Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 16


 
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
ILIPOISHIA:
Ikawa asubuhi naingia kutafuta kuni na kushughulikia kilimo kilichoachwa na babu. Nilijikuta namaliza miezi mitatu bila kutegemea. Siku moja niliporudi shamba nilikuta mwili wa mtu aliyekufa. Nilikimbia mbio hadi nyumbani babu alishangaa na kuniuliza kulikoni nilimuelezea nilivyoona.
SASA ENDELEA...

“Basi mjukuu wangu hayo ya kawaida la muhimu uufukie ule mwili .“
“Hapana babu wanaweza kuniua.”
“Kama kufa ningekufa mimi huu ni mwaka wa nne nipo huku na nishazika watu si chini ya mia mbili rudi ukazike mjukuu wangu.”
“ Hapana babu sirudi,” nilikataa.
“Usiogope kumbuka usipouzika utajiletea matatizo.“
“Matatizo! Matatizo gani?”
“Ule mwili ukioza patakuwa hapakaliki harufu ya mwanadamu ni kali sana.“
Nilijipa moyo nikarudi kuuzika mwili wa yule mtu alikuwa msichana, nilishangaa alikuwa amevaa hereni na mkufu wa bei mbaya nilijiuliza ina maana waliomuua shida yao ilikuwa ni nini? Nilichimba na kuufukia ule mwili .
Tangu hapo nikaanza kuwa na moyo wa ujasiri nilishangaa woga ulinitoka hata nilipokuta mwili mwingine niliufukia bila hofu yoyote. Siku moja nilirudi kutoka kwenye kilimo chetu, tena siku hiyo nilikuwa nimekamata kware nilijua babu Utakufalini atafurahia na kuona nimeanza kumrithi katika uwindaji.
Nilimkuta Kalekwa analia babu alikuwa amelala tu, si kawaida yake kumuacha Kalekwa alie kiasi kile. Nilipofika nilimnyanyua na kumbembeleza, baada ya kunyamaza nilimfuata babu Utakufalin. Nilishangaa kumkuta amelala wakati mjukuu wake alikuwa analia. Nilimuamsha alifumbua macho lakini macho yake yalikuwa mazito.
“Babu vipi?”
“Ha…a…a…a….apa..na,” aliongea kwa shida .
“Babu nimerudi, tena leo nimekuletea kitoweo.“
“Thereza,“ babu aliniita kwa sauti ya chini.
“Abee babu,” niliitaka huku nilimuinamia ili nimsikilize vizuri.
“Mtu …nze..Ka..le..kwa.”
“Ba..bu..vipi?”
Babu alinyoosha mkono aliokuwa ameukunja ngumi na kunipa kitu nilipokea hakikuwa kingine zaidi ya kile alichonionyesha na matumizi yake. Nilipokipokea tu swali la jina jina lake kuwa atakufa lini ilitimia, baada ya kupokea kile kizizi babu alikata roho.
Nilishindwa kulia japo roho iliniuma ,yaani dhamira yangu ya kulipa fadhila iliyeyuka kama donge la mafuta kwenye kikaango cha moto. Nilitamani kulia lakini nilijikaza, najua udhaifu ninapolia hasa msiba uwe unanihusu. Kwa kiasi gani babu Utakufalini alivyookoa maisha yangu nilijua kilio changu cha kawaida lazima nitapoteza fahamu kitu kitakachomfanya Kalekwa apate shida.
Nilijikaza kiume na kuchimba kaburi kisha niliuzika mwili wa shujaa wangu mzee Jacob au maarufu kama Utakufalini mtu aliyekufa kifo kama mnyama kutokana na roho mbaya za watu wanaoonekana nje kondoo lakini ndani ni wanyama wakali kushinda mbwa mwitu.
Niliuzika mwili wa mtu muhimu maishani mwangu, roho iliniuma lakini ndio hivyo Mungu amemuita. Mimi nilimpenda lakini yeye alimpenda zaidi. Baada ya mazishi siku ya pili alfajiri nilianza safari kurudi mjini njia ya pori na pori kutafuta barabara. Ungeniangalia ungesema labda ni mzuka jinsi nilivyokuwa na Kalekwa, tulikuwa na nywele ndefu utafikiri mizimu iliyofufuka, miili yetu ilikuwa imepauka na vumbi jingi. Nguo zetu chafu na zilizochanika zilituweka nusu uchi, nilianza safari ambayo kidogo ilikuwa ngumu.
