Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 15


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
" Baada ya kuona tukio lile babu ulifanya nini? Mmh hapo babu ni lazima uwe mwendawazimu kufa watu 20 kwa wakati mmoja si mchezo lilikuwa ni pigo kubwa tena takatifu sijui kwa nini Mungu amewapa uwezo watu madhalimu kama yale," nilimuuliza huku macho yangu yamejaa macho na moyo kuiuma kama kidonda.
SASA ENDELEA...

"Mjukuu wangu ndio maana waswahili walisema ukishangaa ya Musa utaona ya firauni na si kwamba Mungu amewapa uwezo ili watunyanyase sisi wanyonge bali amewaacha ili siku ya hukumu wayakute maovu yao na malipo yao ni moto wa milele.
"En’he baada ya kushuhudia mauaji yale ambayo kama yangetokea enzi hizo wangeyaita sunami ulifanya nini?" nilimuuliza swali huku nilifuta machozi na kupenga kamasi nyembamba ambazo mara nyingi zilikuwa zikiambatana na machozi.
Kabla ya kujibu alinyanyuka ili akamlaze Kalekwa aliyekuwa amempakata kwa kipindi kirefu tangu tuanze mazungumzo yetu. Baada ya kumlaza ndani alirudi tena ili tuendelee na mazungumzo yetu na baada ya kukaa aliongeza majani makavu kwenye moto na kuongeza mwanga.
"En’he babu lete bahari."
"Mjukuu wangu uchungu nilioupata nilijikuta naangua kilio mzee mzima watu walinizinguka na kunipa pole ambazo zilikuwa kama zimechokonoa kidonda. Mara walitokea askari na kunipeleka kituoni kwa ajili ya mahojiano juu ya vifo vya familia yangu.
“Nilikutana na mkuu wa kituo na kunihoji nawafahamu vipi wauaji wa janga lile. Mjukuu wangu nilimweleza yote niliyoyaona jana yake kanisani na jinsi nilivyotafutwa na asubuhi niliyoyakuta.Walitumwa askari kwenda kufanya uchunguzi huku mimi nikibaki ofisini kusubiri majibu ya uchunguzi wao.
“Nilikaa kama dakika kumi hivi mara mkuu wa lile kanisa Pasta Jonasan aliingia. Alinipita na kuingia ofisini kwa mkuu wa kituo na baada ya dakika mbili walikuja vijana na kunibeba juujuu bila kuelewa nini kinaendelea.
“ Nilitupwa mahabusu bila ya kufahamu kosa langu, nikiwa katikati ya mawazo nilifuatwa na kubebwa juujuu na kuingizwa kwenye chumba kilichokuwa na giza mara taa ziliwashwa na kujikuta nimekalishwa kwenye kiti na mbele yangu kuna meza na kiti kingine.
“Ndani nilikuwa peke yangu mara mlango ulifunguliwa na mkuu wa kituo aliingia na kuniita jina langu:
"Mzee Jacob."
"Jina langu."
"Kwa nini unalidanganya jeshi la polisi?"
"Sikuelewi mkuu."
"Unaidanganya serikali kuwa kanisa lililojitolea kwa ajili ya Mungu ni wauaji, wanyonya damu na pia wachuna ngozi.”
"Sidanganyi nisemayo yana ukweli kabisa na nina ushahidi nayo,” nilisimamia kauli yangu
"Haa..ha..ha,”alicheka kidogo kisha akasema:
"Hivi huo upuuzi wako utamuuingia nani? Ni nani atakubaliana na uzushi wako yaani kanisa na watumishi wake eti ni wauaji pia ni wanyonya damu na kuchuna ngozi," mkuu wa kituo alinigeuka.
"Mkuu hata mimi ninayoongea mbele yako ningehadithiwa na mtu nisingekubali hata ningekuwa radhi kupinga uhai wangu."
"Una maana gani?”
“Watumishi wa kanisa lile wapo sawa na jeneza lililopandwa kwa nje na maua mazuri lakini ndani ni mzoga uliooza tena unaotoa harufu kali."
"Mzee JJ."
"Naam mkuu."
"Kwa nini umeiua familia yako?"
“ Ati unasemaje?” niliuliza swali kama vile sikusikia.
"Nauliza kwa nini umeiua familia yako?"
"Siwezi na hata siku moja nisingeweza kufanya hivyo hata siku moja."
"Mzee JJ acha kujitoa akili narudia tena kwa nini umeiua familia yako?”
"Mkuu huo ni utani kama huna swali bora uniache niende zangu."
“ Ulisikia wapi muuaji anaachiwa huru."
“Nani muuaji?"
“Wewe, sasa naomba unieleze kisa na mkasa uliokufanya uiue familia yako?”
