Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 19


 
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
"Kuna tanuru kwa ajili ya kuchoma miili yao na ikisha kuwa jivu tunaitupa baharini.
"Dr Ray unaweza kunisaidia vipi maana hata sijui nifanye nini hata najuta kuingia
mkataba, ningeyajua haya mapema nisingekubali, bora ningeendeleza msimamo wangu," niliingiwa wasiwasi na taarifa ile.
"Bora umekubali wangekuua."
"Na kuhusu pesa nitazilindaje?"
SASA ENDELEA...

"Ni rahisi zibadili kwenye akaunti ubadili na jina ukiwezakana weka mafungu hata kumi benki tofauti hapo utakuwa umewaweza tena kwa majina tofauti."
"Nini kingine cha muhimu hiki ni muhimu 'pass word' zitakusaidia sana hasa hii ya
Father Gin yule si Father bali Jasusi Gin anayepaka matope dini za watu yule ni shetani sijui kwa Mungu atajibu nini juu ya roho za watu alizozipoteza”
Dr Ray alinipa pass word zaidi ya tano za shirika lile la ujasusi ambalo halikuwa la dini kama linavyojulikana. Ndiyo maana hata Bwana Yesu kabla ya kuondoka alitutaadharisha na watu wataojinadi kwa jina lake hao tusiwaamini na ndio wanaochafua watu wa kweli walio wasafi mbele ya bwana.
Nilikumbuka kile kikao watu wanaonekana wasafi mbele ya dini zao kumbe wanyonya damu ukiwakuta mbele ya waumini wao wanavyo mtukuza Mungu kumbe mashetani.
Lakini kwa Mungu kila kitu kitalipwa kulingana na matendo yao, Mungu si mwongo wala si mtani wa mtu, ipo siku kweli itadhihiri hata ufanye gizani.
"Dr Ray ulijuana vipi na Father Gin?"
"Of course yule Father Gin alinichukua kutoka chuo cha ujasusi kazi yangu kubwa
ilikuwa kuwatibu watu wote walio chini yake, hasa kuzingatia kazi ya ujasusi ni ya
hatari yenye majeraha na makovu mengi.
"Ili kupoteza lengo tulijenga hospitali kubwa Kibaha na kuwahudumia watu wote lakini ni kituo cha ujasusi,” Dr Ray akionekana pombe zimemkolea aliongea kwa sauti ya huzuni.
"Thereza."
"Unasemaje?"
"Naomba uniahidi kama utakuwa tayari kufa kwa ajili yangu kwani na mimi nimejitoa kwa ajili yako."
"Dr Ray makuahidi."
"Basi kama nitakufa atayeniua si mwingine ila Father Gin na kuomba umuue kwa mkono wako."
"Nakuahidi nitafanya hivyo."
“Thereza naomba penzi lako kwa usiku huu japo sina uhakika kama nitauona usiku
wa kesho,” Dk Ray alizungumza kwa sauti iliyokata tamaa.
"Usihofu mpenzi leo mwili wangu utakuwa mali yako na tukivuka mtihani uliopo mbele yangu na yako ruksa kunivisha pete."
"Mpaka hapo hata kama nitakufa basi nitakufa moyo wangu ukiwa shwali nina imani
penzi lako lina thamani kwangu kuliko uhai wangu."
Nilimshika mkono na kupanda naye juu, baada ya kuongea tulioga pamoja na kujilaza
Kilichofuata nilimpa alichokitaka. Asubuhi baada ya supu zito na kuzimua na whisky Dk Ray aliniaga akiwa na furaha moyoni nina imani unajua nini kilichomfurahisha.
Baada ya kuondoka nami nilioga na kujiandaa kukabiliana na kilicho mbele yangu nilijiona nimo ndani ya kinywa cha mauti na uwezekano wa kutoka ni mdogo sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano kwani vifo vilikuwa nyuma na mbele sidhani kama vyote nitaweza kuvikwepa.
Penzi langu kwa Mr Ray si penzi la moyoni, kwangu kama shukurani ya kunifungua
macho. Yeye alikuwa na mapenzi ya kweli moyoni mwake na kuwa tayari kufa juu yangu.
Sikuwa na budi kuonyesha mapenzi ya dhati juu yake japo siyo moyoni bali ya kuunda kwa kipindi kile yeye alikuwa mtu muhimu sana ambaye alinisaidia kuyajua
mengi . Lakini mwanzo alinisaidia kwa ajili ya kuwafanyia kazi zao.
