya Anderson kutokuwa karibu na mkewe. Kitendo cha kutolala kila siku nyumbani na mkewe na kutopata muda wa kuzungumza, kwa muda mwingi, kuwa bize na shughuli za serikali. Hali iliyosababisha mkewe amjie juu na kumuomba achague moja kazi ama mke.
Pamoja na kumwambia mkewe umuhimu wake kwa taifa lake, kuwa yeye ni mtumishi wa watu. Lakini mkewe hakumuelewa na kutishia endapo ataendelea hivyo basi yeye atarudi nyumbani kwao.
Anderson alifikiri kuwa ni utani, siku moja aliporudi kutoka kwenye msako wa muuaji hakumkuta mkewe alikuwa amerudi kwao, alijikuta amechanganyikiwa. Muuaji hakumtia mkononi na mkewe ndio amekimbia na alipokwenda kwao alimkatalia katakata huku akimwuliza:
“Huyo muuaji ameshampata?”
“Bado.”
“ Kama bado unanifuatia nini?”
“Sikiliza mke wangu muuaji na ndoa yetu ni vitu viwili tofauti kila kitu kina nafasi yake.”
“Kwa hiyo muuaji amechukua nafasi zote au sio? Basi mimi nakuachia umsake huyo muuaji ni mtu mwenye mbinu za hali ya juu hivyo kumtia mikononi ni vigumu itachukua muda mrefu.”
“Mimi kurudi nyumbani sitaki chagua moja uachane na kazi hiyo ya kumsaka muuaji au la mimi niendelee kubaki nyumbani.”
“Mke wangu elewa kazi ndiyo inayotuweka mjini, sasa nikiacha unataka tukae tunatazamana, tutakula mawe?”
"Ina maana hiyo kazi nzito umeanza leo, tuna miaka minne sijaona kitu kama hicho basi watu wote walioolewa na watu kama ninyi hawafurahii maisha ya ndoa?”
“Hapana mambo haya hutokea kwa msimu hivyo nivumilie.”
“Siwezi, we endelea sijakuzuia, najiona sina tofauti na mlinzi wa nyumba, mara simu ililia Anderson alilipokea ilikuwa inamjulisha kifo cha meneja wa wa kampuni ya mafuta jijini ambaye amekutwa ofisini kwake.
Anderson alijikuta katika kipindi kigumu, alijiuliza atamwelezaje mke wake juu ya ujumbe alioupata muda ule.
“Unashangaa shangaa nini?” Mkewe alimuuliza.
“Aah! Kawaida.”
“Wee nenda,” mkewe alisema baada ya kuigundua simu ilikuwa ya kazi.
“Sawa….. sasa tutaongea vizuri nikirudi mpenzi.”
“Sawa, lakini hakikisha unampata muuaji ama sivyo uzi ni uleule, bai,” mkewe alimuaga huku akishikilia msimamo wake.
Anderson aliingia katika gari na kuelekea eneo la tukio, alijikuta katika kipindi kigumu maishani mwake toka atoke tumboni kwa mama yake. Kazi aliipenda ndiyo inamfanya aitwe mwanaume na mkewe vile vile anampenda ni zaidi ya kazi kwani ndiye pumbazo la moyo wake suruhisho la mawazo yake.
Ule usemi wa mwili mmoja wa mke na mume, mkewe Sarah aliudhinisha kwani alikuwa mshauri mwema wa mumewe. Alimlea kama mwanawe na mtoto wao wa kike Gift.
Hali ya mkewe kubadilika ilimchanganya, alikuwa na haki ya kulalamika, mwezi wa pili hajalala ndani kwa kusaka muuaji. Heri angempata kuliko kuwa kama anazurula bila mpango.
Anderson alifika kwenye eneo la tukio kwenye ofisi moja iliyopo katikati ya jiji, alikuta umati wa watu wengi. Alijipenyeza katikati yao na kukutana na kijana wake walipanda juu ya ghorofa ya tatu.
Waliingia na kumkuta mtu mmoja mwenye umbo kubwa aliyevaa kinadhifu akiwa amelalia meza akitokwa na povu lililochanganyika na damu. Walimnyanyua na lile povu liliochanganyika na matapishi yenye damu lilichuruzika chini ya meza.
