Header Ads

Mastaa Waislam Bongo Mchana Watakatifu Usiku Mapopo Mwezi Mtukufu wa RamadhaniWakati Waislam duniani kote wakiwa kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wakitakiwa kujiepusha na maovu kwa kutenda yaliyo mema, kuna baadhi ya mastaa Waislam Bongo ambao mchana wanajifanya ni wanyenyekevu lakini usiku wanampa Mungu kisogo! 

UCHUNGUZI WA IJUMAA
 Uchunguzi uliofanywa na Ijumaa tangu mfungo uanze Jumanne iliyopita wiki hii umebaini kuwa, baadhi ya mastaa hao wamekuwa wakimchezea Mungu kwa kuendeleza maovu gizani lakini wanapokuwa mbele za watu, wanajifanya wana hofu ya Mungu ‘watakatifu’, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya dini hiyo.

 MCHANA NJIWA, USIKU POPO… 
Katika uchunguzi huo, imebainika kuwa, wapo mastaa ambao mchana wanafunga na kuvaa mavazi ya staha kama vile mabaibui, madira, magauni marefu na kanzu huku wakipewa jina la Team Njiwa lakini usiku ni mwendo wa kuvaa kihasara na kukesha kwenye kumbi za starehe ambapo hawa wamepewa jina la Team Popo. Imefahamika kuwa, licha ya kujinadi kuwa ni Waislam, baadhi ya mastaa hao wamekuwa wakiendelea kufanya mambo ya anasa usiku ikiwemo kuzini, kunywa pombe na mambo mengine ya kumchukiza Mungu lakini mchana wanajifanya wamefunga na wakati mwingine kuzuga kwa kwenda msikitini sambamba na kuwafuturisha watu. 

NI WAISLAM MAJINA 
Ilielezwa kwamba, kutokana na matendo yao, mastaa hao wa kada mbalimbali hasa wa filamu na Bongo Fleva, wamekuwa wakiitwa Waislam majina ambapo licha ya kuitwa majina kama vile Aisha, Salama, Juma, Said na mengineyo, bado wamekuwa wakifanya
mambo ambayo ni kinyume na imani ya dini yao. Ilibainika pia kwamba, wapo ambao wamekuwa hawafungi wakidai wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali lakini kumbe siyo kweli, wanalenga kukwepa kutimiza nguzo hiyo muhimu katika Uislam. 


WAUMINI WAWACHANA 
Wakizungumzia tabia hiyo kwa nyakati tofauti, baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislam waliozungumza na Ijumaa walisema kuwa ni vyema mastaa hao wakajiangalia upya kwani kama wao ni kioo cha jamii, wanaposhindwa kufuata taratibu za dini yao, wanawayumbisha hata mashabiki wao ambao huwachukulia kama mfano wa kuigwa. “Kwa mfano, Wema Sepetu, Shilole (Zuwena Mohammed), Nisha (Salma Jabu), Batuli (Yobnesh Yusuf) na wengine wa Bongo Muvi najua ni Waislam na wana mashabiki wengi Waislam na Wakristo, sasa wao kama wasanii wanatakiwa kufuata dini yao inasemaje ili hata wale mashabiki wao wa Kiislam wafuate kile wanachokifanya. “Ikiwa kwa mfano Wema anafunga halafu usiku anaonekana klabu au baa, mashabiki wake hawawezi kumuelewa,” alisema Seleh Idd wa Sinza jijini Dar. Mwingine ambaye hakupenda jina liandikwe gazetini alisema: “Hili ni tatizo, wapo baadhi ya mastaa ambao tunawajua ni Waislam lakini cha ajabu ndiyo wanaoongoza kwenye kufanya mambo maovu. Unaweza kumkuta staa wa kike mchana katinga baibui na ushungi lakini usiku kakuvalia kipensi. Huyu naye utamuita Muislam?” 

MAMA SUBIRA AWAFUNGUKIA 
Naye mama Subira wa Kinondoni jijini Dar alifunguka: “Hili halipo kwa mastaa tu, wao ni kwa sababu ya umaarufu wao ila kuna Waislam wengi ambao mchana ni wapole lakini usiku ni micharuko. Unaweza kukuta kijana mchana kavaa kanzu na
kuonesha swaumu imembana sana lakini adhana ikipigwa tu ni kama amefunguliwa kufanya maasi, anakuwa ni mtu wa kubadili viwanja hadi kunakucha. “Mtu kama huyu si bora asifunge tu kuliko kumchezea Mungu? Hili ni tatizo kubwa na wengi hawajui thamani ya mwezi huu, wamefanya maasi kwenye miezi yote iliyopita na huu nao wanataka kuuchafua, viongozi wa dini wafanye kazi ya ziada kuwarudisha, hasa vijana kwenye mstari ulionyooka na hii si kwa mastaa pekee bali hata wasiokuwa mastaa.


” SHEHE MKUU DAR AWAPA VIDONGE VYAO 
Katika suala hilo la baadhi ya mastaa mchana kuwa na sura ya kumuogopa Mungu kisha usiku kuwa micharuko, Ijumaa lilimtafuta Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salim (pichani) ambaye alipopatikana aliwapa mastaa hao vidonge vyao: “Ujue kuna watu na majini watu, sasa hao wa hivyo ni majini watu, maana kufunga si mchana tu, bali ni katika kipindi cha mwezi mzima na maana ya funga ni kujizuia na mabaya yote yaliyokatazwa na Mungu na kufuata yale yaliyo mema aliyoyaamrisha. “Sasa itakuwaje mtu mchana azingatie hayo halafu usiku aende kinyume na maadili ya dini inavyotaka, tena kwa makusudi? Maana wanajua kwamba wanachofanya si sahihi, niseme tu kwamba Muislam yeyote anayefanya hivyo basi ajue funga yake ni batili na anamkosea Mungu.” Baadhi ya mastaa Waislam ambao wanatakiwa kuwemo kwenye mfungo huu kama hawatakuwa na udhuru unaokubalika ni pamoja na Wema, Shilole, Nisha, Batuli, Tiko Hassan, Rose Ndauka, Kulwa Kikumba ‘Dude’, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, Tamrina Poshi ‘Amanda’ na wengineo.

No comments