“'Sikujibu niliona sasa huu ni upumbavu na uonevu yaani familia yangu iteketezwe halafu kesi inirudie mimi. Ama kweli asiyekujua siku zote hakuthamini. Sikumjibu nilibaki kimya, kimya kilipozidi aliniuliza.
''Utajibu au hujibu,” mimi nilikaa kimya.
“ Moja ' kimya ' mbili ' kimya aliwaita vijana wake walionipa kipigo kitakatifu eti niseme kwa nini nimeiua familia yangu. Nilijigeuza bubu kila walivyokuwa wakiniuliza nilipata kipigo kitakatifu kilichonitoa damu mdomoni puani na kichwani nilikuwa nimepasuka, damu zilikuwa zinanitoka sana.
Nilichukuliwa na kwenda kutupwa kwenye chumba chenye baridi kali mjukuu wangu usiombe uchungu wa kupoteza familia yangu na bado mbichi kabisa na bado nimepewa mateso mazito. Mateso na vipigo viliendelea kwa siku tatu mfululizo bila kupata majibu wanalotaka.
“Nilirudishwa rumande na kufunguliwa mashtaka ya mauaji, siku ya kwanza mjukuu wangu niliposimamishwa kizimbani sikujibu neno lolote si siri watu wote walikuwa wakinililia kuwa nimeonewa lakini hakuna aliyejali vilio vyao. Mara ya pili sikujibu kitu zaidi ya kusomewa shitaka la kuiteketeza familia yangu kutokana na hali ilivyokuwa inaendelea kwa vile nilikuwa sina wakunitetea zaidi ya wananionea huruma kuwa naonewa.
“Siku moja wakati tunatoka mahakamani katika gari tuliokuwa kumi na mbili, gari letu lilipata ajali iliyosababisha lipinduke na mlango wa nyuma kufunguka. Tuliona kama ndio wokovu wetu. Hapo mjukuu wangu sikulaza damu nilitimua mbio moja kwa moja na baadhi ya wafungwa wengine waliokuwa na majeraha makubwa walishindwa kukimbia.
“Hata mimi nilikuwa na jeraha mguuni sikujua nilikimbia vipi kuingia porini, amini usiamini nilikimbia kwa wiki nzima usiku na mchana hadi kwenye pori hili nilikuwa nina imani kama wangenitafuta kwangu watachemsha, Katika pori hili nilifika nilikuta hakuna kitu chochote ndipo nilipoanzisha maskani yangu mpaka leo hii naishi peke yangu huu ni mwaka wa nane nipo huku."
Zilikuwa habari nzito zilizonifanya mwili wangu uingie baridi na kugundua pesa siku zote zinapindisha haki na kuwa batili nilimsongelea babu Utakufalini nilimshika mgongoni nakumpigapiga kidogo wakati huo alionyesha ni mtu mwenye majonzi sana. "Pole babu nina imani Mungu kayaona yote haki ya mtu haipotei lazima itapatikana na ukweli utajulikana."
" Ni vigumu, wenye pesa wamehodhi sehemu zote ambazo wanyonge tunapokimbilia."
"Hata pesa izibe vipi ipo siku amini mwanya utaonekana, sasa hebu ona jinsi ulivyofanyiwa halafu usilipize kisasi?”
“Katu sitalipiza Mungu atanilipia."
“Kauli hizo ndizo zinazowapa vichwa wazidi kutukandamiza, babu umenieleza mengi juu ya maisha yako inavyoonekana umekuja peke yako vilevile katika maongezi yako yote sikusikia taarifa za mama wa mtoto huyu?"
"Mjukuu wangu kama nilivyolibatiza jina hili pori kuwa la mauti, Siku moja narudi kutoka shambani kwangu, nilipopita sehemu moja nilishangaa kuona kitoto kidogo kikimnyonya mama yake ambaye ulalaji wake ulinitia mashaka. Nilisogea hadi pale wakati huo kitoto kiliendelea kumnyonya mama yake.
“Hali ya yule mama ilinishtua haikuwa ya uzima, kweli nilipomsogelea karibu niligundua yule mama niseme ni msichana alikuwa amefariki. Nilijiuliza amefikaje pale na yupo na nani nililichunguza eneo lile kwa muda lakini sikuona mtu yeyote. Niliamua kumchimbia kaburi na kumzika na kumchukua huyu mtoto na kuja nae hapa kwangu.
“Japo mwanzo ilikuwa vigumu kuishi naye, kama ujuavyo mtoto mchanga aliyezoea kunyonya kwa mama yake. Lakini kuna mti mmoja ambao ukiuchemsha maji yake hayawi tofauti na maziwa ya mama yake.