Nilimbeba Kalekwa mgongoni kuanza safari nisiyojua naelekea wapi. Pori lilikuwa linatisha niliweza kupishana na wanyama wakali kama Simba, Chui, Tembo hata Vifaru. Kizizi nilichopewa na babu ndicho kilichonisaidia kusafiri salama, nilisafiri saa kumi na mbili nilipumzika na mdogo wangu Kalekwa kupata chakula na kujilaza hadi siku ya pili.
Siku iliyofuata alfajiri niliianza safari yangu, nilitembea kwa muda wa siku tatu hadi kukutana na barabara kuu ya magari. Tulipokuwa tunakaribia barabarani nilisikia watu wakiongea.
" Eeeh bwana jisaidie haraka tunataka Dar tufike saa nne usiku."
Nilibadili njia na kutokea upande mwingine lakini si mbali nao, mbele nilikuta lori la mizigo. Nilimshukuru Mungu kimoyomoyo nilitaka kuwaomba lakini hali yetu kama mizimu iliyofufuka nani angetukubalia au wangetaka kutuhoji na kutufikisha polisi niliona mambo yanaweza kuwa kama ya mzee Utakufalini afanyiwe ukatili ategemee polisi wamsaidie ndio kwanza wanamkandamiza na kumbambikia kesi nzito ya mauaji.
Niliamua kutumia ukomandoo wangu kama ndani ya sinema, nilinyata taratibu na kuwazunguka na kwenda kupanda nyuma kwenye mizigo. Muda si mrefu safari ilianza. Nilimuomba Mungu anifikishe salama. Dua yangu ilisikiliozwa tulisafiri bila tatizo gari liliingia Dar saa 4.30 usiku.
Kama kawaida yangu niliruka kwenye gari lilipokuwa limesimama taa za barabarani za maeneo ya Ubungo. Nilianza safari ya kuelekea kwangu, nilifika kwangu majira ya saa kumi alfajiri. Niligonga geti mlinzi alihoji kabla ya kufungua, nilimweleza ni mimi. Alipofungua alishangaa hali niliyokuwa nayo kwanza alinikatalia katakata kuwa si mimi. Baada ya kumuelewesha aliniruhusu kuingia ndani.
Alitaka kujua nini kilichomsibu hadi kuwa kwenye hali ile nilimweleza aniache nipumzike kwanza. Niliingia hadi ndani cha kwanza niliyesimama mbele ya kioo nilikuwa sina tofauti na mabush man. Kabla ya yote nilijipiga picha mimi na Kalekwa ili niweke kumbukumbu kwenye maisha yangu.
Nimekubali maneno ya babu Utakufalini kuwa tembea uone na kuishi kwingi kuona mengi. Baada ya kupiga picha kadhaa za ukumbusho ambazo ni hizi,” Malaika Mweusi alivuta droo na kutoa bahasha ambayo alimpa Anderson ambaye alizitazama na jinsi walivyokuwa kama wanyama.
Baada ya kuzitazama kwa muda alimrudishia bila kusema neno, Malaika Mweusi akaendelea:
“ Basi niliingia bafuni kuoga na kumwosha Kalekwa kisha tulijitupa kitandani na usingizi mzigo ulitupitia. Kutokana na uchovu niliamka siku ya pili saa kumi jioni kwa msaada wa Kalekwa aliyehi kuamka. Niliamka mwili ukiwa umechoka na njaa ilikuwa unauma kama kidonda, nilipiga simu Shoprite watuletee chakula.
Vilevile niligundua akili ya Kalekwa ilikuwa ya kiporipori kama angeendelea kuishi porini angekuwa kama mnyama. Kila kitu kilikuwa kigeni wakati huo alikuwa na miaka miwili. Umri wa Kalekwa ulinijulisha kumbe nilikaa kule porini kwa miaka miwili.
Baada ya kujirudisha hali ya ubinadamu, Sikutaka kupoteza muda lilikwenda moja kwa moja kwa Doctor Ray. Aliponiona hakuamini alinikumbatia kwa furaha. Hakuficha furaha yake na kuniuliza.
"Ulipotelea wapi Mr embo afadhali umeonekana kuna kazi inawaumiza akili watu, nina imani ufumbuzi ni wewe kama utaifanya vizuri malipo yake nina imani ni makubwa si chini ya bilioni moja."
"Kazi gani hiyo yenye pesa nyingi hivyo?”