Japo Mungu kanijalia uzuri wa shani unaowazuzua wanaume wengi, nilishangaa
kwa kauli yake kuwa anipenda mtu aliyezichezea sehemu zangu za siri mara nyingi sikujua nini kilichomvutia kwangu.
Niliingia chumba changu nilicho kiteua kwa kazi zangu za kijasusi, chumba ambacho
nilikifunga mitambo ya mawasiliano. Nilizichukua zile picha tano za watu wanaotakiwa kuuawa.
Niliwaangalia kati ya hao watano walikuwa wazungu mmoja ndiye alikuwa mweusi kama mimi. Wote walionekana watu wa makamo kasoro msichana Marry White alikuwa umri kama wangu kama kunizidi ni miaka miwili. Baada ya kuzihifadhi picha zote kichwani nilianza kuangalia ramani na mitaa.
Walikuwa wanaoishi maelezo yaliyonionyesha nitateremka katika uwanja wa ndege wa London na kufikia hotel ya Browns Hotel London. Ofisi za wabaya zangu zilikuwa jirani mtaa wa Regent.
Na Italy nishukie uwanje wa ndege wa Rome na kupanga kwenye Hotel iliyo jirani na
uwanja huo wa ARZEMIDE. Na Ujerumani ilionyesha nishukie uwanja wa ndege wa
Pusseldorf ulio katika mji wa Dusseldorf. Na kupanga hotel ya karibu ya RADISSON SAS HOTEL DUSSELDORF. Iliyopo kwenye mtaa wa Kaiserwerther.
Baada ya kuihifadhi ile ramani kwenye kumbukumbu za ubongo wangu. Nilipata
kifungua kinywa nikiwa napata kifungua kinywa wazo moja lilinijia ni muhimu kujua
mazingira watoto wale waliotunzwa kwa ajili ya kuvunwa damuna ngozi hapo baadaye. Niliona haina haja ya kumshirikisha tena Father Gin juu ya safari yangu
kuwatembelea wale watoto.
Nilimuona Dk Ray anafaa sana ni muhimu anaweza kunisaidia zaidi, nilimpigia
simu.
"Vipi honey mzima?"
"Wa afya sijui wewe ua la moyo wangu."
"Mimi mzima ni hivi upo kazini?”
"Ndiyo"
"Nakuja sasa hivi nina shida na wewe."
"Nipo nimejaa tele kama pishi la mchele," kidogo nicheke Mzungu ana maneno kama
Mswahili.
Basi nakuja mpenzi."
"Ila usije moja kwa moja ofisini teremkia mbali na uje kwa kupitia mlango wa nyuma."
"Sawa," nilikata simu.
Sikuwa na muda wa kupoteza nilikodi gari, sikuwa na haja ya kwenda na gari
langu nilijiona kama nimeishaianza kazi, nilianza kwenda mwendo wa machale, kama nilivyo elekezwa na Dk Ray.
Niliwasiri Kibaha baada ya nusu saa niliteremkia mbali na kutembea kwa miguu hadi pale hospitali tena nilipitia kwa nyuma. Nilipofika ofisini nilikutana na pigo la mwaka mwili wa Dk Ray ulikuwa umelazwa juu ya meza ukiwa umetenganishwa na kichwa matumbo yakiwa nje.
Kengele ya hatari ililia kichwani kuonesha shughuli imeshaanza, nikiwa bado nimepigwa na bumbuwazi mara nilisikia sauti za watu wakiongea nje ya chumba.
"Hivi huyu malaya wake atakuja saa ngapi? Unajua sister tumemuahidi kazi itakuwa ya saa moja." mmoja alimuuliza mwenzake.
"Atakuwa amepitia wapi au tumfuate kwake?" Mwingine alichangia.
"Tunaweza kuchengana naye tumsubiri namba yake ya simu si unayo tumpigie tukijifanya Doctor Ray we nakuamini kwa kuigiza sauti za watu."
Kusikia vile moyo ulinipasuka nilijua nitajulikana, niliitoa simu haraka
na kuizima nilijua kwa mtindo huo wamenikosa. Nilimsikia mmoja akisema:
"Unajua Marc sio siri inavyoonekana huyu msichana ni mtu hatari sana, kwani hata
sister Marry White alionyesha jinsi anavyomuhofia.”
