Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 18


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
ILIPOISHIA:
"Thereza usifanye hivyo basi sema unataka kiasi gani zaidi ya Bilioni 100 sema tupo tayari kukupa."
“Father Gin nielewe, ukitaka tuongelee habari ya kazi uondoe unafiki ndani ya kundi lako hapo tutakuwa tayari kuifanya kazi yako."
"S...sa....asa..."
"Hakuna cha sasa fanyia kazi niliyo kueleza kwaheri."
Nilinyanyuka na kuondoka bila kugeuka nyuma. Wote walibakia midomo wazi, nilitoka hadi ofisini kwa Dk Ray.
SASA ENDELEA...
"Vipi mmemalizana?"
"Sifanyi kazi ya kitoto."
"Mbona sikuelewi?"
''Unajua hao sijui mabosi wako wanathamini masirahi yao kuliko uhai wa mtu ambaye ndio muhimu kuliko kitu chochote.”
"Teddy mbona unazidi kunichanganya."
“Sikuchanganyi bali ninyi ndio mnataka kunichanganya.”
"Kivipi?"
"Kinachotokea kwenye kundi kama sio kugeukana ni nini iweje mtu auawe kabla ya kazi ni nani aliye toa siri kama sio ninyi kwa ninyi, mnataka mnimtoe sadaka?”
"Wacha woga nina imani mafunzo yaliyokutoa woga."
"Sio kwa mtindo huu."
"Kwa hiyo?"
"Kazi siifanyi na gharama zenu zote nijulisheni ni kiasi gani ili niwalipe," nilisema kwa jeuri.
"Thereza ni kweli usemayo lakini ni mapema sana fikiria mara mbili"
"Kwanza Ray wale vijana mliowaandaa kwa ajili ya kuvuna damu na ngozi wapo wapi?"
"Wapo kijiji cha Farijika."
"Mnawavuna toka vijijini?"
"Kapana."
''Mnawatoa wapi?"
“Sasa hivi tuna muundo mpya wa kupita vituo vyote vya kulelea watoto wa mitaani na kukusanya wale wakubwa kwa kisingizio kuna chuo tumeanzisha kwa ajili ya stadi za kazi. Tukiwachukua baada ya muda huvuna damu na ngozi."
"Ooh vizuri wacha niende."
“Sasa vipi kuhusu hiyo kazi?"
"Tafuteni mtu mwingine."
"Thereza usicheze na Father Gin utakufa kifo kibaya."
"Hiyo itakuwa kesi nyingine.''
Nilimuacha Dk Ray macho yamemtoka pima, niliingia kwenye gari langu na safari ya mjini ilianza. Nikiwa njiani nilikuwa na mawazo mengi juu ya miradi haramu ya Father Gin na kikundi chake mtu niliyekuwa namheshimu kutokana na tabia yake ya upole ukarimu anayejali watu kumbe ni subiani mkubwa mnyonya damu za watu.
Roho iliuma kuona kumbe vijana wadogo wanakusanywa wakidhani wanapewa misaada kumbe ni mavuno yao ya damu na ngozi. Suala la kuwakusanya vijana ili kutengeneza vuno la damu na ngozi toka kwenye vituo vya kuletea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu liliniumiza kichwa.
Lilifanya mwili usisike na kuona hata katika vituo vyangu vya kulelea watoto wa mtaani wameisha nyofoa baadhi ya vijana wangu kwa kisingizio cha kuwapa stadi za kazi. Mwili ulinisisimka nikaona kuna umuhimu kuwaita wakuu wote wa vituo vyote vilio chini yangu niwaulize ni watoto wangapi wamechukuliwa.
Najua utajiuliza nini hatima yangu ya kukataa kuifanya ile kazi na kulikataa donge nono la bilioni 100. Wasiwasi wangu ulikuwa ni uamuzi wa Father Gin juu yangu. Kukataa kule nilikuwa na maana yangu tulia utaijua sasa hivi.
Mafunzo ya mwaka mzima yalinijenga kimwili na akili, niliamua kurudi nyumbani
kwangu kupumzisha akili. Nilipofika nyumbani nilioga kula na kulala ili kujipumzisha akili. Simu ya getini alilia nilinyanyuka na kuipokea.
"Unasemaje Joe?" nilimuuliza mlinzi wangu mtiifu.
"Kuna wageni."
"Waulize ni kina nani," nilimsikia akiwauliza:
"Madamu ni Father Gin na Doctor Ray."