Anderson baada ya kumchunguza yule mtu aliwaamuru vijana wake kumpeleka hospitali kwa ajili ya uchunguzi. Alimchukua secretari wa meneja aliyeuawa, na aliondoka naye kwa mahojiano zaidi.
Walipofika ofisini alikuwa na mahojiano mafupi na secretari.
“Binti una muda gani katika ofisi ambayo imetokea mauaji?”
“Ni mwaka na miezi mitano sasa.”
“Unazifahamu vizuri tabia za bosi wako?”
“Kuzifahamu kivipi?”
“Yaani muundo wa maisha yake kwa ujumla.”
“Si sana.”
“Nieleze unavyomfahamu.”
“Bosi ni mtu mpole, mcheshi na alikuwa anajali wafanyakazi wote tulio chini yake.”
“Unaweza kunieleza kifo cha bosi wako kimetokana na nini?”
“Kwa kweli sijui.”
“Ni nani aliyegundua bosi wako ameshafariki?”
“Mimi.”
“Uligundua kivipi?”
“Wakati nampelekea kahawa kama ilivyo kawaida yake, muda ukifika ni lazima nimpelekee. Nilishangaa kumkuta bosi kalalia meza na povu lililochanyanyika na damu lilimtoka mdomoni.”
“ Baada ya kuona hivyo ulifanya nini?”
“Nilipiga kelele ya woga iliyowafanya wafanyakazi wenzangu waje kuangalia kuna nini, ndipo ilipojulikana kuwa amefariki na kuamua kujulisha chombo cha usalama.”
“Ni nani aliyeingia ofisini kwake kwa mara ya mwisho?”
“Mmh! Sina uhakika sana…Aaaha, sawa ni msichana mmoja hivi.”
“Unamkumbuka sura yake?”
“Hapana alikuwa amevaa hijabu iliyomfunika uso na alikuwa akizungumza lafudhi ya Kiunguja.”
“Alichukua muda gani?”
“Mmh! Sina kumbukumbu sidhani kama alitoka, maana nina uhakika sikumuona akitoka. Hata muda wa kumpelekea kahawa nilijua bado yupo nilibeba vikombe viwili, ajabu sikumkuta na kukuta bosi katika hali kama vile nilivyoeleza.”
“Unadhani ni muda gani alipita toka yule msichana aingie na wewe kupeleka kahawa?”
“Zaidi ya saa tatu.”
“Saa tatu! Mazungumzo gani ambayo hukuyatilia wasi wasi?”
“Saa tatu mbona ni chache, huzungumza na wateja zaidi ya saa sita.”
“Sawa, unaweza kwenda lakini uwe tayari muda wowote tunakuhitaji.”
“Sawa muheshimiwa,” yule secretari aliruhusiwa kuondoka.
Anderson aliongozana na baadhi ya vijana wake kuelekea hospitali kwa ajili ya majibu ya kifo cha meneja. Alipofika alipata maelezo kuhusiana na kifo cha meneja wa kampuni ya mafuta. Dokta alimweleza kuwa kifo cha meneja kimetokana na kupuliziwa dawa ya sumu iliyoharibu mapafu na kifua.
Kwa mara ya kwanza Anderson aliona kazi ya upelelezi ni ngumu, kumtafuta mtu asiyemjua na mtu mwenyewe awe na ujuzi wa hali ya juu anayefanya mauaji yake kwa mpangilio wa hali ya juu. Wakati anatoka hospitali alikuwa ni mwingi wa mawazo juu ya mauaji yale alijiuliza maswali yasiyo na majibu.
“Kwa nini muuaji ameamua kufanya vile, lazima ipo sababu yake au ndiyo kiasasi? Na kama kisasi kwa nini asitoe taarifa kwenye vyombo husika ili wabaya wake wakamatwe na kufunguliwa mashtaka? Mbona mauaji yenyewe yanachanganya? Mmh! Kazi ya upelelezi ni ngumu kumtafuta mtu usiyemjua inawezekana kabisa anakufahamu na kula naye meza moja.
