Header Ads

MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 17


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
Ndani ya ndege kulikuwa na watu zaidi ya hamsini kila mmoja alikuwa kimya.
Tulisafiri kwa muda wa siku mbili. Siku ya pili ndege ilitua ilikuwa ni usiku wa manane, tuliteremka sikujua ule ni mji gani hata nilipo wauliza wenzangu nao walisema hawajui lakini ni moja ya nchi za Ulaya.
SASA ENDELEA...
Hata nilipo muuliza mkuu wa msafara alinijibu eti nilichofuata ni mafunzo sio kujua ule ni mji gani au nchi gani.
Kesho yake asubuhi tuliamshwa na kukumbiza mchakamchaka, maisha yale hayakuwa mageni kwangu kwani hayana tofauti na yale niliyoishi na mzee Utakufalini ni ukomandoo tosha.
Tofauti yake mafunzo yalikuwa ya kisasa yenye kukufanya mwanadamu uwe na moyo wa chuma roho ya kinyama ya kumuua mwanadamu mwenzio kama unaua nzi. Nilijifunza vitu vingi kutumia silaha za kila aina, vifaa vyote vya electr onic kutumia vyombo vyote vya kisasa.
Niliweza kuongea lugha zaidi ya tano kiswahili kiingereza, kifaransa, kiarabu na kitaliano. Vilevile nilikuwa na uwezo wa kuigiza sauti tofauti zaidi ya ishirini.
Nilifuzu mbinu za mapigano ya silaha na mikono baada ya kuhitimu mafunzo nilirudi Tanzania kwa mtindo uleule nilioondokea wa kufungwa kitambaa usoni.
Baada ya kufika nyumbani Tanzania nilipewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kujulishwa ni kazi gani iliyo mbele yangu iliyoonekana nzito. Lakini kulikuwa na tofauti kati ya mwanzo na muda ule.
Mwanzo nilipokuwa nikiifikiria hiyo kazi nisiyoijua moyo uliingia hofu na woga mwingi ulinitawala. Lakini baada ya kurudi kutoka kwenye mafunzo ya hatari sikuwa tena na woga hata chembe, nilikuwa tayari kwa kazi yoyote iliyo mbele yangu.
Baada ya mapumziko niliitwa Kibaha tayari kukabidhiwa hiyo kazi, kama kawaida nilikutana na Dk Ray:
"Ooh karibu mrembo."
“Asante.”
“Nina imani upo tayari kwa kazi?”
“Ndio maana yake”
“Sawa, subiri wakubwa watafika muda si mrefu ili kukueleza cha kufanya
“Hakuna tabu.”
Nilikaribishwa sebuleni na kupewa kinywaji nikiwa nawasubiri hao wakubwa.
Niliendelea kupata kinywaji laini na kusoma magazeti ya siku ile.
Mara kundi la watu wasiopungua kumi na mbili walinipita kuelekea chumba cha mikutano hakuna aliyenisalimia zaidi ya kupita kimyakimya. Nami sikuwasalimia nilitulia tuli nikisoma magazeti, mara alikuja Dk Ray na kunieleza:
“Thereza jiandae wazee wameisha kuja.”
“Nijiandae kwa kipi?” nilimuuliza.
“Ili kukabiliana na maswali yao.”
“Wana swali gani jipya ambalo halijawahi kuulizwa duniani?”
“Unaonekana unajiamini sana?” Dk Ray.
“Lazima nijiamini, ndio maana nipo hapa tayari kwa lolote.”
“Nilikuwa nakutaarifu tu.”
“Shaka ondoa nipo tayari kukabiliana na mtu yeyote kama niliweza kukabiliana na kifo, mwanadamu ni nini kwangu?”
“Mmh, sikuwezi.”
Dk Ray aliondoka na kuniacha nikisoma gazeti lakini mawazo yakiwa juu ya kikao hicho. Nilijikuta najiuliza swali la awali inaweza kuwa ni kazi gani. Hao wakubwa sio siri ni wakubwa kweli wengine wapo serikalini tena wana vyeo vya juu. wengie wapo taasisi za dini walio mbele katika kutoa misaada kwa jamii lakini wengine walikuwa wageni machoni mwangu.
Kikao kilifanyika kwa zaidi ya saa mbili na mimi niliendelea kusubiri mpaka nilipo fuatwa na Dk Ray.
“Vipi upo tayari?”
“Tayari kivipi?” nilimuuliza.