Habari hizi zilinishtua ni kazi gani tena hivyo yenye malipo mazito pesa ambazo sikuwaza kuzipata maishani bilioni mia moja, mmh hapana ni kazi gani hii ambayo imesababisha moyo upasuke kwa mshtuko.
"Ray ni kazi gani hiyo yenye malipo kama hayo ambayo naona kama ndoto, au umekosea kusema?" nilishtuka.
"Hapana Thereza malipo ya kazi ni bilioni 100 kama utakubali advance shilingi bilioni 60 pale utakapo kuwa tayari kuifanya."
"Mmh! Mbona unanitisha ni kazi gani?"
"Utaelewa tu, vipi ulisafiri?"
“We acha niliyonikuta Mungu anajua nahitaji msaada wako mwingine,” nilimwambia Dokta Ray.
"Unashinda gani? Sema tu nipo tayari kukusaidia kwa hali na mali."
"Twende ofisini kwako," niliongozana na Dokta Ray japo yeye anapenda nimwite Mr Ray hadi ofisini mwake.
Nikiwa ofisini mwake aliniletea glasi iliyo jaa whisky ilikuwa miaka miwili imepita bila kutumia kilevi chochote. Sikuwa na haja tena ya kuendelea kunywa pombe kali.
Nilijua ule ndio wakati muafaka wa kuacha pombe kali ikiwezekana kuacha kabisa unywaji wa pombe. Nilimtaka radhi Mr Ray.
"Samahani Mr Ray situmii pombe."
"Hata bia?"
"Pombe ya aina yoyote."
“Ooh! Sasa itakuwaje na kwenye friji yangu kuna maji tu."
"Maji yanatosha sana," alinijazia maji kwenye glasi baada ya kukaa na kuitengeneza sauti yake alisema:
"Ehe...Thereza kwanza habari za siku?"
"Mbaya."
"Mbaya! Una maana gani?"
"Ndio maana nimerudi tena kwako.”
“Nina imani unakumbuka vizuri sababu iliyonileta hapa mara ya kwanza?"
"Ndio nakumbuka vizuri, kama sikosei ni tukio la kubakwa."
"Sawasawa kabisa."
"Vipi umebakwa tena?"
"Bora ningebakwa nikajua moja.”
“Sasa umepata masahibu gani?”
Nilianza kumwelezea kisa chote kilichonitokea mwanzo hadi siku ile nipokuwa mbele yake kama golikipa aliye okoa penati za Ziraili.
Habari zile zilinisisimua Dl Ray mpaka rangi yake nyeupe kuwa nyekundu. Aliniangalia mara mbili mbili kisha alishusha pumzi na kusema:
“Pole sana Thereza, wewe ni mwanamkae wa shoka, nina imani kwa hatua zote ulizopitia hautasita kuifanya kazi yetu.”
"Dk Ray niweke wazi ni kazi gani? Mbona moyo wangu unalipuka."
"Kwanza kabla sijakueleza ni kazi gani la muhimu kuishughulikia afya yako."
Niliongozana na Dk Ray hadi chumba cha uchunguzi na kuyachunguza makovu yangu sehemu za siri yaliyoniweka kwenye shepu mbaya.
Baada ya uchunguzi tulirudi ofisini kwake, aliniacha kidogo na kuingia kwenye chumba kimoja. Baada ya dakika kama tano alirudi na bahasha kubwa kidogo pamoja na kitabu kikubwa na kuviweka mezani.
Alinieleza nizunguke upande wake, baada ya kufanya hivyo alinifungulia kile kitabu kilichokuwa na picha za watu wenye majeraha na makovu ya kutisha na picha zingine wale watu wakiwa wamepona.
Kisha alinitolea picha za kawaida na kunionyesha watu waliopata matibabu kwenye hospitali yake walioungua moto lakini baada ya matibabu ya ngozi zao hurudi kwenye hali ya kawaida.
Vilevile watu wenye makovu ya kutisha waliofanyiwa upasuaji pale na hali zao zilivyo kuwa nzuri, huwezi kuamini kama hapo awali alikuwa na jeraha au kovu.
"Sasa Ther eza kazi yako ni ndogo nitaifanya kwa wiki tatu utakuwa mzima kabisa, kwa maelezo yako yule mzee aliyeokoa maisha yako dawa zake zilifanya kazi kubwa bila hivyo lazima ungekufa au kuoza kizazi mpaka utumbo kazi yangu ni upasuaji mdogo kuna dawa za kuponyesha kidonda kwa wiki kunakuwa kumepona vilevile kuna dawa za sindano zinazo kausha kidonda kabla ya kupakwa dawa juu ya kidonda ambayo hugeuka ngozi, ninajua utashangaa jinsi utakavyopona."