Mmh! Kweli huu ni mwaka wangu, muuaji ananichanganya na mke wangu aishi vituko vinavyotishia maisha ya ndoa yangu. Kitu kisichowezekana eti niamue kuacha kazi tutakula mawe?”
Anderson alijikuta anazidi kuchanganyikiwa, ili kutuliza mawazo aliamua kuingia katika ukumbi mmoja wa starehe wa Puzzo Hill Hotel na kutafuta meza moja ya pembeni mwa ukumbi uliokuwa umejaa watu. Lakini kuna meza moja ilikuwa tupu watu ndiyo kwanza walikuwa wamenyanyuka.
Alipoketi kitini alionekana mtu mwenye mawazo mengi, mikono ilikuwa shavuni. Hata mhudumu alipofika kumsikiliza mbele yake hakumuona.
“Samahani kaka nikusaidie nini?”
“Ooh! Samahani dada yangu nilikuwa mbali nisaidie safari mbili.”
”Sawa kaka yangu punguza mawazo, kama huna kampani mimi nipo kwa ajili yako.”
“Asante dada yangu nitakapohitaji nitakujulisha.”
Yule mhudumu alifuata bia huku sehemu zake za nyuma akizitingisha, naye hakuwa haba Mungu alimjalia. Anderson aliyekuwa katikati ya mawazo hakukiona alichokifanya muhudumu yule. Baada ya kumuagiza alizama tena ndani ya dimbwi la mawazo kwa kurudisha mikono yake shavuni.
“Samahani mpenzi kinywaji hiki,” mhudumu alishtuka zaidi ya mara mbili, Anderson alizipiga zote mbili kama tarumbeta kisha akaagiza nyingine mbili. Nazo alizipiga kama tarumbeta zilipofika sita aliagiza nyingine mbili ambazo alikunywa taratibu muda huo sasa ulikuwa majira ya saa moja usiku.
***
Anderson aliamka siku ya pili yake na kugundua sehemu alipolala si nyumbani kwake ilikuwa sehemu ngeni. Alipepesa macho yake, alishtuka kuona pembeni yake amelala binti mwenye urembo wa shani. Kama yule binti angekuwa mweupe na uzuri ule basi angejua ni jini.
Binti aliyelala pembeni yake alikuwa na uso wa kitoto yaani ‘baby face’. Alikuwa amepitiwa na usingizi wa fofofo, Anderson alianza kujiuliza:
“Hapa ni wapi?”
Alipepesa macho yake na kugundua pale ni nyumba ya wageni, alijiuliza amefikaje pale, kutoka alipofunga ndoa na mkewe hajawahi kulala nje, pasipokuwa na sababu za kikazi wala kuwa na uhusiano na mwanamke yeyote zaidi ya mkewe mama Gift.
Alijiuliza yule mwanamke ni nani mbona hamtambui ilibidi avute hisia za jana ilivyokuwa.
“Mmh! Jana nilipotoa hospitali nilikwenda Puzzo Hill Hoteli..Ehe nimekumbuka, niliagiza vinywaji.. eeh.. sawa.. aliingia msichana aliyeushtua moyo wangu aliyekuja moja kwa moja ahadi kwenye meza yangu na kuniambia nikae naye.
”Oooh sawa nilimkubalia na kuanza kunywa pamoja, mmh nina imani hapo ndipo mwisho wa kumbuumbu zangu. Lakini kilichoendelea sikujua cha kushangaza nimeshituka alfajili hii na kujikuta nipo hotelini na mtu nisiyemjua wala kuwa na uhusiano naye.
“Hizi pombe sasa zinanipeleka pabaya Mungu wangu! Sijui nimefanya nae ngono? Na kama nimefanya sijui kama nimetumia kinga huu ndiyo mwanzo wa kuambukizwa ukimwi.”
“Vipi umeamka zamani,” Sauti tamu mithili ya kinubi cha mtume Daudi alichotumia kumbembeleza mfalme Sauli, ilipenya wenye ngoma za masikio ya Anderson na kumfanya alishtuka kutoka kwenye lindi la mawazo.
“Eeeh!”
“Pole sana kaka yangu, inawezekana kuna jambo linakutatiza lililokuchanganya akili yako, tena si dogo ni kubwa,” alisema yule binti huku akitambaza mikono yake laini mgongoni kwa Anderson.
