Header Ads

Zijue hasara za ushauri wa kimapenzi 2KARIBU tena msomaji wangu wa kona hii ya Sindano za Mahaba. Natumai mu wazima wa afya, kwa wale Waislamu niwatakie mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Baada ya wiki iliyopita kugusia kidogo juu ya hasara za ushauri wa kimapenzi ambapo tuliangalia vipengele kadhaa vikiwemo kukupotosha, kukurahisishia mambo pamoja na kukugeuza.
Endelea kuwa nami katika kumalizia vipengele vilivyobaki;
UTAKUONDOLEA UJASIRI
“Kwa maelezo hayo mumeo ni malaya sana, naona itakuwa vigumu kumbadilisha ni bora ukaanza maisha yako kwa sababu kuna siku hali itakuwa mbaya.”
Huu ni ushauri unaoweza kumuondolea mtu ujasiri wa kukabiliana na tabia ya mumewe hadi kufikia hatua ya kumrekebisha.
Ushauri huondoa ujasiri wa kukabili tatizo hasa pale anayeku-shauri atakapo-lipeleka suala lako kwenye njia ngumu isiyokuwa na ufumbuzi. Ikumbukwe kuwa anayeamini kushindwa ni mshauri lakini wewe kama mwanamke unaweza kusimama kutetea penzi lako na kuliweka sawa mpaka jamii ikasema: “Jamani huyu dada kamrekebisha sana mumewe kaacha ulevi.”
UTAKUNYIMA FURSA
Kwenye mapenzi kuna fursa nyingi za mafanikio ambazo unaweza usizipate ukiwa mtu wa kusikiliza sana ushauri wa watu.
Baada ya kuangalia madhara ya ushauri wa kimapenzi sasa tugeukie katika njia za kuzuia watu wasiingilie mapenzi yenu.
Udhibiti wa taarifa kwa wengine 
Kadiri unavyoelezea uhusiano wako kwa watu wengine ndivyo unavyowapa nafasi kutoa maoni na hata kudhani kuwa wana dhamana ya kukuelekeza unavyotakiwa kuishi na mwenza wako.           Hivyo basi, chukua muda wa kutosha kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu masuala yako ya uhusiano kabla haujaanza kutafuta maoni, ushauri kwa watu wengine.
Upekee wa mambo
Tambua kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya kipekee, mazingira pia ya tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa wengine yanaweza kuwa ni ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza yasikusaidie moja kwa moja katika suluhisho lako.
Ukitambua hili, utafanya bidii ya kujenga uwezo binafsi wa kuchambua tatizo unalokumbana nalo.
Kwa leo niishie hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

No comments