Header Ads

A-Z Gwajima Alivyoingia Kwenye 18 Za Polisi Uwanja wa Ndege, Dar


ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima si mtu anayetafutwa tena na Jeshi la Polisi nchini, kwa sasa angalau.
Aliingiaje kwenye 'hatua 18' za Polisi?
Baada ya kusakwa na polisi kwa siku 25, Askofu Gwajima amekamatwa na kikosi cha polisi cha viwanja vya ndege, alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA), akitokea Nairobi Kenya jana.
Hali hii ni tofauti na mara kadhaa ambapo askofu huyo, amekuwa akikamatwa na polisi wenye silaha na magari baada ya kuzingira nyumba yake kwa saa kadhaa.
Mara ya mwisho kukamatwa na polisi, Askofu Gwajima alionekana akitoka Kituo Kikuu cha Kati cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, akiwa anatumia baiskeli ya wagonjwa, baada ya kutakiwa kuripoti huko muda mfuoi baada ya kulazwa kwenye hospitali moja jijini.
Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi viwanja vya ndege, Martin Otieno, alisema Askofu Gwajima alikamatwa jana saa 2:45 asubuhi alipowasili akitkea Nairobi.
“Tulipomkamata tulimkabidhi kwa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambako huko ndipo alipohojiwa,” alisema Kamanda Otieno.
Alipotafutwa kwa simu yake ya mkono, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, baada ya mwandishi kumweleza jambo ambalo anataka ufafanuzi wake, alijibu kwa kifupi “nipo na watu,” kisha akakata simu yake.
Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala, hata hivyo, alithibitisha kwamba mteja wake amehojiwa na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kisha kumuachia majira ya saa sita mchana.
“Ninachoweza kusema ni kwamba, kweli mteja wangu alihojiwa leo (jana) na Polisi Kanda Maalum na ilipofika majira ya saa sita aliachiwa,” alisema Kibatala.
Alipoulizwa kama mteja wake huyo atakuwa na kesi zaidi baada ya kuhojiwa, Kibatala alisema “Kwa sasa ninachoweza kusema ni kwamba amehojiwa na kuachiwa na yupo nyumbani, hatua nyingine kama zipo ama laa, mimi na mteja wangu hilo hatulijui.”
Juni 17, mwaka huu, polisi wapatao sita wakiwa na gari aina ya Land Cruizer walizingira nyumba ya Askofu Gwajima iliyopo Mbezi Salasala, lakini hawakufanikiwa kumpata.
Taarifa iliyotolewa wakati huo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime ilieleza kuwa Jeshi la Polisi linamtafuta Askofu Gwajima kwa mahojiano.
Lakini taarifa zilizokuwa zinazagaa katika mitandao ya kijamii zilieleza kuwa Jeshi la Polisi lilikuwa linamsaka Askofu Gwajima baada ya kuwapo kwa ujumbe wenye sauti uliokuwa unadhaniwa kuwa wake, ikimtuhumu Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kuhusika na usimamizi mbovu wa uchumi wa nchi.
Miongoni mwa shutuma za askofu huyo kwa Rais Kikwete ni pamoja na kutotumika kwa mita ya kupima mafuta kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kuwapo kwa watumishi hewa serikalini.
Katika ujumbe huo, sauti hiyo ilisikika ikimshauri Rais Dk. John Magufuli atumie mamlaka yake kuwasilisha bungeni muswada wa kufuta kinga ya Rais kushtakiwa baada ya kumalizika kwa muda wake wa kukaa madarakani, ili watangulizi wake Ikulu wafikishwe mahakamani panapokuwa na tuhuma dhidi yao.

Kusakwa huko kwa Askofu Gwajima haikuwa mara ya kwanza kwani mwaka jana Jeshi la Polisi lilimsaka na kufanikiwa kumkamata kwa kosa la kutoa kauli za kumkashifu Askofu Mkuu wa Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinali Pengo.

CHANZO: NIPASHE

No comments