“Kuonana na wazee.”
“Nilikuwa tayari tangu nilipotoka nyumbani kwangu.”
“Basi tuongozane kwenye kikao ambacho nakiona ni kizito tofauti na vikao vyote.”
Niliongozana na Dk Ray hadi kwenye ukumbi wa mikutano uliokuwa mzuri uliojengwa kisasa.
Nilipoingia nilionyeshwa kiti kwa ishara ya mkono, kilikuwa kiti cha kati yaani kinachotazamana na mwenyekiti wa kikao. Baada ya kuketi Ray alitoka nje ya chumba cha mikutano ikimaanisha kicheo ni mtu mdogo sana.
Baada ya kuketi alikuja msichana aliyevaa mavazi yaliyouacha uchi mwili wake kwa asilimia themanini. Kile kilinishtua yaani mhudumu ni tofauti kubwa na picha iliyokuwa ndani kwenye kikao cha watu wasio pungua kumi na mbili wenye heshima zao.
Walikuwepo viongozi wa dini mbili viongozi wa serikali na viongozi wa mashirika ya dini ya nje na taasisi zisizo za kiserikali (NGO!S) za kitaifa na kimataifa. Nilijiuliza iweje msichana alijiweka sehemu kubwa ya mwili wake uchi ndiye awe mhudumu wao?
Hapo kengele ya tahadhari ililia kichwani mwangu, niliachana na hilo kwa vile sicho nilichokifuata. Muhimu kwa muda ule kujua ni kazi gani ninayotaka kupewa.
Mhudumu aliyekuwa amesimama pembeni yangu aliniuliza:
“Dada unatumia kinywaji gani?”
Wakati huo kila mmoja aliyekuwa mule ndani alikuwa akitumia pombe kali.
“Nipatie soda ya aina yeyote.”
“Ooh! Samahami dada yangu hakuna soda ya aina yeyote zaidi ya pombe kali na pombe zingine.”
“Maji yapo?”
“Ndio yapo.”
“Niletee.”
Mhudumu aliondoka baada ya muda alirudi na chupa kubwa ya maji pamoja na glasi. Baada ya kunijazia maji kwenye glasi aliondoka, wakati wote huo kikao kilikuwa kimya wakipitia nyaraka muhimu kila mmoja alikuwa ameinama akisoma. Wakiwa wanaendelea kupeuzi na mimi muda ule niliutumia kuwasoma sura zao.
Kati ya watu kumi na mbili sura sita nilizifahamu hazikuwa ngeni machoni mwangu ila sita kila nilivyojitahidi kuzikumbuka jibu lilikuwa mbali. Nilitulia tuli huku nikiendelea kuisoma mandhari ya mule ndani.
Nilishtuliwa na mlio wa meza iliyogongwa ikimaanisha tuwe tayari kumsikiliza mwenyekiti wa kikao ambaye hakuwa mwingine ila Father Gin mkuu wa kanisa la Watu waliojitolea kwa ajili ya Bwana.
Alikuwa ni mtu ninayemuheshimu sana ambaye ndiye kinara wa kutoa misaada si kwa wananchi tu hata serikali nayo iliuthamini mchango wake kwa maendeleo ya nchi.
“Karibu Thereza ilikuwa sauti yake nzito Father Gin.”
“Asante.”
“Kabla ya yote sister Caroline mwapishane ili awe tayari kwa kikao chetu.”
Mmoja wa wajumbe wa mkutano alinyanyuka na kuja karibu yangu. Niliapishwa kiapo tofauti na viapo nilivyokwisha wahi kuona mtu akiapa. Kilikuwa kiapo cha kulinda na kuhifadhi siri ya kundi na kuwa tayari kufa kuliko kutoa siri ya kikundi. Vilevile kuwa tayari kuuawa pale nitapobainika nimetoa siri.
Baada ya kiapo ndipo nilipotambulishwa kwa wajumbe wa kikao kile, wageni kulikuwa na raia wa Pakistan, Columbia, Afrika magharibi , Uturuki, Marekani ya kusini.
Baada ya kutambushwa kwao Father Gin alinigeukia mimi:
“Ndugu wajumbe wa mkutano wa PT au Pigo Takatifu huyu ndiye tuliyemwandaa kwa ajili ya Operesheni Pigo Takatifu. Leo hii kama tulivyoongea kwenye kikao chetu jukumu lote tunamkabidhi binti ambaye nina imani ataifanya kazi vizuri na kuweza kufanikisha opereshemi yetu, Thereza,” aliiniita:
“Abee.”
