Header Ads

KIONGOZI WA KLABU ANAYESHANGILIA YANGA KUFUNGWA, KLABU YAKE IKIWA INABORONGA, KWELI ANAJITAMBUA HUYU?Na Saleh Ally
RAHA ya soka ni ushabiki, hakuna anayeweza kushangaa ndiyo maana mashabiki wa Simba wanaonekana kuwa na furaha sana kuona Yanga inafeli au kushindwa kusonga katika hatua ya Kombe la Shirikisho.

Yanga ndiyo wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho lakini kwa mambo yalivyo, hakika nafasi ya Yanga ni finyu na kama itabadilika, basi itakuwa ni ile miujiza ya kisoka.

Mashabiki wa Simba na timu nyingine, inawezekana Azam FC na nyinginezo wanaweza kuwa na furaha sana kwa kuona Yanga inafeli. Maana sasa katika Kundi A inaendelea kushika mkia baada ya sare moja katika mechi tatu.

Sare hiyo inaifanya Yanga kuwa mkiani ikiwa na pointi moja tu, Medeama ya Ghana wanafuatia wakiwa na pointi mbili baada ya sare mbili na Mo Bejaia na TP Mazembe hata kabla ya mechi ya jana na baada ya mechi hiyo, watabaki kwenye nafasi ya kwanza na ya pili.

Mashabiki hasa wa Simba, waliishangilia sana Medeama, hata mashabiki wa Yanga wangeweza kufanya hivyo kwa Simba kama ingekuwa hatua hii, au waliwahi kufanya hivyo, mfano wakati Simba ikichapwa na TP Mazembe miaka michache iliyopita.

Mimi ni mtumishi wa wapenda michezo, sioni vibaya kuwashawishi wasomaji wa gazeti hili kwamba bado suala la uzalendo linapaswa kupewa kipaumbele kama utalinganisha na kila kitu. Yanga ni ya Tanzania na si kutoka Ghana, DR Congo au Morocco.

Mashabiki kwangu pia wanaweza kuwa si tatizo sana lakini ningependa kutupa jicho mbali sana hasa kwa viongozi wa klabu nyingine ambao wanaonekana hawajitambui na wanajiona wao ni sehemu ya mashabiki wa soka.

Si sahihi kiongozi wa klabu kubwa kuonyesha ushabiki kama ule unaoweza kuonyeshwa na shabiki wa kawaida wa soka aliye jukwaani. Nasema hivi kwa kuwa mmoja wa viongozi wa klabu maarufu nchini, alionekana kuchanganyikiwa baada ya Medeama kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga.

Kiongozi huyo alikuwa na furaha, jasho linamtoka na hata akafikia kuwapongeza wachezaji wa Medeama baada ya mechi dhidi ya Yanga, juzi Jumamosi. Kwamba amefurahishwa na sare hiyo.

Angeweza kufurahi kama shabiki, lakini kama kiongozi pia anapaswa kujiuliza klabu ambayo anaiongoza imefikia wapi? Iko wapi na mafanikio yake yakoje kwa kipindi husika.

Inawezekana presha yake kubwa ilianza baada ya Yanga kubwa bingwa Tanzania Bara, ikaendelea ilipokuwa bingwa Kombe la FA. Huenda imemkera zaidi ilipofikia kucheza Kombe la Shirikisho. Kwake ilikuwa si vema Yanga ikafanikiwa.

Ushabiki wake unaweza usiwe hoja ya msingi au tija, hoja kuu linaweza kuwa swali la kipi alichokifanya kuisaidia timu au klabu yake kupata maendeleo makubwa?

Huyu anayefurahia timu nyingine kufeli, huku yake ikiwa haina hata mfano wa mafanikio, anapaswa kuwa kiongozi? Binafsi ninaingiwa na hofu kwa kuwa kiongozi bora alipaswa kuwa na malengo, anayepaswa kujifunza na anayetaka kutimiza ndoto.

Kiongozi anayefurahia Yanga iishie njiani, yeye timu yake ameiandaa? Alipaswa kufurahia au kujifunza zaidi? Kweli alipaswa kuonyesha amechanganyikiwa kwa furaha kuona Yanga imetoka sare?

Kama anapata muda huo, wakati gani anapata muda wa kufanya maandalizi ya kutosha na kuisaidia klabu yake? Jiulize kiongozi kama huyo ambaye yeye ameishafeli kwa misimu kadhaa. Kweli anapaswa kuwa na furaha kuona wengine wanafeli pia?


Maana yake amekubali kufeli kwake na angefurahi wengine wafeli zaidi kwa kuwa yake ipo taabani na haifanyi vizuri. Sasa maendeleo ya soka yanatokea wapi? Ushauri wangu ni hivi, ushabiki hauepukiki lakini vizuri kuwa na staha katika hili kuepuka kuonyesha upungufu wako hadharani bila ya kujua unajimaliza.

No comments