Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 14


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
Maumivu yalikuwa makali nilimsikia mama Gift akiwaamuru wale vijana wake wanipige hadi niage dunia. Kipigo kiliendelea mpaka nikapoteza fahamu sikujua kilichokuwa kinaendelea.
SASA ENDELEA...

Nilipozinduka nilijikuta nipo kwenye nyumba moja mbovu mbovu ya miti ambayo aliyekuwa nje anakuona waziwazi juu iliezekwa na majani, nilijishangaa sana pale nilipo ni wapi nilipotaka kujigeuza nilihisi maumivu makali sana mwili mzima nilikuwa nimelazwa kwenye kitanda cha kamba nilitulia kidogo na kuvuta hisia kuwa pale ni wapi na nimefikaje na mara ya mwisho nilikuwa wapi.
Nikiwa katikati ya mawazo mara alitokea mzee mmoja wa makamo akiwa amembeba mtoto mdogo kama wa miezi saba mgongoni na kanga chakavu.
''Unajisikiaje mjukuu wangu?”
''Wewe ni nani na hapa nilipo ni wapi?” nilimuuliza yule babu ambaye kichwani alikuwa na nywele nyingi nyeupe.
''Mjukuu wangu hapa ni kijiji cha Nyato au kama wenyeji wanavyopenda kukiita Hatanijua nani, na mimi mjukuu wangu naitwa Nitakufa lini siku zenyewe hazisogei.” “Mmh jina hili kiboko,” niliguna kimoyomoyo.
''Samahani babu utakufa lini hapa kwako nimefikaje?”
''Ni historia ndefu la muhimu kwanza ni kushughulikia afya yako, Mungu mkubwa sikutegemea kama ungeongea tena.”
“Kwani babu ilikuwaje?”
“Taratibu mjukuu wangu labda nikuulize wewe ulikumbwa na masahibu gani?” Kabla ya kujibu nilitulia kwanza kurudisha kumbukumbu mara ya mwisho kipi kilichonisibu Taratibu nilianza kuvuta kumbukumbu na kukumbuka mara ya mwisho, nilikumbuka vizuri aliyonifanyia mkeo mama Gift ilionyesha wazi kuwa alidhamilia kuniua. Nilipotaka kumweleza babu nilianza kusikia maumivu ya kifua na mbavu.
''Babu...babu kifua kinaniuma.”
“Basi pumzika, hata hivyo hali yako bado taratibu itakaa vizuri mjukuu wangu.”
Babu alininywesha majani yenye ukakasi uliochanganyikana na uchungu, kisha alinipa maji mengine mekundu yenye harufu fulani ambayo sio nzuri kidogo nitapike.
''Hii dawa ndio iliyokusaidia kurudisha damu yako ulikuwa huna damu kabisa baada ya kunywa dawa babu alitoka na aliporudi alikuja na debe lililoonyesha halijui maji kwa nje na lilikuwa likifuka mvuke kuonesha maji yaliyomo ni ya moto.
Yule mzee alianza kunikanda mwili mzima pale nilipokuwa nimelazwa kwenye kitanda cha kamba alinivua nguo zote na kubaki kama nilivyozaliwa. Alinikanda mwili mzima maji yalikuwa ya moto na wakati mwingine nilipiga kelele za maumivu na kufikia hatua ya kutukana ili aniachie kwani haikuwa lazima kama maumivu ni yangu lakini hata hivyo babu hakusikia maneno yangu alinieleza.
“Binti huruma yangu ndio kifo chako.”
Alinigeuza na kunikanda sehemu za mgongoni kisha alinichua na mafuta yenye harufu mbaya ambayo alijipaka mikononi na kubanika kwenye moto na kuanza kunikanda mwili mzima kisha hunipa uji wa muhogo mweusi na viazi. Nilikuwa najiuliza yule mzee ni nani na pale ni wapi kama kwa mganga nani kanipeleka.
****
Siku zilizidi kukatika hali yangu iliendelea vizuri, kidogo nilianza kukaa chini angalau kwa nusu saa. Nilishindwa kuelewa kama pale ni kwa mganga wa kienyeji mbona sioni wagonjwa wengine zaidi ya yule mtoto aliyekuwa naye bila mama yake. Siku mmoja ilinibidi nimuulize:
"Hivi babu Utakufalini huyu ni mtoto wa nani na bibi yupo wapi maana siku zote nakuona uko peke yako?”