Habari zile zilizidi kumchanganya ilibidi amuulize yule binti kwa ukali.
“Hizi habari zangu umezijuaje? Wewe ni nani na hapa ni wapi na nimefikaje?”
“Aah! Kaka yangu unaniuliza kwa ukali hivyo au wema wangu kwako umekuwa mbaya? Basi nisamehe kwa wema wangu.”
Kauli tamu ya binti mrembo ilimfanya Anderson kuwa mpole.
“Samahani dada yangu, sikuwa na nia hiyo kauli yangu imekuwa kali naomba nisamehe kwa hili.”
“Basi kaka yangu jana nilipoingia ukumbini, sehemu zote zilikuwa zimejaa watu ila meza uliyokuwa umekaa peke yako ilikuwa na nafasi ndipo nilipokuja kukuuliza kama una mtu ulinijibu kuwa uko peke yako kwa sauti ambayo ilionyesha umeshaanza kulewa.
“Tulijumuika pamoja na tukaanza kunywa kwa pamoja huku ukinikataza nisilipe utalipa wewe. Tulipokuwa tukiendelea kunywa ulionekana ni mtu mwenye mawazo mengi. Ilikuwa haipiti dakika mbili lazima ujifyonye na kila nilipokuwa nikikuuliza, ulinijibu we acha tu.
“Sikujua una maswahibu gani kilichonishangaza zaidi ni unywaji wako wa pombe wa kupita kiasi. Hata nilipojaribu kukukataza ulinikaripia nikuache la sivyo utanifukuza.”
“Nilikuacha unywe utakavyo, ukinywa mpaka ukawa ujielewi na kulala juu ya meza, nikawa sina jinsi siwezi kukuacha peke yako unaweza kuiibiwa na vibaka vitu vyako si unajua jinsi vibaka wanavyo watamani walevi.
“Ilibidi nikunyanyue kwa shida mpaka nje kwenye gari lako, kwani nilikuwa nalijiua wakati unateremka garini nami nilikuwa naingia. Nilipokupapasa nilikukuta na funguo ya gari na pesa shilingi laki mbili na ishirini. Nilikukokota hadi kwenye gari na kukupeleka sehemu ambayo utapumzika kwa amani hadi asubuhi hii uendelee na shughuli zako.”
“Mmh! Siamini wewe ni msichana wa ajabu hii ni hoteli gani na gari langu liko wapi?”
“Hapa ni Biski Hill Hotel, Hoteli ya kitalii iliyo pembeni mwa bahari yenye ufukwe mwanana na gari lako lipo salama kwenye maogesho ya magari ya hoteli hii.”
“Siamini wewe ni kiumbe wa ajabu lazima nilipe fadhila zako.”
“Hapana sikukutendea wema ili unilipe fadhila, bali ni msaada kama msamaria mwema.”
“Sawa, suruali yangu ipo wapi?” Mr Anderson aliuliza.
Yule msichana alimletea, aliingiza mkono mfukoni na kuhesabu fedha zake na kuzikuta sawasawa pia simu yake ilikuwemo, alichukua laki moja na kumpa yule msichana kama asante.
“Hapana kaka yangu ukinipa siku nyingine nitachukua siyo leo.”
Wakati huo yule binti alikuwa akinyanyuka kutoka kitandani na kuelekea bafuni kuoga alipotoka bafuni alivaa nguo zake na kumuaga.
“Samahani kaka wacha nikuache uendelee kupumzika,” yule binti aliupitia mkoba wake ili aondoke, Anderson alitaka kumfahamu vizuri.
“Samahani mrembo, unaitwa nani?”
“Naitwa Teddy”.
“Ooh! Jina zuri kutokana na vitu ulivyonitendea sina budi kukubatiza jina lingine.”
“He! Lipi tena hilo?”
“Nakuomba nikuite ‘Black Angel’ Malaika Mweusi.”
“Sidhani kama ninalingana na hilo jina,” Teddy alisema huku akibinua midomo kike.