"Inawezekana machale yamemcheza hata simu yake haipatikani."
"Ingia ndani ukaangalie namba kwenye simu ya Doctor Ray kama zinalingana."
"Nilijua shughuli rasmi imeanza nilijibanza nyuma ya mlango, sauti za nyayo za viatu nilizisikia zikisogelea mlango wa ofisi, mara mlango ulifunguliwa aliingia kijana aliyeonyesha mwili wa mazoezi alikwenda kwenye meza ili achukue simu iliyokuwepo juu ya meza pembeni na mwili wa Dr Ray.
Niliurudisha mlango kwa mguu, nilimsogelea kidogo nikijua sehemu ile teke la
kuzunguka litampata vizuri. Nilikohoa ili ageuke na kuweka vizuri kisogo chake.
Alipogeuka kabla hajashangaa niligeuka na teke mzunguko lililompata kwenye kisogo. Hakuwahi kupiga hata kelele alikuwa mgeni wa kuzimu. Nilimlaza pembeni na kumsubiri wa pili niliyemsikia akimwita mwenzake:
"Marc vipi mwaka mzima?"
"Tunapoteza muda kama vipi tumfuate kwake."
Alipoona kimya aliingia mwenyewe alionyesha hakujiandaa, aliingia kizembe
ilionyesha alijiamini sana. Alipoingia alishangaa kutomuona mwenzake
alimwita.
"Marc," ilimwita kwa sauti ya juu kidogo.
"Unasemaje?" niliitikia, alipogeuka nusra azirai kwa mshtuko alikuwa kama ananifananisha.
"Wewe ni Thereza?"
"Ndiyo mimi."
"Marc yupo wapi?"
"Wanaongea lugha moja na Doctor Ray."
"Yaa..ani umemuua?" Aliniuliza macho yamemtoka pima.
"Sijui muulize mwenyewe,"nilimjibu kwa dharau.
"Sikubalii," alichomoa kisu.
"Aaah... Aibu mwanaume mzima uliyekamilika unanibebea kisu mtoto wa kike."
Kauli yangu ilimfanya aone aibu na kukitupa kisu pembeni alivua fulana
iliyo kuwa imembana na kuuonyesha mwili wake uliojengeka kimazoezi.
Nilijua lazima atapigana kwa pupa alinifuata kama mbogo na kutupa ngumi nzito iliyotoa mlio wa kukata upepo iliponikosa. Niliinama na kumpiga kiwiko cha kuzunguka kwenye mbavu changa alizozinyoosha wakati wa kupiga ngumi. Nilimsikia akiguna kwa maumivu.
Alipopiga ngumi nyingine niliiongezea na teke kwenye maungio aliongeza kilio
Kingine. Mkono ulipoteremka ulikuwa umelegea nilijua nimeshauvunja.
Nilimalizia na teke la kuzunguka la chini lililomrusha juu na kuanguka chini kama mzigo. Nilimfuata na kumuongeza ngumi mfurulizo zilizomlegeza. Nilimfuata na kumuuliza:
"Marry White yupo wapi?" nilimuuliza kwa sauti ya ukali kidogo, lakini hakujibu alionesha kiburi.
"Aaah unajifanya nunda siyo?"
Wakati huo hasira zilikuwa zimenipanda nilitamani kunywa damu ya mtu, mauaji ya Dk Ray yaliniongezea hasira.
"Utanijibu hunijibu?"
Aliendelea kuwa kimya, niligeuka kufuata kisu, akili yangu ilicheza na yeye siku zote
jasusi yoyote hakubali kufa kikondoo. Nilipogeuza uso nilikuta ndio anapeleka mkono wa kulia mdomoni kwa vile wa kushoto nilikwisha uvunja, Niliruka kama mkizi na kufanikiwa kuupiga pembeni alichotaka kukimeza ili ajiue. Nilimshikia kile kisu na kumuuliza.
"Nakuuliza kwa mara ya mwisho Marry White yupo wapi?"
"We niue tu mi sijui," alionesha kiburi cha hali ya juu.
"Aah unafanya utani siyo?"
Niliingiza kisu katika jereha lake la jichoni, maumivu yalipozidi alipiga kelele:
"Utaniua bure, we niue kabisa kuliko kunitesa hivi mi’ sijui lolote."
"Nitalitoa jicho kama utaleta kitu kujua," wakati huo nilikuwa nakandamiza kisu kwenye jeraha. Yule mtu alipiga kelele za maumivu makali.
