Header Ads

Pluijm: Aisee Medeama lazima tuwafunge

pluijmKocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
Wilbert Molandi, Dar es Salaam
KOCHA wa Yanga, Hans van Der Pluijm ametamba kuwa ni lazima wawafunge wapinzani wao, Medeama ya Ghana katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika ili wafufue matumaini ya kusonga mbele.
Yanga tayari imepoteza michezo miwili ya hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa kufungwa na MO Bejaia ya Algeria na TP Mazembe bao 1-0 katika kila mchezo.
Jana, Shirikisho la Soka Afrika (Caf) liliithibitishia Yanga kwamba ombi lao la kutaka kucheza na Medeama Jumamosi ijayo limepitishwa, hivyo itacheza na Medeama siku hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Pluijm alisema mechi yao dhidi ya Medeama ndiyo itawapa dira ya wao kusonga mbele kutokana na kuhitaji pointi.
Pluijm alisema, katika mechi hiyo watapambana kufa au kupona pamoja na wachezaji kuhakikisha wanafikia malengo yao waliyoyaweka ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Aliongeza kuwa, tayari ameona upungufu uliowasababishia vipigo katika mechi mbili zilizopita na tayari ameiongezea makali safu yake ya ushambuliaji ambayo inapoteza nafasi nyingi za kufunga.
“Nimeshajua upungufu wetu uliotusababishia tushindwe kupata matokeo mazuri kwenye mechi mbili tulizocheza dhidi ya MO Bejaia na TP Mazembe.
“Upungufu ulikuwepo kwenye safu ya ushambuliaji iliyoshindwa kutumia nafasi nyingi tulizokuwa tunazipata za kufunga, hivyo ninaendelea kukiandaa kikosi changu ili tupate ushindi mechi na Medeama.
“Naamini hakuna kitakachoshindikana, kama tukiwafunga, basi wachezaji watatengenezeka kisaikolojia na kushinda michezo ijayo, kwani wachezaji wangu wanaonekana kuwa na hamu ya ushindi hali inayosababisha wacheze kwa presha kubwa,” alisema Pluijm.
Yanga bado inaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam huku ikiweka kambi Bahari Beach Hotel.
CHANZO; CHAMPIONI

No comments