“Siku zote kioo cha kujifahamu ni yule aliye pembeni yako wewe mwenyewe hata siku moja huwezi kujijua,” Anderson alisema huku akimtamaza yule binti.
“Nakushukuru kwa jina hilo, langu umelijua sijui wewe unaitwa nani?”
“Naitwa Anderson.”
“Nakushukuru kaka yangu kwa kulijua jina lako, nilikuwa na hamu ya kujua nini kilichokusibu lakini muda hauniruhusu ila siku yoyote Mungu akijalia tutaonana.”
”Hapana Malaika wangu, nina mengi ya kuzungumza kila nikikuangalia sipati jibu. Hivyo nakuomba jioni ya leo tukutane Puzzo hoteli.”
”Sawa basi tukutane saa 12:00 jioni tuwe na ahadi za uhakika japokuwa wengi wanakasumba kusema za kizungu, ina maana mzungu akichelewa atakuwa na ahadi za Kiswahili?”
“Inaonekana u muelewa sana, kwa kugundua kasumba iliyotutawala wengi.”
Anderson aliagana na Mailaka Mweusi, alipotaka kumsindikiza alitakataa.
“Kwa nini nisikusindikize?” Anderson alihoji.
“Hapana usisumbuke kuna usafiri hapo nje unanisubiri,” Malaika Mweusi aliondoka na kumwacha Anderson bado akiwa kitandani amejifunga shuka.
Baada ya Malaika Mweusi kuondoka Anderson alibakia na maswali mengi kichwani juu ya msichana yule aliyetoka muda mfupi na kukiacha chumba kikinukia manukato ya bei mbaya. Alimshangaa yule msichana alikuwa wa aina gani, wasichana wengi jijini hujiuza ili kujikimu na ugumu wa maisha. Lakini ilikuwa tofauti na tena kwa tofauti kubwa. Alikuwa na uwezo wa kuchukua kila kitu hata gari, lakini kila kitu amekikuta kipo katika hali nzuri, ilikuwa ajabu kubwa kwake.
Aliomba jioni ifike haraka ili aweze kuonana na binti wa ajabu aliyemfananisha na Malaika Mweusi. Aliona hakuna muda wa kuendelea kuwa pale alinyanyuka na kwenda bafuni kuoga ili akirudi nyumbani kubadili nguo ili aingie ofisini kumtafuta muuaji ambaye ameichanganya akili yake kila kukicha na bila ya kumsahau.
Mke wake aliyempa masharti ya kutorudi nyumbani mpaka awe amempata muuaji sharti lililompa wakati mgumu. Lakini vitu alivyofanyiwa na Malaika Mweusi vilimpunguzia mawazo yake aliyaelekeza kwake alimuona ni msichana wa ajabu.
Kutwa nzima alifanya kazi lakini akili yake yote ilikuwa kwa Malaika Mweusi msichana wa ajabu ambaye akuwahi kumuona katika maisha yake yote. Ilipotimu saa kumi jioni alirudi nyumbani alijiandaa kwa ajili ya kukutana na Malaika Mweusi.
Anderson alivalia nguo zenye hadhi ya juu na kujipulizia pafyumu ya bei mbaya ambayo huitumia mkewe ili aonekane mtu wa hali ya juu. Alijitazama kwenye kioo na kujiona amependeza kwani nguo zilikuwa zimemkaa vyema, alitazama saa yake ya ukutani iliyomuonyesha ni saa kumi na moja na robo alijua muda ule utamtosha kufika Puzzo Hoteli.
Alikwenda kwenye banda la gari na uchukua gari lake tayari kwenda Puzzo Hoteli kwa ajili ya kuonana na Malaika Mweusi binti wa ajabu ambaye alimfanya asiamini kama kweli aliyoyafanya yanatendeka katika dunia ya sasa ambayo asilimia kubwa ya akina dada wamekuwa na roho ya kinyama.
Kwa hali aliyomkuta angeibiwa kila kitu ikiwa pamoja na gari lake. Majira ya saa kumi na mbili kasoro dakika tano aliwasili eneo la Puzzo Hotel, alipepesa macho yake huku na kule ili atafute sehemu nzuri ya kuegesha gari lake na baada ya muda aliiona sehemu nzuri ya kuegesha gari lake.