"Mjukuu wangu duniani kuishi kwingi si kuzeeka bali ni kuona mengi wahenga walisema kuwa uyaone ."
"Una maana gani babu?” nilimuuliza.
"Historia ya huyu mtoto ni ndefu inahitaji nafasi la muhimu kwanza ni kuangalia afya yako inatengemaa ili siku moja urudi ulipotoka."
Sikutaka kumdadisi zaidi nilitulia na kuendelea na shughuli zangu za matibabu ya kiasili ambayo sasa si mageni kwangu. Baada ya muda niliweza kusimama na kuanza kutembea lakini kuna wakati nilitembea kwa kuinama kutokana na maumivu ya mgongo.
Babu aliendelea kunihudumia kuhakikisha afya yangu inaimalika , vyakula nilivyokula havikuwa vigeni sana kwani hata kijijini nilikotoka ndivyo vilikuwa vyakula vyetu vikuu. Afya yangu baada ya muda iliimalika kiasi yalibaki madoa na maumivu madogomadogo japokuwa sehemu zangu za siri zilikuwa bado zina makovu kama nimekatwa na panga.
Babu Utakufalini baada ya kuridhika na hali yangu siku moja tulikuwa tumekaa baada ya kumaliza kula chakula cha usiku, tukiwa tumewasha majani kama taa yetu ya asili alianza kunipa mikasa mizito.
Kuwa sehemu kama ile kama una roho ndogo huwezi kukaa muda wote huo kwani ilikuwa inatisha usiku kulikuwa na wanyama wakali kama simba ambao walikuwa wanapita karibu na eneo la nyumba yetu. Lakini babu Utakufalini alikuwa ni mjuzi alisema yote mwenye nia mbaya pale hawezi kupaona alianza kunieleza jinsi alivyonipata mimi.
"Mjukuu wangu siku moja wakati nikitoka shambani nilipovuka bonde moja mbele yangu niliona gunia. Nililisogelea ili nijue kuna nini niliposogelea ndipo nilipogundua lilikuwa na damu. Nilijiuliza kuna nini ilinibidi nifungue nijue kilichomo nilishtuka kuona mwili wa binadamu japo nilishangaa lakini sikushtuka wala kuogopa kwani hali ile nilikuwa nimeshaizoea.
“Mwanzo nilikuwa nashtuka na kuogopa pale nilipokuta maiti za watu, mjukuu wangu katika pori hili kama una moyo mwepesi huwezi kukaa kuna miujiza na matukio ya kutisha. Katika kila mwezi ni lazima niokote maiti moja au zaidi.”
“ Eti ulikuwa unasema unaokota maiti moja kila mwezi hizo maiti zilikuwa zinatoka wapi?” nilimuuliza.
“Ukweli sijui lakini inavyoonekana huu msitu watu wengi wanautumia kutupia maiti za watu. “
“Kwa nini babu usipeleke taarifa polisi?”
“Mjukuu wangu we acha tu, vuta subira utaelewa tu kwa nini sikupeleka taarifa polisi?"
"Ee’he tuendelee babu ndio ikawaje?”
“Kama nilivyokueleza kuwa msitu huu hasa pale bondeni ndipo jalala la kutupia maiti za watu, kuna kipindi huwa naokota maiti mpaka tatu kwa mwezi. Basi mjukuu wangu baada ya kuona mwili wako kwenye gunia na kuulaza nje ili niuchimbie. Kilichonishangaza mwili wako ulikuwa umejaa damu sehemu moja mapajani na sehemu za siri. Lakini mwili wako ulikuwa na joto tofauti na miili mingine niliyowahi kuiokota kabla ilikuwa imesha poa. Kutokana na uzoefu wangu nikagundua hujafa bali ulikuwa umepoteza fahamu.
“ Sikuwa na jinsi ilinibidi niubebe mwili wako hadi nyumbani kwangu na kuuchunguza ambao niligundua kuwa sehemu zako za siri kulikuwa na majeraha makubwa. Kutokana na uwezo wangu wa kujua dawa za magonjwa ya siri nilianza mara moja kukutibu majeraha hayo makubwa. Ilichukua muda kurudiwa na fahamu zako ndipo siku ile nilishtuka kukuona katika hali ile nilimshukuru Mungu.
