Header Ads

Helen Kijo Bisimba: CUF, CCM zitafute msuluhishi!


Katika sehemu ya kwanza ya mahojiano haya wiki iliyopita tulisoma jinsi Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Helen Kijo-Bisimba pamoja na mambo mengine, alivyoshauri na kupendekeza kufutwa kwa adhabu ya kifo nchini. Katika sehemu hii ya pili amezungumzia mgogoro wa kisiasa unaofukuta Zanzibar na mambo mengine. Ungana nasi:
Zanzibar kuna mgogoro mkubwa wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha wananchi (CUF) baada ya kufutwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na kurudiwa mwaka huu, unashauri nini kuhusu tatizo hilo ili amani izidi kutawa katika visiwa hivyo?
Jibu: Hili suala ni nyeti sana na muhimu na ninawashangaa wanaobeza. Niiambie serikali kuwa huwezi kuficha kichwa mchangani kama mbuni huku kiwiliwili chake kikiwa nje. Vyama vikubwa vya siasa CCM na CUF nawashauri viongozi wake wajishushe na wapatane ili suluhu ipatikane na wapate msuluhishi. Wenyewe hawawezi kusuluhishana na kupeana haki. Hatutaki yatokee kama yaliyotokea miaka ya nyuma ambapo nchi ilizalisha wakimbizi, ilikuwa ni aibu kwa taifa.
Mwaka jana tumeshuhudia wananchi wakivamia vituo vya polisi kwa nia ya kuwaadhibu watuhumiwa au kuwatoa raia walioswekwa ndani, nini maoni yako kuhusu hilo?
Jibu: Hapa kuna tatizo la wananchi kujichukulia sheria mikononi na ni hatari sana kama taifa. Raia wanapaswa kuheshimu polisi. Lakini kwa nini tumefika hapa? Uchunguzi sahihi ni lazima ufanyike kwani ni hatari kwa usalama. Vituo vinavamiwa na polisi kama wametishika, matokeo yake sasa baadhi ya vituo vinafungwa usiku au kuwekewa uzio. Ipo haja ya polisi kutafuta mbinu kukabiliana na hali hiyo ya vituo vyao kuvamiwa. Waondoe hofu ya wananchi iliyopo sasa kwamba ukiona kituo kinafungwa kutokana na woga wa kuvamiwa na majambazi vipi sisi raia majumbani mwetu? Jeshi la polisi halipaswi kuogopa. Lakini pia wanapaswa kutenda haki na kushirikiana na raia wema bila kuwatendea haki wananchi watashindwa kazi na hilo ni tatizo, wanapaswa kutambua hilo.
Kuna tafiti mbalimbali nchini zinazoonesha kuwa polisi na mahakama kumekithiri kwa rushwa, hilo unazungumziaje?
Jibu:Sisi tulitafiti na kwa bahati mbaya hata tafiti nyingi zinaona polisi wanaomba rushwa au kushawishi rushwa kutolewa. Haki ikikosekana wananchi wanajichukulia sheria mkononi kwa sababu mifumo ya haki inashindwa kumsaidia kupata haki yake.
Tuliwahi kusikia kituo hiki kikimshitaki aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kuwaambia polisi ‘raia wapigwe tu’, kesi ile ilikwishaje?
Kwanza wananchi walidhani (aliyekuwa) Waziri Mkuu Pinda yupo juu ya sheria lakini baada ya ile kesi wakajua kuwa anaweza kushitakiwa. Kesi ile ilikwenda vizuri lakini ilihukumiwa kisiasa kwamba alikosea lakini sisi kama taasisi mahakama ikasema hatuwezi kupigwa tukaumia. Lakini polisi haohao waliwahi kukamata vifaa vyetu vya kazi tukaumia kikazi wakati wa uchaguzi mkuu. Hatujakata tamaa kwani tuna mpango wa kukata rufaa.
Ipo migogoro mingi ya ardhi nchini na bado kuna baadhi ya makabila yanawadhulumu wanawake haki ya kumiliki ardhi hasa baada ya waume wao kufariki dunia, kituo kinawasaidiaje wanawake kama hao ambao pengine wengine hawajui haki zao?
Jibu: Ni kweli tunapokea watu mbalimbali ambao wana shida za kisheria kwenye ndoa au mirathi. Ukiniuliza tunaawasaidiaje jibu ni kwamba wapo ambao tunawasimamia kesi zao mahakamani japokuwa tuna mawakili wachache sana na gharama za huduma hiyo ni kubwa, wapo wananchi ambao tunawapa elimu ya kutambua haki zao na hasa vijijini, sheria za kimila zinawanyima haki wanawake wengi nchini. Sasa huko wilayani tunafundisha sheria kwa umma ili watu watambue haki zao, hilo tumefanikiwa kwa kiasi fulani kwani hivi sasa wanajua haki ni nini.
Lipo tatizo zito linaloharibu sifa ya taifa letu la mauaji ya albino, kama kituo cha haki za binadamu unafikiri nini kifanyike kuondoa aibu hii sugu?
Jibu: Ukatili umeongezeka sana, sijui ni roho gani imepandikizwa kwa Watanzania.Tatizo hili baya lipo na serikali inakosea. Wanafuatilia wakataji wa viungo na kuwaacha wanaowatuma, wafuatwe hao watumaji ambao wengi ni waganga wa kienyeji ambao wanatoa ahadi ya fedha. Nadhani inawezekana kwa sababu polisi ina intelijensia kali. Suluhisho lingine ni elimu kwa umma itolewe kwa watu wote ili wajue kuwa albino ni binadamu kama wengine. Roho ya kuthamini utu ifufuliwe kuanzia shuleni, asasi za dini zishirikishwe ili mtu asitamani viungo vya watu na aone ni dhambi, hakika ucha Mungu umepungua sana. Albino tuliwahi kuwatetea mahakamani lakini walijitoa, wakatuvunja nguvu sana.
Mna mpango gani kuhakikisha kituo hiki kinajulikana na wananchi wengi nchini ili kiweze kuwasaidia wenye uhitaji?
Jibu: Kazi za kituo hiki siyo za kibiashara hivyo hatujitangazi, tunatoa msaada tu wa kisheria na ndiyo maana hatuna mabango mitaani. Kwa mfano Kinondoni pekee tuna watu zaidi ya 80 waliosaidiwa na kituo hiki kisheria. Tuna mchango mkubwa kitaifa kuwafanya watu kujua haki za binadamu ni nini. Na ndiyo maana kituo hiki kinakaribisha wanachama wa jinsia zote ilimradi tu awe anaheshimu haki za binadamu.
Tunakushukuru mkurugenzi.
Kijo-Bisimba: Asante na karibuni tena.

CHANZO: UWAZI -GPL

No comments