Header Ads

Kanga Moja Kiunoni...Mbengembenge-11

 

ILIPOISHIA : “Kuwa kwangu tayari si inategemea unataka kutoa dukuduku gani anko, mimi niko tayari nakusikiliza...” SASA JIACHIE MWENYEWE... JOMBI alimwangalia mwanamke huyo kwa macho yaliyojaa aibu licha ya kwamba ni mwanaume kisha akasema... “Najua huenda nitakukera lakini unatakiwa kunivumulia...” “Mimi nimeshakuvumilia anko, ndiyo maana niko hapa tena nimekuletea na chakula, huoni kuwa nimekuvumilia?” “Kweli...kweli umenivumilia... kifupi anti mimi kama mimi, yaani kutoka moyoni mwangu humu, tena ndani kabisa ya moyo kusema ule ukweli labda niwe wazi tu ili nitoe dukuduku langu ni kwamba, kutoka moyoni mimi mwenzio nimeamua kufunguka,” alibabaika Jombi mpaka
mama Mei akashangaa... “Sasa hapo mimi nikueleweje anko? Ndiyo umesema nini sasa?” mama Mei aliuliza akiwa ameegemeza mikono kwenye meza na kumwangalia Jombi kwa macho ya mvuto... “Ina maana hujanielewa anti?” “Sijakuelewa anko, umemaliza kwa kusema umeamua kufunguka, sasa unafunguka kuhusu nini?” “Aha! Yaani mimi kama mimi... kwanza mimi naitwa Jombi, nina mke na mtoto mmoja, nafanya kazi serikalini, tunakwenda kazini kila siku kasoro Jumamosi na Jumapili tu au siku za sikukuu au siku niumwe na nikiumwa lazima niende na sick sheet.” Mama Mei alijikuta akishikwa na kicheko cha moyoni lakini akajikaza asikioneshe waziwazi kwa Jombi... “Maskini, pole sana kwa kuumwa anko, kumbe huwa unaumwa mpaka unachukua sick sheet...?” “Eee! Lakini hilo silo nililotaka kulisema...” “Ulitaka kusema lipi anko?” “Mimi nakukubali saa anti, yaani Mungu amekuumba vizuri, amekupendelea kila idara yaani...da! nampongeza sana mista, amepata mke mzuri,” alisema Jombi huku macho yake yakiangalia ukutani ambako kulikuwa na bango la tangazo la kampuni moja ya bia... “Asante sana anko kwa kunipamba, lakini mimi najiona kawaida sana...” “Wewe unajiona kawaida lakini watu
wengine tunakuona si kawaida.” Mama Mei alicheka, Jombi yeye aliachia tabasamu tu kisha kukapita ukimya kwa muda wa kama sekunde kadhaa... “Sasa hujanipa jibu anti,” alisema Jombi, mama Mei akashtuka... “Anko jibu gani tena?” “Kwani nimesema nini?” “Umenipongeza tu, nikasema asante jamani kwa kunipamba.” Mpaka mama Mei anaaga ili kuondoka kwenye baa hiyo, Jombi alikuwa hajui hatima yake lakini alikiri moyoni mwake kwamba, maneno yake aliyomwambia mama Mei hayakuwa yanatosha kumfanya ajisikie ametongozwa, akaamua kulipuka... “Anti mimi kusema ukweli nakupenda tu...” “Asante anko kwa kunipenda,” alijibu mama Mei kwa kulegeza sauti... “Natamani sana uwe wangu,” Jombi aliongeza... “Kivipi anko?” “Uwe wangu katika mapenzi...” “Ha! Anko, itakuwa ngumu sana, yaani una mke, una mtoto na mimi nina mume nina mtoto halafu tunakuwa wapenzi, mbona ngumu sana.” Jombi alijisikia vibaya sana kwa jibu hilo, akaamua kuongeza gia... “Kwa hiyo unataka kusema unataka kuwa na mpenzi asiye kuwa na mke au?” “Sitaki kuwa na mpenzi kabisa, kwani
tayari ninaye.” Jombi alihema kwa nguvu huku mama Mei akishika kapu lenye hotpoti tayari kwa kusimama... “Kesho basi anko...” “Da! Umeniacha njia panda anti...” “Kivipi?” “Sasa nijue nini?” “Si nimeshakwambia jamani anko.” “Oke...oke!” Mama Mei aliondoka huku Jombi akimsindikiza kwa macho mpaka anaishia. Wateja walimwangalia na kucheka, wapo waliojua si mkewe alikuwa anaimbisha tu na amepigwa chini kavukavu. *** Hakukuwa na mawasiliano kati ya Jombi na mama Mei kwa muda wa siku tatu tangu walipokutana siku ile, baa. Siku hiyo sasa, saa nne usiku, Jombi akiwa kwenye baa nyingine, alipokea simu ya mama Mei... “Anko uko wapi?” “Niko huku bondeni, kuna baa inaitwa Mundu...” “Nakuomba njoo nyumbani...”
Je, Jombi atakwenda? Na je, atakutana na nini huko? Usikose kusoma Gazeti la Ijumaa Wikienda, Jumatatu ijayo. Pia soma chombezo langu lingine kwenye Gazeti la Uwazi, Jumanne ijayo

No comments