Kusikia vile nilishtuka kidogo, baada ya kushusha pumzi nilimjibu:
"Waruhusu,” nilijinyanyua kitandani na kuelekea bafuni kuondoa uchovu kisha nilirudi chumbani na kujifunga koti langu jepesi la kulalia na kuteremka chini kuonana na wageni wangu. Niliwakuta sebuleni, nilipo waona niliwakaribisha kwa tabasamu pana.
"Karibuni sana."
"Asante sana." walijibu kwa pamoja.
"Sijui wageni wangu mnatumia vinywaji gani?" niliwauliza.
"Mimi hapana," alijibu Father Gin.
"Hata mimi nashukuru."
"Haya kama hamtaki leteni habari najua mna mengi nyuso
zenu zinajionyesha,” niliwauliza swali kwa vile nilijua lazima kile kitu kitatokea.
"Ni kweli, uamuzi wako sikuutegemea umenichanganya sana," alisema father Gin.
"Wa kuchanganyikiwa ni wewe au mimi ambaye ndiye unaye ninadi uhai wangu kwa bei nafuu."
“Sema chochote utakavyo ili tu kazi yangu ifanyike."
"Sio kwamba kazi sitaifanya.”
"Ila?"
"Pale nimeikataa makusudi lazima uelewe wenzio wanakuzunguruka we hujiulizi kwa nini siri inavuja?" nilimpa siri ya kukataa mbele ya wenzake.
“Kwa hiyo unataka kusemaje?"
"Kazi ipo palepale, ilibidi nilikatae ili kama kuna msaliti ajue sitaifanya japo najua bado nitafuatiliwa ili nitolewe uhai."
"Kazi nitaifanya ila nataka maelezo kamili ya adui zangu picha zao na wanaishi wapi ili kazi ianze mara moja."
"Ooh! Siamini maneno yako kweli wewe umetuzidi akili kwa kulijua tusilo lijua, vipi kuhusu mkataba?" aniuliza Father Gin.
"Kesho kama kawaida nitapofuata maelezo ya kazi kama ulivyo nieleza mambo yote anayo Dk Ray."
"Hamna taabu, siku njema."
"Nanyi pia," niliagana nao nami nilirudi ndani kujipumzisha.
Asubuhi siku ya pili niliamka na kwenda kibaha. Nilipofika bila kuchelewa nilipewa maelezo ya adui zangu picha zao na ramani ya miji wanayokaa. Niliingia mkataba wa shilingi bilioni 100 pale nililipwa bilioni 60 taslimu. Nilipotaka kuondoka Dk Ray alinieleza mengine mapya.
"Thereza kutokana na mapenzi mazito juu yako imebidi niuweke rehani uhai wangu."
“Una maana gani?"
"Kuna siri moja ambayo kila nikikuangalia moyo unaniuma hivyo nipo tayari kufa kwa ajili hivyo, nipo tayari kufa kwa ajili yako....najua nitahatarisha maisha yangu sina budi
kukupa siri hii."
Kauli na Dk Ray ilinishtua na kujiuliza ni siri gani itayo hatarisha maisha yake.
''Dk Ray ni siri gani hiyo mbona unanitisha?”
"Thereza hapo si sehemu yake nitakuja kwako usiku ili nikupe siri ambayo nina imani
inaweza kuchukuwa uhai wangu."
“Hakuna taabu nitakusubiri kwa hamu.”
Niliagana na Dk Ray na kurudi Dar. Nilipita vituo vyote kuchukua taarifa ya watoto walioingia na waliotoka. Baada ya kufika nyumbani nilipitia taarifa zote za vituo vilivyo chini yangu. Moyo ulinipasuka kukuta watoto zaidi ya watoto tisini wamechukuliwa na Father Gin kwa ajili ya kuvuna damu na ngozi.
Nilijiapiza kuwa si watoto wangu tu hata hao wa vituo vingine nitahakikisha
hawanyonywi damu na kuchunwa ngozi. Nilijua mimi ndiye mwenye dhamana ya
kuokoa uhai wao. Nilipanga kabla ya kuondoka nitamdanganya Father Gin
tuwatembelee watoto ili niwaone vilevile kujua mandhari yake iko vipi ili nijue
jinsi ya kuwakomboa.
Siku ile saa nne na nusu usiku Dk Ray alifika nyumbani kwangu. Nilimkaribisha sebuleni, nilimkaribisha kinywaji kikali ambacho nilikiandaa kwa ajili yake.
"Karibu sana Dk Ray.”
"Asante sana mrembo."
Tukiwa tunapata vinywaji yeye vinywaji vikali mimi nilikuwa na malta guiness.
"Dk Ray nina imani una siri nzito moyoni mwako ambayo unaonyesha wazi imekunyima raha toka ulipotamka suala la siri bado uso wako unaonyesha hofu fulani moyoni mwako."