“Ndio nikaendelea na matibabu mpaka hivi leo hali yako kidogo inaridhisha nina imani siku zinavyozidi kwenda ndipo nitakapokuruhusu urudi ulipotoka."
“ Babu nashukuru sana sijui nikulipe zawadi gani ya kuokoa maisha yangu, lakini ninakuahidi utaishi maisha mazuri nusu ya peponi pale nitakapotoka kwenye msitu huu na kurudi nyumbani, " nilimuahidi mzee Utakufalini.
“Tumuombe Mungu hebu leo naomba unipe kisa cha wewe kilichokuweka kwenye hali ile ambayo kama Mungu asingenionesha mwili wako basi jina lako ulimwenguni lingepotea."
Kutokana na jinsi babu alivyonifanyia sikuwa na sababu ya kuuficha ukweli nilimweleza yote tangu mambo yaliyomsibu marehemu mama yangu kipenzi na jinsi mimba yangu ilivyopatikana na mlolongo mzima wa maisha yangu mpaka hatua iliyofikia ya kuwa pale kwake.
Babu aliniangalia na kutikisa kichwa chake kisha alinipa pole.
" Pole sana mjukuu wangu yote hiyo ni mitihani ya maisha lakini usife moyo, mama yangu alinikataza nuisilie kisasi naamini kama nitamfuata yeye mwishowe nami nitakufa kama yeye, kwa nini mama yangu hakuniruhusu kulipa kisasi?...Kwa nini mama umeniacha mwanao kwenye dunia yenye viumbe wenye roho mbaya walio tayari kuyapoteza maisha ya mwanadamu mwenzake.
Kufika hapo nilianza kulia ilibidi babu afanye kazi ya ziada kunibembeleza.
“Babu inauma sana ona sasa mama yangu ameona hali hii ya kinyama niliyofanyiwa unafikiri kuna usalama tena wa maisha yangu akiniona tena atanibakisha kama sio safari hii atanikata kichwa kabisa ili uokote kiwiwili kilichotengana na kichwa.
“ Ni kweli usemayo lakini Mungu yupo kama alikulinda na hili basi atakulinda na lingine.”
“ Babu kutokulipa kisasi ni donda ambalo litaendelea kunitesa, nina imani donda moyoni linaweza kuniua kuliko kipigo.”
“ Tujifunze kusamehe, japo tuna machungu moyoni mwetu bwana atatupa farijiko na kuyasahau maumivu yote ya mioyo yetu.”
“ Babu nitajitahidi, lakini, sijui..hasa shoga yangu sijui..sijui..sijui.”
“ Naheshimu wosia wa mama yako nina imani mzimu wake ndio unaochangia sehemu kubwa ya kuokoa maisha yako.”
“ Sina budi kufuata wosia mama sina budi kumuenzi mama yangu, mama yangu nilimpenda kuliko kitu chochote duniani ..eenhe Mungu mpe mama yangu makazi yaliyo mema kwenye pepo ya milele.”
“Najua mjukuu wangu una machungu sana yasiyoelezeka moyoni mwako muombe Mungu atakupa farajiko lenye kukufanya uyasahau.

“ Ameni..ee Mungu hebu nipe nguvu ili niweze kukujua wewe na kutimiza wosia wa mama yangu na kushinda nguvu za shetani,” pamoja na machungu nilijikabidhisha katika mikononi mwa Mungu.
“ Nina imani dua lako limesikilizwa njia pekee ni kuwa karibu na Bwana.”
Huku nikifuta machozi nilimuuliza babu Utakufalini:
“ Babu hebu nielize kwa nini umeamua kuishi katikati ya pori la kutisha namna hii tena peke yako huku ukiwa na mtoto mdogo, bibi yuko wapi kwani tangu nifike hapa sijaone mtu mwingine tofauti zaidi yetu. Vilevile Kalekwa ni mdogo sana anahitaji malezi ya mama yake.”
“Ndio maana mjukuu wangu nilikueleza awali kuwa kuishi kwingi si kuzeeka bali ni kuona mengi. Mjukuu wangu mimi nilikuwa ni mganga wa jadi miaka sita iliyopita.” “Ina maana kuna wagonjwa huwa wanafika hapa?”