"Ooh!Niache nitakueleza."
Nilikichomoa kile kisu kilichokuwa kimeingia robo tatu, wakati huo damu zilikuwa zikizidi kutoka kwenye jeraha.
"Haya ongea."
"Nimeamini kweli wewe mtu hatari sifa na hofu alizoonyesha sister Marry White nilifikiria ni uongo kweli dada unatisha,"alisema yule jamaa huku anauma meno kwa maumivu makali.
"Sikuja kusifiwa hapa nieleze Marry White yupo wapi?”
"Yupo Nairobi."
"Nairobi anafanya nini?"
"Sijui ila alisema mpaka jioni atakuwa Arusha."
“Yupo sehemu gani pale Nairobi?"
"Huwezi kumuwahi ila jioni ya leo wana kikao kingine Arusha."
"Vikao vyao vinahusu nini?"
"Ukweli mimi sijui, sisi kazi yetu kubwa ni kutumwa kufanya mauaji."
"Ooh, vizuri, mmeshaua watu wangapi?"
"Sisi kama tungekuua wewe ungekuwa wa sita."
"Ina maana wapo wengine?"
"Tupo wengi."
"Kwa nini mlitumwa kuniua mimi?"
"Ujuzi tunatofautiana hivyo sisi ndio tulioonekana tupo juu kutumia silaha hata mapigano ya mikono."
"Mbona unaonekana cha mtoto hata hujui kupigana?" Nilimdhihaki.
"Wewe unatisha ningejua uwezo wako uko hivi wala nisingedhubutu kuja kunadi uhai wangu kwa bei ya bure."
"Nieleze hapa mjini mpo wangapi?"
"Tupo sita."
"Wengine wapo wapi?"
"Wanafuatilia biashara za bosi."
"Biashara gani hiyo?"
"Ya kukusanya vijana" kusikia vile nilishtuka.
"Hao vijana mnawakusanya ili iweje?"
"Kwa kweli hapo mimi sijui."
"Acha kuniudhi nieleze ukweli."
"Ukweli sijui ila baada ya kuwakusanya huwapeleka nje kidogo ya mji wa Arusha sehemu hiyo nilishafika mara moja kupeleka watoto. Lakini zaidi ya hapo sielewe mara nyingi tulishawakusanya huwapeleka na tukiwafikisha sisi tunarudi."
"Umesema biashara una maana gani?"
"Mara nyingi hutumia pesa kupewa vijana waliopo kwenye vituo vya kulelea vijana."
"Hii biashara mmeianza lini?"
"Ni mwezi wa sita sasa."
"Mungu wangu!"
"Dada mbona umeshtuka kwani hii biashara ina nini?" Yule mkora aliniuliza.
"Aaah, wacha tu," nilificha ninachokijua.
"Umenieleza wenzio wapo hoteli gani?"
“Wote tupo New African Hoteli."
"Pale mmetumia majina gani?"
"Pale nilipanga chumba kimoja na Marc"
"Wewe unaitwa nani?"
"Zone."
"Ehe na wengine?"
"Yupo Cathy ambaye yupo chumba kimoja na Puchu na Kallo yupo na John."
"Ok, vizuri, umenieleza Arusha sehemu gani?"
"Nje ya Arusha mimi si mwenyeji sana."
"We raia wa wapi?"
"Kenya"
"Umesema mkishakusanya vijana mnarudi lini Arusha?"
"Leo usiku."
"Asante kwa msaada wako."
"Naomba na mimi unikimbize hospitali."
Sikumjibu nilikuwa kama nataka kuondoka niligeuka na teke kali iliyomvunja shingo na kumuwahisha kuzimu. Nilipitia mlango wa nyuma na kutokomea zangu, nilimkuta dereva wangu usingizi umempitia.
"Kaka vipi? Niwahishe Dar."
"Ooh, dada umeisharudi, umesema?" Dereva alikurupuka katika usingizi wa mang'amung'amu.
Dereva aling'oa gari kwa mwendo wa kasi kurudi Dar, njiani nlikuwa na mawazo mengi juu ya vita iliyo mbele yangu nilijua kazi imeisha anza. Kwa maana moja au nyingine niliona kazi yangu huenda ikawa nyepesi hatua za awali baada ya kujua kumbe kundi la Marry White lipo hapahapa Tanzania na shughuli zake anazifanya Arusha.

Itaendelea

No comments