Header Ads

Michael Yogayoga: Mwanasarakasi aliyekataa uraia wa Ujerumani

Kijana Mtanzania, Michael Elias Mondosha maarufu kama Michael Yogayoga mzaliwa wa Mpanda mkoani Katavi akifanya yake juu ya meza ndani ya ofisi ya Global.
SASA imebaki historia tu, kwani hakuna au hufanyika kwa nadra sana, hii ni michezo ya sanaa za mazingaombwe na sarakasi ambayo zamani ilikuwa ikifanywa katika shule mbalimbali lengo likiwa kuwaburudisha wanafunzi.
Yawezekana ni maendeleo ya sayansi ya teknolojia, maonyesho ya sanaa hizo hayafanyiki mara kwa mara katika shule za msingi hata zile za sekondari.
Michael Yogayoga (1)
...Akiendelea kuonyesha manjonjo.
Wakati huo, michezo hii iliwatia ujasiri watoto na kuona mambo mengi yanayoonekana kuwa magumu yanawezekana pale inapokuwepo nia kwa mtendaji.
Kijana Mtanzania, Michael Elias Mondosha maarufu kama Michael Yogayoga mzaliwa wa Mpanda mkoani Katavi yeye ni mwanasarakasi aliyebobea na bado anafanya maonyesho yake, bahati mbaya mengi anafanya nje ya nchi.
Michael Yogayoga sanaa yake hiyo anaifanya katika nchi mbalimbali za Ulaya lakini makazi yake yapo nchini Ujerumani.
Michael Yogayoga (2)
Michael Yogayoga akiwa nje ya ofisi ya Global.
Katika mahojiano yake na Championi Jumamosi hivi karibuni, Michael Yogayoga anasema tofauti na hapa nchini, Ulaya sanaa hiyo ina wapenzi wengi bado.
“Nilionekana nina kipaji cha sarakasi nilipokuwa na miaka sita nikiwa nyumbani kwetu Mpanda mkoani Katavi, lakini baada ya kuanza kujitambua kuna jamaa alinichukua na kunipeleka Dodoma.
“Nilipofika huko mwaka 1987 nilijiunga na kundi la sanaa lililokuwa chini ya Mzee Mwinamila.
“Nilikaa na mzee huyo kwa muda mpaka nilipopata bahati ya kupelekwa na serikali nchini China kwa ajili ya mafunzo kuongeza ujuzi wa sarakasi.
“Baada muda nilirejea nchini na mwaka 1993 nilienda tena kusoma sanaa hiyo katika Chuo cha Saana Bagamoyo, nilipohitimu nikaajiliwa  kituo cha utamaduni Bujola mkoani Mwanza, hata hivyo sikudumu kituoni hapo nikaanza kujitegemea.
Michael Yogayoga (3)
AFISA UTAMADUNI
“Hata hivyo mwaka 1997 nilikutana na mwandishi wa habari wa Redio Burundi, yeye aliniunganisha na jamaa fulani hivi ambao niliingia nao mkataba wa kuzunguka nchi mbalimbali za Afrika.
“Baada ya mkataba huo kumalizika nilirejea nyumbani na kuajiriwa serikalini kama Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Maswa mkoani Shinyanga, hiyo ilikuwa mwaka 1999.
“Kazi hiyo nilifanya kwa muda mfupi kisha nikaenda kuanzisha bendi ya Mwanamuziki, Saida Kaloli, nilifanya naye kazi kwa miaka mitano hivi,  baada ya hapo ndipo nikapata dili la kwenda Ulaya.
AINGIA REKODI ZA GUINNESS
“Mwaka 2007 niliingizwa katika kitabu cha rekodi duniani cha Guinness kutokana na kazi zangu za sarakasi nikaanza kuandaliwa mazingira ya kuwa nyota kwa kushiriki katika matukio mbalimbali makubwa Ulaya.
 AKATAA URAIA WA UJERUMANI
“Baadhi ya viongozi wa Serikali ya Ujerumani baada ya kuvutiwa na kazi yangu, walianza harakati za kutaka kunibadili uraia bila ya mimi kujua, nilipogundua njama zao hizo nilikataa kufanya.
“Niliona ni bora niendelee kuwa Mtanzania hata kama hali ya kiuchumi ya kwetu siyo nzuri, ni bora kuishi kwa amani kuliko kubaguliwa japokuwa napata fedha nzuri.
“Ukiachana na hayo, pia hivi karibuni natarajia kwenda Ufaransa kufanya shoo katika tuzo ya kumsapoti mtoto wa Afrika na watoto wanaoishi katika mazingira magumu duniani,” anasema Michael Yogayoga.
AZINDUA DVD YAKE
“Kwa sasa nipo hapa nchini nimekuja kwa ajili ya kuzindua DVD (video) yangu ambayo itakuwa na mambo mengi yanahusiana na mchezo wa sarakasi.
“Katika DVD hii, nimeshirikisha wanasarakasi mbalimbali kutoka mataifa 18 ya Afrika pamoja na Marekani, mambo yatakapokuwa tayari kila mtu ataipata, ina burudani nzuri ndani yake.
“Fedha zitakazopatikana katika DVD hiyo natarajia kuzitumia katika ujenzi wa kituo changu cha kuendeleza michezo mbalimbali hapa nchini ninachotarajia kukijenga mkoani Dodoma ambako nina eneo la hekari 15,” anasema Michael Yogayoga.
 AMUIBUA WABOGOJO
“Nikiwa na Saida Kaloli nilifanikiwa kumtoa na kutambulisha Wabogojo (Athuman Ford) hapa nchini baada ya Mr Nice (Nice Lucas) kutaka nifanye naye video ya wimbo wake wa Kikulacho.
“Nilikataa kufanya naye video hiyo kwa sababu sikupenda kuchanganya mambo kwani wengi walizoea kuniona nipo na Saida Kaloli hivyo wangeniona tena kwenye video hiyo isingekuwa vizuri.
“Kutokana na hali hiyo nilimwambia Nice kuwa nitampatia mtu afanye naye kazi ni mzuri na atafurahia kazi yake, ndipo nilipoamua kumpeleka Wabogojo kwa Mr Nice,” anasema Michael Yogayoga.
WANASARAKASI MSIKATE TAMAA
“Nawaomba wasanii wenzangu kutokata tamaa pindi wanapotafuta mafanikio, huwezi kujua ni siku gani mambo yatakuwa sawa hivyo inatubidi tupambane siku zote za maisha yetu.
“Jambo jingine ninalopenda kuwashauri ni kwamba majungu na fitina havijengi tunatakiwa kuwa kitu kimoja ukimuona mwenzako anafanikiwa ni vizuri ukamuuliza amefanyaje ili na wewe uweze kupata mwanga au njia ya kupita,” anamaliza Michael Yogayoga.

CHANZO: CHAMPIONI

No comments