Header Ads

Mama Diamond Platnumz amsifia Wema Sepetu...amemmwagia sifa tano

 Mambo juu ya mambo! Licha ya mzazi mwenza wa msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kutua jijini Dar, usiku wa saa 7:00 kisha kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa ya mama wa staa huyo, Snura Kassim ‘Sandra’, bado mzazi huyo amemmwagia sifa tano aliyewahi kuwa ‘mkwewe’, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’, Wikienda lina ubuyu kamili. 

KUTUA KWA ZARI 
Habari kutoka kwa chanzo makini ambacho ni mtu wa karibu wa familia hiyo kilidai kuwa eti Zari alitua Dar usiku wa manane wa kuamkia Alhamisi iliyopita akitokea nchini Afrika Kusini ‘Sauz’ ili kumfumania Diamond baada ya kuwepo kwa tetesi za kurudiana na Wema. Kilidai kuwa, mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Zari hakusubiri kupokelewa na mtu aliyetumwa kumpokea aitwaye Q-Boy, badala yake alichukua usafiri binafsi na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Diamond, Madale jijini Dar. Hata hivyo, alipofika nyumbani hakumkuta Diamond kwa kuwa alikuwa kwenye shoo mkoani Mbeya hivyo ishu ya kumfumania ikawa imeyeyukia hapo. 

KWENYE SHEREHE SASA Ilifahamika kwamba, sherehe ya kuzaliwa ya mama Diamond iliyokuwa ifanyike usiku huo wa
Alhamisi haikufanyika badala yake ikafanyika usiku uliofuata wa Ijumaa na kuhudhuriwa na watu lukuki wakiwemo mastaa wa kada mbalimbali Bongo na Diamond mwenyewe akiwa amerejea kutoka Mbeya na timu yake ya Wasafi Classic Baby (WCB). 


MAMA DIAMOND, ZARI WASEREBUKA
 Katika sherehe hiyo ya kukata na shoka, ili kuonesha wapo vizuri na hakuna ‘mizinguo’ mama Diamond na Zari walikula na kunywa pamoja huku wakiserebuka usiku kucha kupitia muziki uliokuwa ukiporomoshwa na bendi laivu. “Jamani mama Diamond ameserebuka vya kutosha na mama Tiffah ili kuonesha wapo vizuri tofauti na watu wanavyowachukulia,” kilidai chanzo hicho. 

MAMA DIAMOND AMMWAGIA SIFA WEMA 
Chanzo hicho kilidai kwamba, licha ya shughuli hiyo ya kihistoria na kuonesha mbwembwe zote na Zari lakini bado mama Diamond alijikuta akimmwagia sifa Wema kwa kitendo chake cha kumtakia heri ya siku yake ya kuzaliwa, jambo ambalo hakulitarajia. “Unajua kitendo cha Wema ‘kumuwish happy birthday’ kwenye mitandao ya kijamii kimemjengea mama Diamond picha tofauti sana juu yake na imekuwa ni kama ‘sapraizi’ kwake na amemfariji sana. “Amejikuta akitamka waziwazi sifa tano alizonazo Wema kuwa, moja ameonesha ni mtu mwema asiye na kinyongo yaani ana
roho safi, pili ameonesha ni mwenye hekima, tatu ni mwenye adabu kwa mzazi yeyote, nne ameonesha kiwango cha juu cha busara na tano ameonesha ni mtu mkarimu sana,” kilinyetisha chanzo hicho kwa shati la kutotajwa gazetini. 

 
BOFYA HAPA KUMSIKIA MAMA DIAMOND 
Akizungumza na Wikienda saa kadhaa baada ya shughuli hiyo, mzazi huyo alisema anawashukuru watu wote waliomtakia heri ya siku yake ya kuzaliwa na kuhudhuria kwenye shughuli hiyo iliyoweka rekodi ya aina yake. “Kiukweli ilikuwa shughuli kubwa maishani mwangu, mimi ninachoweza kusema tu nashukuru kwa kila jambo walilonifanyia,” alisema mama Diamond akionekana mwenye furaha. Alipoulizwa juu ya sifa alizommwagia Wema, mama huyo alisema kuwa Wema amemfariji mno na kumshangaza
kwani hakutarajia kama angemtakia heri ya siku yake ya kuzaliwa na kupata ‘komenti’ kibao ambazo hazina matusi kama zamani. “Ameonesha ni mtu mkarimu sana na ana watu wengi na wazuri mitandaoni,” alisema mama Diamond. 


WEMA NAYE
 Kwa upande wake Wema alisema kuwa kinachoonekana watu wengi wanapenda yeye na Diamond wawe kwenye bifu kwa kuwa hujipatia wafuasi wengi kwenye kurasa zao wanapoweka vitu vinavyowahusu lakini ukweli ni kwamba hana tatizo na familia hiyo badala yake anatamani washirikiane katika kazi zao za sanaa. Hivi karibuni kumekuwa na habari nyingi zinazohusiana na Wema na Diamond kurudiana mara baada ya kuanza kupeana sapoti kwenye kazi zao mitandaoni huku kila mmoja akikanusha kuwa hawajarudiana

CREDIT: IJUMAA WIKIENDA/GPL

No comments