''Ni kweli Thereza."
"Ni siri gani hiyo?"
"Thereza,"aliniita jina langu kwa sauti ya chini huku akifuta mdomo yake kwa mkono.
"Abee."
Baada ya kushusha pumzi na kunywa nusu glasi ya whisky kwa mpigo alisema.
"Thereza kwanza elewa nakupenda zaidi ya kupenda nataka kwanza uelewe hilo."
"Nashukuru kwa kunipenda," nilimjubu kwa sauti ya upole.
"Thereza wala si utani ni mapenzi yangu ya chini ya moyo wangu."
“Nashukuru nami nakupenda pia.”
"Sasa Thereza upo tayari kuwa na mimi?"
“Si tatizo ni suala la maamuzi tu hilo usihofu."
"Thereza japo nina imani penzi langu kwako sitalifaidi."
"Kwa nini?”
"Kifo kipo mbele yangu."
"Una maana gani kusema hivyo?"
Wakati huo Mr Ray alikuwa akibugia whisky kwa pupa hata sauti yake ilionyesha ameanza kulewa.
"Si unakumbuka vizuri kiapo ulicho kula kwenye mkutano?"
''Ndiyo."
"Walisema hawatasita kumuua mtu yoyote atayetoa siri ya kikundi?"
"Sasa mimi si mwanachama wa kikundi siri itakuwa ndani ya kikundi."
"Thereza hiki kikundi nakijua mimi vizuri, zipo siri zinazojulikana na zipo siri sirini
ambazo tunazijua sisi tu."
"Mmh, siri sirini?"
"Ndiyo Thereza, kama nikikueleza na wakijua lazima wataniua.”
"Basi haina haja ya kunieleza siri itayohatarisha maisha yako."
"Kama nitakaa kimya itahatarisha maisha yako."
''Maisha yangu! Kivipi?”"
"Eeh, ndiyo."
"Mungu wangu ni siri gani hiyo unayofanya mwili wangu kusisimka na kujawa na hofu kubwa?"
"Thereza bila mapenzi yangu ya dhati juu yako nisingekueleza siri hii vilevile wewe unanihusu mimi sana kuliko mtu yoyote. Pia nina imani ukivuka salama nami nikavuka mtihani ulio mbele yangu tutafunga ndoa, “ alimimina mdomoni whisky iliyokuwa imebakia kwenye glasi na kuniita jina langu kwa sauti ya kilevi:
"Thereza."
"Abee."
''Najua undi hili unalielewa juujuu siku zote jasusi hana rafiki, siku zote anajali masilahi yake..anachojali kazi yake unapoimaliza lazima apoteze ushahidi."
"Kupoteza ushahidi una maana gani?"
"Swali zuri Thereza, siku zote jasusi huwa hajiingizi kwenye kazi zenye ushahidi, humtumia mtu. Ili kufanyiwa kazi hutangaza malipo mazuri yatayomshawishi
mtu aifanye kazi lakini mwisho wa kazi unapowajulisha kazi imekwisha hapo ndipo hukuua ili kupoteza shahidi."
"Eti kufanya nini?" nilishtuka.
"Kukuua ili kupoteza ushahidi ikiwa pamoja na kuchukua pesa zao zote walizokupa kupitia watumishi wa benki ambao ni mawakala wao ambao huwalipa asilimia fulani ya pesa zile."
Habari zile zilinishtua sana zilikuwa mpya kabisa maishani mwangu ambazo sikutarajia kuzisikia. Nakubaliana na usemi wa Dr Ray Jasusi hana rafiki pia jasusi hafanyi biashara ya hasara. Macho na masikio yalifunguka.
"Dr Ray una ushahidi na unayosema?" Nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho.
"Ndiyo, wengi wameuawa baada ya kufanya kazi na kudhulumiwa malipo yao. Japo
wamekupeleka mafunzoni nia yao ni kufanikisha kazi yao ukiimaliza ujue na we ndio mwisho wa maisha yako."
"Hivi wale watu mnaowachuna ngozi na kuwanyonya damu mnawazika wapi?" nilibadili mada kwa faida yangu.
"Kuna tanuru kwa ajili ya kuchoma miili yao na ikisha kuwa jivu tunaitupa baharini.
"Dr Ray unaweza kunisaidia vipi maana hata sijui nifanye nini hata najuta kuingia
mkataba, ningeyajua haya mapema nisingekubali, bora ningeendeleza msimamo wangu," niliingiwa wasiwasi na taarifa ile.
"Bora umekubali wangekuua."
"Na kuhusu pesa nitazilindaje?"
Itaendelea Jumanne

No comments