“Si rahisi mara moja kuyazoea ilimchukua wiki mbili mpaka kuyazoea. Ndipo nilipoanza maisha mapya kwenye pori hili la kutisha lenye wanyama wakali na lenye vibweka kama roho yako ni nyepesi unaweza kukimbia.
“Kuna siku wakati natoka shamba niliona viungo vya binadamu kila ninavyokwenda ndivyo nakiona kimoja kimoja. Mwanzo niliokota mguu wa kushoto, mbele nikaokota mguu wa kulia mbele kidogo kichwa nusura nikimbie lakini nilijipa moyo kwani bora nifie huku kuliko kuchunwa ngozi. Mara ya mwisho kabisa niliokota kiwiliwili, kama kawaida yangu nilivizika.”
“Yaani nashngaa ina maana serikali hawajui haya?" niliuliza huku nimeshikilia kifuani.
"Basi mjukuu hii ndio historia ya maisha yangu na Kalekwa."
"Jina la Kalekwa ulilitoa wapi wakati ulikuta mama yake ameshakufa?"
"Ndio maana nikamuita kalekwa yaani kaachwa nina imani alikuja bila kitu."
“Siku zote Mungu humpa unafuu kiumbe wake, katikati ya pori hili nilikuta mabaki ya ndege yaliyoanguka zamani kutokana na hali yake nina imani waliyaacha."
“Sasa babu nazidi kukuhaidi utaishi maisha mazuri nusu ya peponi."
"Nitashukuru mjukuu wangu na nimechoka kuishi maisha ya porini kama mnyama sina wa kuongea naye zaidi ya mjukuu wangu Kalekwa na wanyama wakali yaani nikitoka nje kidogo najiona kama binadamu kamili ninayeweza kuongea na binadamu wenzangu.”
"Babu poza moyo naona usiyahesabu kuwa ni matatizo muda si mrefu yatafika ukingoni, “nilimuyajidi babu maisha mazuri baada ya kurudi mjini,
"Nitashukuru mjukuu wangu nakuombea kwa Mungu upone kwa haraka."
Kwa vile usiku ulikuwa mkubwa tuliingi kulala. Siku zilivyozidi kwenda ndivyo hali yangu ilivyozidi kuwa kuimalika. Babu Utakufalini aliporidhika na hali yangu alinipangia siku ya kuondoka. Nilikubaliana na babu niondoke peke yangu ili kama nikirudi nirudi na gari kuwachukua wote. Yaani kwa muda ule sikujua nimekaa porini kwa muda gani.
Usiombe yaani lile pori kweli ndio maana mzee Utakufalini alijibatiza jina Atamjua nani, kweli unaweza kuzaliwa pori lile ukazeekea kule na watu huwajui wala kuonana na mtu zaidi ya wanyama na ndege.
Unaambiwa kutoka pale porini hadi kuishika barabara ni mwendo wasaa 36 na ukiwa legelege siku tatu hadi kufika barabarani. Siku niliyopanga na babu Utakufalini ilipowadia . Niliamka alfajiri kwenda kumuaga , ili nianze safari ya alfajiri nilipanga lazima nifike barabarani jioni ya siku ya pili.
Nilipokwenda chumba cha babu Utakufalini nilimsikia akikoroma tena mkoromo mzito. Ile hali sikuwahi kumuona nayo kipindi chote nilichokuwepo pale. Nilizidi kumwita lakini sikupata jibu lolote zaidi ya mkoromo kuendelea. Niliamua kuingia chumbani kwake nilimkuta macho yamemtoka pima.
Ile hali ilinitisha wakati huo Kalekwa naye alikuwa ameamka, nilimtenga akajisaidia kisha nikarudi kwa babu utakufalini. Hali yake ilinisikitisha kwa vile na mimi nianza kuwa mjuzi wa miti shamba, mara moja nilikoka dawa yaliyoweka moshi mwigi baada ya dakika tano babu Utakufalini alitoka jasho jingi kidogo hali yake ikawa afadhali.
Ilibidi nivunje safari ili nimhudumie babu na Kalekwa.
Pamoja na babu kupata nafuu lakini alikuwa hawezi kazi kwa kipindi kile. Ilinibidi shughuli zote nizifanye mimi. Suala la safari nililisitisha kwa muda , mtoto wa kike nikavaa rasmi kazi ya babu Utakufalini.
Ikawa asubuhi naingia kutafuta kuni na kushughulikia kilimo kilichoachwa na babu. Nilijikuta namaliza miezi mitatu bila kutegemea. Siku moja niliporudi shamba nilikuta mwili wa mtu aliyekufa. Nilikimbia mbio hadi nyumbani babu alishangaa na kuniuliza kulikoni nilimuelezea nilivyoona.

ITAENDELEA

No comments