“Nina imani lazima utashangaa na kujiuliza ni kazi gani hiyo yenye malipo mazito lazima utakuwa na wasiwasi. Kweli kazi ni nzito inabidi mafunzo ya kina ndio maana tulikuandaa kwa ajili ya kukabiliana na kazi nzito. Malipo tuliyotoa ni kulingana na kazi nzito ambayo maisha ya muhusika huwa hatarini kwa asilimia tisini, ndio maana tumetoa malipo manono pindi mtu wetu akifariki kazini kwa ajili ya watu wanaomtegemea.
"Leo hii utakabidhiwa pesa zako taslimu bilioni 60 na umalizapo kazi yetu tutakupatia bilioni 40 zilizobaki kama utaifanikisha lazima tutakupa zawadi, mimi kama mimi ninakuahidi bilioni 30 sijui wenzangu,” aliwageukia wenzake.
“Sisi hatuahidi ila ataona baada ya kazi,” walijibu wajumbe wa mkutano.
“Kwanza kabla ya kukueleza ni kazi gani lazima uelewe sababu za kukupa hiyo kazi. Hili unaloliona ni kundi la watu kumi na sita hapa tupo watu kumi na mbili na wanne waliojitoa.
"Kundi hili lina shughuli nyingi ambazo ni siri zisizojulikana na mtu yoyote zaidi yetu sisi kumi na sita. Kwanza kabisa mimi ndiye muasisi wa kundi hili nchini na kuanza kukusanya watu walio tayari kufanya kazi nami nashukuru niliwapata na wakanielewa.
"Kundi hili lina sura mbili, kwa nje lina sifa nzuri kwani lipo mbele kutoa msaada kwa jamii ambao hudhani wanakula kumbe wanaliwa. Msaada tunaoutoa kama
kujenga makanisa makubwa bila msaada wa sadaka, huduma vijijini kama maji,umeme hospitali na huduma nyingine kwa jamii.
“Kitu kinachofanya watu wajenge imani juu yetu. mradi wa makanisa au kujenga vituo vya msaada ili kuwavuta karibu na kufanikisha azma yangu. Mradi tulioanza nao ni wa kuuza damu, nina imani kazi hiyo hata wewe uliifanya bila kujua. Ulipompata mteja na kumuacha hotelini vijana wetu aliingia na kumnyonya damu na kumchuna ngozi yake.
"Biashara hii inatuingizia pesa nyingi sana hasa baada ya wakubwa wengi kuathirika na ugonjwa wa ukimwi. Katika watu walioliingizia faida kubwa ulikuwa wewe hivyo tulikuandaalia asante lakini ajabu ulipotea kiajabu.
"Mradi wetu wa uuzaji wa damu nchi za nje uliingia dosari baada ya kugundua damu nyingi za watu wazima zimeathirika hivyo ndivyo tulivyobuni njia nyingine ya kupata damu iliyo safi kwa kuanzisha mradi wa kukusanya vijana kwa njia ya kuwapeleka nje kusoma au kufanya kazi.
"Kutokana na jinsi tulivyojijenga wazazi wao hawakuwa na pingamizi njia ile ilitusaidia kupata damu iliyo safi na biashara ya ngozi za watu. Ndani ya miaka mitano tulitengeneza pesa nyingi sana. Hakukuwa na biashara hiyo tu vilevile tulitumia kivuli cha kanisa kuingizia dawa za kulevya pamoja na kusafirisha madini na nyara za serikali nje.
"Ukweli kivuli cha dini kilituingizia pesa nyingi mpaka leo hii ni nani atayeamini kuwa sisi tunahusika na kazi hii hata mheshimiwa Rais sijui kitu zaidi ya kutupa ushirikiano na yeyote aliyetaka kufuatilia nyendo zetu tulimpoteza.
"Muungano wetu uliingia ufa miaka miwili iliyopita ufa baada ya wenzetu wanne kujitoa ambao waliweka mpasuko mkubwa. Mpasuko huo ulisababisha hata biashara yetu ya damu na ngozi za watu zikose soko na kusababisha tupate hasara ya trion 20.
“Vilevile kupotea mkataba wa trilioni 150 ambazo ni malipo yetu ya uuzwaji wa damu, ngozi, pembe na madini tuliyo wapelikea mawakala wetu.