"Nitashukuru sana, sijui gharama zake ni shilingi ngapi?”
"Hapana sihitaji pesa yako zaidi ya kunikubalia kuifanya hiyo kazi."
"Usiwe na wasiwasi sitakuangusha kwa vile wewe ni mtu muhimu sana kwangu nina imani nitaifanya hiyo kazi bila pingamizi," nilijikuta nakubali bila kujua ni kazi gani.
"Waawoo Thereza katika siku uliyonifurahisha ni leo na mimi nakuahidi kukupa ushirikiano wa kutosha," Dk Ray alifurahi sana bila kujua sababu ya furaha yake na kazi anayotaka kunipa.
"Nitashukuru."
"Sasa sijui matibabu tutaanza lini?"
"Nilipendelea hata leo lakini kwa vile nina mdogo wangu ambaye hajuani na mtu yeyote lazima nimtengenezee mazingira mazuri kesho kutwa nitarudi kwa ajili ya matibabu.
Niliamua kuagana na Dk Ray ili nizungukie miradi yangu kujua maendeleo yake baada ya kutoweka kwa miaka miwili na ushee si mchezo unaweza kukuta mabadiliko makubwa.
Kabla ya kuagana Dk Ray alinieleza nisubiri kidogo alinyanyua simu moja, machoni kwangu ndio mara yangu ya kwanza kuiona. Ipo kama radio call, lakini ni ndogo sawa na simu za kawaida.
"Haloo mkuu yule mtu ameonekana.”
“Nani huyo?” kwa vile ilikuwa sauti inayosikika nilisikia maongezi yao.
“Thereza."
“Thereza ndio nani?"
"Yule msichana wa kazi ya PT."
"Ooh. samahani si unajua mambo mengi vipi amekubali?”
"Ndio amekubali.”
"Vizuri sana yupo tayari kuianza kazi?"
"Ndio nimekutana naye, vilevile ana matatizo anahitaji msaada wetu japo yeye mwenyewe yupo tayari kujilipia."
"Vizuri, anatatizo gani?"
Dk Ray alimweleza mtu wa upande wa pili tatizo langu.
“Ooh, siyo tatizo hakikisha anapata matibabu ya hali ya juu ya yatayomponyesha vizuri, nina imani unaelewa umuhimu wake?”
"Ndiyo bosi."
“Sasa, kwanza hata sijui niseme nini yaani kupatikana kwa binti huyo kumenipa matuini ya ajabu najishangaa hata furaha imemjaa ghafla nina imani binti ataifanikisha vizuri na mhakikishia akiifanya vizuri nitamuongezea bilioni 30 kama asante, matibabu anaanza lini?"
"Kesho kutwa bosi."
"Vizuri mpe shilingi 150 ili zimsaidie kipindi cha matibabu yake."
“Sawa bosi."
“Hakikisha vitu muhimu vinakuwa tayari ili amalizapo matibabu aanze kazi mara moja.''
“Hamna tatizo bosi."
“Ok bai kazi njema."
Baada ya maongezi Dk Ray alishusha pumzi nzito kisha alisema:
"Thereza subiri," aliingia tena kwenye kile chumba na kurudi na mfuko mkononi aliuweka juu ya meza na kuufungua.
Ulikuwa na maburungutu ya pesa zilizokuwa zimefungwa mafungu matano.
"Hizi ni milioni 150 unaweza kuzihesabu."
"Za nini zote hizi?"
“Nina imani miaka miwili uliyoipoteza umepoteza na kipato chako hivyo zitakusaidia wakati wa matibabu."
"Sawa, lakini ni nyingi sana wakati kazi yenyewe bado sijaifanya," pesa zile zilinitisha.”
"Sawa, wacha nikapumzike ili nihakikishe namtengenezea mdogo wangu mazingira mazuri kipindi chote nikiwa katika matibabu yangu," nilisema huku nikizirudisha zile pesa kwenye mfuko ili niondoke zangu.
“Zihesabu ili uzihakikishe.”
“Sina wasi wasi nawe nakuamini," niliubeba mzigo wangu na kuagana na Dk Ray.