Akiwa katika harakati za kupaki gari lake mara gari dogo aina ya Mitsubishi Pajero nyeusi ilipita na kwenda kusimama mbele yake, akiwa anasubiri lile gari limpishe aliteremka binti mrembo katika lile gari.
Anderson alijikuta anapigwa na bumbuwazi na woga wa kumtawala alijikuta akijisemea moyoni. Yule msichana alipiga hatua za alipiga hatua za taratibu kwenda alipo.
Ile ilimpa nafasi ya kumsoma vizuri yule mrembo sura na umbile lake alianza kumwangalia toka nywele zake za rasta ndogondogo zilizoishia mgongoni na usoni alivaa miwani ndogo ya mviringo iliyobebwa na pua ndogo ya kitusi, midomo yake midogo ambayo ilionekana kama iliumbwa kwa matumizi ya vitu laini na vinywaji baridi.
Akiwa bado anamkazia macho yule msichana aliyekuwa amemuelekea alikutana na tabasamu lililozidisha uzuri wa binti aliyekuja mbele yake ambaye alionesha kama anamfahamu lakini kwake alikuwa mgeni.
Lilikuwa tabasamu tamu lililonakshiwa na mwanya mwembamba lililopoteza mawasiliano katika ubongo wa Anderson. Yule msichana alikuwa amevalia brauzi cha rangi ya jani la mgomba iliyoishia juu ya kitovu na kuliacha tumbo lake dogo wazi kidogo, chini alivaa sketi yenye rangi kama kiblauzi iliyoishia kidogo juu ya makalio kutokana na kupasuliwa kwa nyuma na nyuma alikuja amejaaliwa kiasi hakika mwenyezi Mungu alimpendelea kwa kila kitu.
Shingoni alikuwa na cheni tatu za dhahabu hesabu ya haraka haraka zilikuwa na thamani ya milioni mbili kasoro, masikioni kila sikio lilitobolewa matundu matano na kila tundu lilikuwa na hereni ya dhahabu, vidoleni kila kidole kilikuwa na pete ya dhahabu ya miundo tofauti mkono mmoja ulikuwa na bangili ya dhahabu na mwingine ulikuwa na saa ndogo vilevile ya dhahabu, mdomo ulikuwa na meno mawili ya dhahabu.
Tabasamu ya yule binti nusra lisimamishe mapigo ya moyo katika mwili wa Anderson. Akiwa bado ameshangaa kama kaona meli barabarani yule binti mrembo alipita upande wa pili wa mlango wa gari la Anderson na kufungua mlango baada ya kuingia alifunga mlango.
Aliona kama yupo ndotoni baada ya kuona ule mlango unafunguliwa na yule msichana mwenye uzuri wa ajabu aliyevaa vitu vyenye mamilioni ya pesa.
“Eeeh…unataka lifti?’ Aliuliza huku akimtupia jicho la wizi.
“Anderson vipi?” yule msichana alisema kwa sauti tamu na laini. “Unasemaa….Umejuaje jina langu?” Anderson alimshangaa yule mrembo.
“Unanitania au unasema kweli?” binti mrembo aliuliza.
“Si utani, we nani na umejuaje jina langu?”
“We umekuja kukutana na nani hapa?”
“Swali lile lilimshtua Anderson alituliza akili na kumuangalia yule binti aliyekaa pembeni yake ambaye kipindi hicho alikuwa amevua miwani yake. Taratibu sura yake ilianza kumjia na kugundua ni Malaika Mweusi lakini huyu ni mzuri mara dufu lakini harufu ya manukato yalimfanya abahatishe.
“Ina maana wewe ni Malaika wangu?”
“Ndio mimi wala si mwingine,” Malaika alijibu huku akilegeza sauti.
“Umebadilika kwa asilimia mia.”
“Si kweli, sura na umbile lilelile kilichobadilika ni mavazi.”
“Malaika Mweusi umependeza sana, hongera sana unastahili pongezi zangu.”
“Nashukuru, sasa ni hivi geuza gari tuelekee tulipolala jana, ni sehemu inayofaa kwa mazungumzo,” Malaika alimweleza Anderson.