"Hizo zilikuwa njama za wenzetu manne waliojitoa hasa Marry White ambaye ni mpenzi wa bosi wa shirika tuliokuwa tunawapelekea vitu vyetu. Cha kushangaza disc iliyokuwa na mkataba wa malipo ilipotea katika mazingira ya kutatanisha hata kumbukumbu nazo zilikuwa zimefutwa kwenye Computa.
"Tuliogopa kuwajulisha tumepoteza disc hata kumbukumbu, Mary White na wenzake wana mpango wa kuchukua zile hela ambazo ni nyingi sana. Kama watazichukua litakuwa pigo kubwa kwetu.
"Cha kufanya ni kuhakikisha watu hawa wanauwawa vilevile utumie ujuzi wako uweze kupata mkataba huu ambao upo katika ofisi za mawakala wetu. Utafanyaje? Sisi hatujui ndio maana tumekupa mafunzo mazito tofauti. Watu hawa ni hatari mafunzo yao na wewe hayatofautiani sana ila yako yamezidi.
"Ila wao ni wazoefu na kazi za mauaji ni watu makini sana hawana mchezo hasa Marry White ni mwanamke hatari sana hasa akigundua wewe ni adui yake anaweza kukufuata huku huku na kukumaliza..
"Mwanzo tuliwatumia vijana wetu wenye uwezo mdogo walikufa kama nzige, wengine walikufa hapahapa siku tuliyopanga waondoke ndio siku waliouawa kinyama.
Kitu kilichotutisha na kujua vita hii ni nzito ambayo inahitaji kujipanga vizuri.
Uamuzi tuliouchukua ndio wa kukuandaa wewe ili ukabiliane na tatizo lililo mbele yetu tuna imani kubwa na wewe kuwa utaiweza.”
Muda wote aliokuwa akiongea Father Gin macho yake yalikuwa hayachezi mbali na paji la uso wangu, nami vilevile sikuchezesha macho yangu zaidi ya kumwangalia na kumsikiliza kwa makini habari ambazo zilinisisimua.
Sio siri habari zile zilifanya nimkumbuke mzee wangu mtu niliye muona ana umuhimu wa pekee mzee Utakufalini. Maelezo yao yalikuwa sawasawa na aliyonieleza juu ya kugundua unyonyaji wa damu na uchunaji wa ngozi za binadamu. Hapo ndipo nilipogundua muuaji harisi wa familia ya mzee Utakufalini ni Father Gin.
Akili yangu uligundua kitu kingine na kuona kumbe duniani wapo watu wanaotumia vivuli vya ukarimu ili kuficha maovu yao, tena wanatumia vivuli vya udini au taasisi ili kuifumba macho serikali na wananchi wake.
"Thereza," nilishtushwa na sauti nzito ya Father Gin.
"A..bee," nilikuwa kama natoka ndotoni.
"Naona upo mbali vipi umenielewa?”
"Ni kweli"...maana kazi iliyopo mbele ni sawa na kuchezea ndani ya kinywa cha mauti."
“Usemayo ni kweli ndio maana tumekupa mafunzo ya kutosha ili kukabiliana nayo vilevile tumetoa malipo manono kwa kuzingatia uzito wa kazi.”
“Sasa ni hivi.." Father Gin alinyamaza kidogo na kupiga funda mbili za Whisky kisha aliendelea kusema:
"Thereza, nilikuwa sijamaliza maelezo yangu."
"Endelea tu Father."
"Mpasuko uliotokea kwenye kikundi chetu umesababisha shughuli zetu zote zisimame hata uvunaji wa vijana nao ulisimama ilibidi tutafute sehemu tuwahifadhi hao vijana ili kusubiri hali ikitulia tuweze kuvuna damu na ngozi na hakuna njia nyingine ni kuwaua hawa watu wanne Marry White na wenzake ambao wote wapo Italy na England.
“Ukifanikiwa kuwaua hawa utakuwa na kazi nyingine ya kwenda Ujerumani ambapo ndipo makuu ya wakala wetu mnunuzi mkuu wa vitu vyote tunavyo vivuna hapa nchini na nchi zingine za Afrika.