Nikiwa narudi Dar nilijawa na mawazo mengi juu ya kazi nitayopewa, nilijiuliza ni kazi gani hiyo ambayo wanamwaga mamilion hata bila wasiwasi wowote.
Niliamua kuachana na mawazo juu ya kazi hiyo kwani kuwaza sana niliona ni kuiumiza akili yangu kwa kitu nisicho kijua.
Niliamua kuachana na kazi ya kuiwaza kazi hiyo ili kusubiri mpaka hapo nitapo elezwa ni kazi gani. Lakini ajabu kila nilipoiwaza kazi hiyo moyo ulinilipuka na kujawa na hofu moyoni. Lilibakia swali kichwani juu ya kazi ninayotaka kupewa.
Malipo billioni 100 advance bilioni 60 pesa za matumizi nje ya malipo milioni150.
Kwa upande mwingine nilijilaumu kukubali bila kuijua, nilijiuliza kama nikiikataa je itakuwaje. Wasiwasi wangu ulikuwa katika kukosa matibabu ambayo yalikuwa muhimu kwangu kuliko kitu chochote.
Nilijiuliza kwa nini niendelee kuumiza akili yangu na kuisubiri kazi hiyo watakayonipa. Wakati huo nilikuwa naaingia kwenye geti la moja ya makampuni yangu.
Siku hiyo nilizungurukia miradi yangu yote , nilimshukuru Mungu kukuta maendeleo vizuri vilevile niliwatembelea washirika wenzangu niliokuwa nao wakati wa uchokoraa.
Nao waliendelea vizuri waliponiona walifurahi sana kuniona nami vilevile nilifurahi. Siyo siri kila ninapowaona washirika wenzangu nlikumbuka mengi kweli maisha yanabadilika.
Tabu za kushinda juani ndizo zinazo niumiza roho sikuwa tayari kuona ombaomba au watoto wanaozurura mitaani. Nazidi kumshukuru Mungu hali ilikuwa inaridhisha japo ripoti ya mikoani ilinifanya niongeze vituo vingi vya watoto.
Nilipanga pesa nitayoipata kwa ajili ya kazi ambayo siijui robo ya pesa hizo ambazo ni bilioni 25 billioni 10 kuongeza vituo na shule pamoja na billioni 15 kujenga kiwanda kitachoongeza ajira kwa vijana.
Baada ya ziara yangu iliyoonyesha mafanikio makubwa pamoja na ongezeko la misaada ya wahisani iliyofikia dola millioni moja. Nilimkabidhisha Kalekwa kwa mlezi ambaye atamlea kipindi chote nitakuwa katika matibabu.
Matibabu yangu yalikwenda vizuri, ndani ya wiki tatu nilikuwa mzima wa afya njema kabisa sikuwa na kovu lolote mwilini kwangu. Kweli nimeamini dawa zipo.
Baada ya matibabu na mapumziko ya wiki mbili zingine, niliitwa ofisini kwa Dk Ray ambaye alinijulisha kuwa nijiandae safari ambayo ingekuwa baada ya wiki.
Ilikuwa kwa ajili ya mazoezi ya mwaka mzima kabla ya kuianza kazi ambayo ilihitaji mafunzo ya hali ya juu.
Nilikabidhiwa milioni 500 kwa ajili ya kuacha nyumbani kama kuna mtu anamtegemea. Sio siri kila muda na dakika nilijiuliza ni kazi gani yenye mafunzo ya mwaka mzima.
Baada ya kurekebisha mambo yangu niliwasili Kibaha kwa ajili ya safari ya mwaka mzima nisiyo jua na kwenda wapi. Majira ya saa moja usiku nilipakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruser V8 na safari ilianza. Ilikuwa safari ya kurudi Dar.
Lakini kabla ya kuingia Dar nilifungwa kitambaa usoni nilipouliza niliambiwa ni mwanzo wa mazoezi. Nilipandishwa ndege nikiwa nimefungwa kitambaa usoni. Ndani ya Ndege wakati ikiwa angani nilifunguliwa kitambaa usoni.
Ndani ya ndege kulikuwa na watu zaidi ya hamsini kila mmoja alikuwa kimya.
Tulisafiri kwa muda wa siku mbili. Siku ya pili ndege ilitua ilikuwa ni usiku wa manane, tuliteremka sikujua ule ni mji gani hata nilipo wauliza wenzangu nao walisema hawajui lakini ni moja ya nchi za Ulaya.

Itaendelea

No comments