Header Ads

Hassan Kessy akacha mazoezi Yanga SC


BEKI mpya wa Yanga, Hassan Kessy, jana alikacha mazoezi ya timu hiyo na kwenda kushughulikia barua ya kumuidhinisha kuichezea timu hiyo kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hali hiyo imetokea ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa Simba ugomee kutoa barua ya kumuidhinisha beki huyo kuichezea Yanga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwa madai kuwa hakusajiliwa kihalali.

Beki huyo, tayari amekwenda kutoa malalamiko yake kwenye Chama cha Wachezaji wa Tanzania (Sputanza), akiishtaki Simba kushindwa kutoa barua ya kumuidhinisha kuichezea Yanga.

Akizungumza na Championi Jumatano kwa unyonge, Kessy alisema yeye anafanya mazoezi kwa ajili ya kucheza mechi, hivyo ameona ni jambo jema kwake kulifuatilia suala hilo mwenyewe kwa makini ili kujua hatma yake.

Kessy alisema, anaumia anaposhindwa kucheza mechi za kimataifa ambazo Yanga inashiriki kwa sababu Simba wameshindwa kutoa barua ya kumuidhinisha ukiwa mkataba wake umemalizika tangu Juni 15, mwaka huu.

Aliongeza kuwa, jana asubuhi alikwenda Mwananyamala Studio Dar, ilipo ofisi ya Sputanza kisha kwenda TFF ili kujua hatma yake ya kuichezea timu yake mpya.

“Leo nimeshindwa kufanya mazoezi ya asubuhi pamoja na wenzangu kwa kuwa nilikwenda kushughulikia barua ya kuniidhinisha kuichezea Yanga kutoka kwa Simba niliyomaliza nayo mkataba.

“Hiyo, ni baada ya kuona sintofahamu ya suala hilo, hivyo niliuomba uongozi na kuniruhusu kwenda Sputanza na baadaye TFF ili kujua hatma yangu.

“Ujue ninakosa amani kabisa na timu yangu mpya ya Yanga, na mimi siku zote napenda kucheza sasa linapokuja suala kama hili ninajisikia vibaya mimi kuonekana mchezaji wa mazoezi pekee,” alilalamika Kessy.
Hata hivyo uongozi wa Yanga kupitia kwa meneja wake, Hafidh Saleh alisema jana: Tumemruhusu kwenda kushughulikia mambo yake barua toka TFF.”


No comments