“ Hapana nilikuwa naifanya kazi hiyo huko mjini ambayo ilinipatia kipato kidogo kilichonisaidia kupata mahitaji ya kila siku na familia yangu. Kazi hiyo ya kutibu watu ilinisaidia kujenga nyumba moja ya vyumba vinne ya tofali na mabati na mabanda madogo madogo ya udongo na nyasi.
“Mjukuu wangu kama ujuavyo waganya wa jadii tulivyo na tamaa kila mteja wa kike mzuri unamtaka nilijikuta naoa wanawake watano. Ndani ya miaka minane ya uganga nilikuwa na watoto kumi na tano. Siku hadi siku maisha yalianza kubadilika na kazi ya uganga ikawa ngumu wateja walipungua na maisha yakawa magumu sana na baadhi ya wanawake wakanikimbia kwa njaa nikabaki na wake wawili na watoto kumi na tano.
Kazi ya uganga niliona itaniua njaa ilibidi nitafute njia nyingine ya kupambana na maisha itakayonipatia riziki tofauti na uganga. Mungu alijalia nilipata kazi katika kanisa la palepale mjini, wengi hawakuamini mganga wa jadii aliyekuwa akiabudu mizimu kumrudia Bwana.
Nilipata kazi ya kufanya usafi na kutunza bustani eneo lote la kanisa mimi ndiye nilikuwa msimamizi mkuu. Nilizidi kumshukuru Mungu kipato nilichopata kilipunguza makali ya maisha pia wanangu waliweza kusoma. Hata hali yangu ya maisha ilikuwa nafuu kidogo nilijikuta najilaumu kwa kupoteza muda wangu mwingi kwa kutumikia nguvu za giza zilizopeleka kumuasi Mungu.
“Nilifanya ile kazi kwa miaka mitatu, muda huo niliongeza nyumba nyingine ya matofali na bati, kidogo kitambi kilianza kutoka usiseme mjukuu wangu madaraka matamu nilichaguliwa kuwa mkuu wa walinzi kanisani pale.
“Siku moja nikiwa katika ukaguzi wa bustani nyuma ya jengo la kanisa nilisikia watu wakiongea kwenye dirisha moja lililokuwa wazi nilimsikia mmoja akisema.
” Aisee usifanye kazi funga dirisha,”
Nilijiuliza chumba kile kuna kazi gani mpaka watu kuogopa kuchunguliwa, niliwasikia wakisema: tufanye chapchap ili tufanye kazi nyingine si unajua kuna damu inatakiwa kupakiwa kwa ajili ya safari ya kesho.”
“Umeshaangalia vipimo vya damu yake?” mwingine aliuliza.
“Ipo freshi.”
“Basi fanyeni kazi.”
Maneno yale yalinishitua ilibidi ninyate hadi kwenye dirisha na kuchungulia ndani sikuamini kama pale ni kanisani sehemu ya ibada kuna mambo machafu yanatendeka! Mjukuu wangu nilishuhudia kwa macho yangu mtu akinyonywa damu kwa mitambo inayotumia umeme. Nilijikuta naingiwa na woga nilijipa moyo kuwa ni lazima niujue mwisho wake. Mara taa iliwaka kwenye ile mashine ya kunyonyea damu imemaliza kunyonya.
Nilimsikia mtu akisema:
“Eeeh, bwana kazi tumeshamaliza mwiteni bosi basi.”
Alitoka kijana mmoja kumfuta bosi, mara alirudi na bosi aliyeongozana naye ndiye Pasta anayetusalisha kila siku. Mtu mwenye huruma na upendo kwa watu wote nilizivuta punzi zangu kwa taratibu sana ili zisitoe sauti nimuone Pasta atasemaje.
“ Vipi kazi mmemaliza?’
Wale vijana waliokuwa sita waliitika wote kwa pamoja, machoni ni watu wazuri ambao nawatambua vizuri
“Tayari bosi.” yeye akasema: “Ok, hii damu changanyeni na ile iliyopungua kwa ajili ya kusafirishwa kesho.”