Anderson aligeuza gari na kwenda Biski Hoteli, waliposhuka Biski Hoteli walikwenda moja kwa moja hadi mapokezi. Chumba kimoja kilikuwa laki mbili na nusu moja za Kitanzania. Mr Anderson aliingiza mkono mfukoni ili atoe malipo ya chumba lakini Malaika Mweusi alimkataza.
“Hapana nitalipa mimi,” Malaika Mweusi alifungua mkoba wake na kutoa noti kumi za kumikumi na kulipa. Walipewa chumba kimoja chenye kila kitu, walipoingia chumbani Malaika Mweusi alikaa kitandani na Anderson alikaa kwenye sofa. Malaika Mweusi alihama kutoka kwenye kitanda na kumsogelea karibu na Anderson, wakati huo Anderson alionekana mtu mwenye mawazo mengi.
“Vipi Mr Anderson naona uko mbali?”
“Ha…ha..pana tuko pamoja.”
“Nina imani huu ni muda mzuri wa kuzungumza lililokusibu jana,” Malaika Mweusi alisema huku akitembeza kikono yake kwenye kifua cha Mr Anderson.
“Halina umuhimu sana tuachane nalo.”
“Hapana Anderson nipo hapa kwa ajili yako nimeacha kazi zangu naomba ujali muda wangu na pia ni muhimu mimi kuwa hapa,” Malaika Mweusi alisema kwa msisitizo. Anderson hakupenda mambo yake yatoke nje wala siri ya kazi yake. Akabaki katikati ya mawazo, Malaika Mweusi alimstua.
“Mr. Anderson naona huna la kuongea?” Malaika Mweusi alinyanyuka na kutaka kuondoka.
“Hapana usiondoke na nitakueleza,” Anderson alinyanyuka na kumshika mkono Malaika.
Wakati huo Malaika Mweusi alikuwa ameshachukua mkoba wake ili aondoke, Anderson alimshika mkono na kumrudisha kwenye sofa.
“Samahani Malaika wangu sina nia ya kukuudhi bali linataka maelezo ya kina.”
“Ndio maana nikaamua kuondoka kwa vile sina msaada kwako wala umuhimu wowote,” Malaika alijibu kwa hasira kidogo.
“Hapana Malaika wangu sina maana hiyo wewe ni mtu ninaye kuona una umuhimu wa kipekee kuliko hata hao niliokuwa nao muda mrefu. Wewe kwa ufupi inaonyesha jinsi gani unanijali sina budi nikueleze kilichonisibu.
“Usinieleze kwa kukulazimisha haitakuwa vizuri bali kwa hiari yako.”
“Nitakuelewa kwa hiyari yangu.”
“Haya nieleze.”
Anderson alimweleza masahibu yote yanayomzonga ubongo wake hadi hatua ya kuichukia dunia na kujuta kwa nini amezaliwa mwanaume. Alikuwa amechanganywa na mauaji yaliyokuwa yakitikisa jiji kwa takribani miezi miwili na nusu. Akiwa katika mtihani mzito wa kumsaka muuaji mkewe naye alimjia juu kwa kitendo cha kukosekana nyumbani usiku na mchana na muuaji haonekani kila moja lilimchanganya sana.
“Nashindwa Malaika wangu nifanye nini, muuaji amenichanganya akili nyumbani nako mke wangu anazidi kunichanganya ati niache kazi, unafikiri nitakuwa mgeni wa nani utaishi vipi bila kazi?” Anderson kwa mara ya kwanza alijikuta anitoa siri ya kazi yake kosa lilikuwa kubwa kumuamini usiyemjua.
Malaika Mweusi baada ya kumsikiliza kwa kina alimsogelea Anderson aliyekuwa ameweka mikono shavuni akionesha wazi kuwa amekosa ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwa mbele yake.
Malaika Mweusi aliuweka mkono wake mgongoni kwa Anderson na kuongea kwa sauti yake tamu mithili ya kinubi cha mfalme Daudi, aliongea kwa sauti ya chini:
“Pole sana Anderson kweli mzigo uliokuwa mbele yako ni mzito sana unahitaji msaada mkubwa... sasa ni hivi….”

ITAENDELEA

No comments