“Matawi yetu yapo Kenya, Uganda, Sudan, Afrika ya kusini, Nigeria na Senegal. Sehemu zote hizi tuna wakala wetu wanaokusanya watoto wa kivuli cha kituo cha kulelea watoto wenye maisha magumu. Ukweli mradi huu umetuingizia pesa nyingi sana, mradi wenye siri kubwa iliyojificha nyuma ya pazia. Na sio kwamba hakuna mawakala wengine ila tunaogopa tukibadili wakala hapo lazima tutapoteza pesa zetu trilion 150.
Sijui una swali lolote juu ya yote niliyokuileza?" Father Gin aliniuliza.
Kabla ya kuuliza swali nilikohoa kidogo kisha niliuliza.
"Samahani Father Gin."
"Bila samahani."
"Unataka kunieleza kuwa kuna baadhi ya watu waliouawa ndani na nje ya nchi pale wanapotaka kufuatilia jambo hili kati ya hao kuna mtu aliyepata mwanga wowote?"
"Hakuna."
"Hao ulio watuma wana ujuzi gani?"
"Ujuzi wao si mkubwa sana ila ni wazoefu.”
"Huoni kama uliwauza?" nilimuuliza swali.
"Kuwauza kivipi?”
"Utampelikaje mtu akapambane na mtu aliyemzidi uwezo?”
‘”Tulifanya kama shambulizi la kushtukiza.”
“Kama shambulizi la kushtukiza iweje wafe kirahisi namna ile?”
“Kwa kweli hata sisi ilitushitua.”
"Usinichekeshe Father Gin iliwashtua kivipi ikiwa bado mliendelea kuwatumia vijana wasio na ujuzi, mbaya zaidi unasema waliuawa hapahapa nyumbani kabla hawajaondoka huoni vita ipo hapahapa wala sio huko mnapotutuma?”
“Maneno yako ni mazito uliyosema sio kwamba tulikuwa na nia mbaya na wote walio uawa, ukweli tulichanganyikiwa tusijue nini cha kufanya," Father Gin alijitetea baada ya kumbana.
"Si kweli siwezi kukubaliana na usemacho yaani watu wanne wawazidi akili watu kumi na mbili tena inafikia hatua watu wanaingia mpaka ndani, nauliza adui yupo wapi ili nikianza kumtafuta nijue na mtafutia wapi?"
"Swali lako ni gumu."
“Kama unaelewa au huna habari ndani ya kikao hiki kuna watu wanatoa siri za kikao hivyo hakuna kitu kitachofanyika. Hata nikikubali nitakuwa nimesaini kifo, nitawezaje
kupigana na mtu nisiyemjua, naye ananijua vizuri mbaya yeye
yupo gizani mimi nipo peupe naonekana. Hamuoni hapo nakichezea kifo, ni wazi adui yenu anawaeleweni vizuri, kuliko ninyi mnavyo muelewa yeye.
“Nikinukuu kauli yako kuwa Marry White anatisha yupo tayari kumfuata
adui yakepopote alipo pale atapojua unamtafuta ni wazi anajua kuwa
mimi nimeandaliwa kwa ajili yao lazima watanizima kabla sijaianza
kazi yenyewe.
“Kwa nini hakunieleza mapema wala nisingekubali kupoteza muda wangu kwenye
mafunzo, nitawezaje kushindana na mtu anaye nifahamu. Inasikitisha mtandao mzito kama huu siri zenu zivuje. Lazima mchunguzane wenyewe kwa hali hii sipo tayari kuifanya kazi hii vilevile nipo tayari kuwalipeni gharama zenu zote."
"Usifike huko Thereza wewe ndiye tegemeo pekee la kundi letu tutakulinda."
"Usinichekeshe, mmeshindwa vipi hao mniweze mimi kwa taarifa yenu sitasaini mkataba vilevile nawahakikishieni siri hii itabakia moyoni mwangu mpaka naingia kaburini ila onyo mtu yoyote asinifuatilie nyendo zangu tutaonana wabaya," mtoto wa kike nilitoa mkwara mzito.
"Thereza usifanye hivyo basi sema unataka kiasi gani zaidi ya Bilioni 100 sema tupo tayari kukupa."
“Father Gin nielewe, ukitaka tuongelee habari ya kazi uondoe unafiki ndani ya kundi lako hapo tutakuwa tayari kuifanya kazi yako."
"S...sa....asa..."
"Hakuna cha sasa fanyia kazi niliyo kueleza kwa heri."
Nilinyanyuka na kuondoka bila kugeuka nyuma. Wote walibakia midomo wazi, nilitoka hadi ofisini kwa Dk Ray.
Itaendelea

No comments