“Sikuamini mjukuu wangu watu niliokuwa nawaona ndio mfano wa kuigwa nami kujifunza tabia zao za upole na ukarimu kumbe ni masubiani wanyonyaji, Ule mwili wa yule mtu ambaye walimnyonya damu ulichukuliwa na kuwekwa kwenye chombo kama droo ya majokofu ya monchwari.
“ Nilisikia akiuliza: “Zile ngozi zimetimia hesabu yake?”
“Ndio bosi tumekamilisha hesabu zake nina imani mzigo wa damu utaondoka na ngozi.” Yule bosi aliwajibu: Ok kazi nzuri, vijana nao walijibu: Asante, nilichokiona kingine mjukuu wangu nilijikuta napiga kelele za mshituko ni pale niliposhuhudia miili ya watu ikichunwa ngozi utafikiri nyama inayo pelekwa buchani, kelele zangu ziliwashitua.
Nilisikia wakishituka na kuuliza: "Nani tena huyo? mara nilisikia: "Mkamateni huyo haraka," Nilijua sasa pale hakuna usalama nilitimua mbio mjukuu wangu japo mwili wangu ulikuwa mkubwa na kitambi nilijikuta naruka ukuta bila ya kutegemea na kuangukia nje ya uzio.
Hivi leo mjukuu wangu ukiniuliza niliwezaje kuruka ukuta siwezi kukujibu, maisha matamu kwa vile nimetambua siri zao lazima wataniua. Hata sielewi hali iliyonikuta siku ile nilisikia haja ndogo ikinitoka na nguvu kuniishia. Namshukuru Mungu walianzia nyumba nyingine mimi nilipata upepo na kutoroka kwa kupitia dirishani. Nilijificha kwenye mti wa jirani nilishuhudia kupitia juu ya mti msako mkubwa ukifanywa uliondelea kila sehemu kwa muda wa takribani robo saa na baada ya kuridhika kuwa sipo waliondoka. Sehemu niliyokuwa nimejificha ilikuwa si rahisi mtu kuniona. Kuna dawa huitumia pale ninipokuwa na matatizo basi hiki kizizi, (huku akinionyesha na kuendelea kunihadithia matatizo yake). Basi mjukuu wangu hiki kizizi unapokuwa na matatizo yenye hatari unakiweka chini ya ulimi mtu hakuoni au anayekutafuta anakata tamaa.
Sikurudi nyumbani upesi nilisubiri kama saa moja hivi ndipo niliporudi, wake zangu na watoto wangu walishangaa na kutaka kujua kulikoni. Niliwasimulia yote niliyoyaona na hawakuamini. Niliwaeleza maisha yangu yapo mashakani ni lazima wataniua ili nisitoe siri na pia najua watanitafuta kwa udi na uvumba wakinishika ni lazima watanichune ngozi au kuninyonya damu.
“Habari zile ziliitia hofu familia yangu ambayo ilinishauri nisilale pale lazima usiku wangekuja kunifuata nilikubaliana nao na kwenda kulala msituni. Mjukuu wangu waliyonifanya Mungu anajua huwezi kuamini kwa kuelezewa tu mpaka ushuhudie mwenyewe.
Asubuhi nilirudi nyumbani ili nijue kuna nini na kupeleka taarifa polisi kwa ajili ya usalama na pia watu wale wakamatwe. Nilichokikuta mjukuu wangu eneo la nyumba zote zilikuwa zimeteketezwa kwa moto familia yangu ya wake zangu na watoto wangu kumi na tano na wajukuu zangu wawili wote walipotelea pale.”
Habari ile zilinishitua na kuufanya mwili wangu kunisisimka huku damu yangu ikichemka na nywele kunisimama. Sauti ya mzee Utakufalini ilibadilika na kuwa ya kilio na majonzi.
"Pole sana babu msiba mzito, unafikiri walifinya vile ili kuhakikisha hata kama nimejificha nifie ndani."
" Baada ya kuona tukio lile babu ulifanya nini? Mmh hapo babu ni lazima uwe mwendawazimu kufa watu 20 kwa wakati mmoja si mchezo lilikuwa ni pigo kubwa tena takatifu sijui kwa nini Mungu amewapa uwezo watu madhalimu kama yale," nilimuuliza huku macho yangu yamejaa macho na moyo kuiuma kama kidonda.

Itaendelea

No comments