Header Ads

PROF JAY, KALA JEREMIAH WATIMBA GLOBAL TV WAFUNGUKA MAZITO JUU YA KAZI ZAO

MSANII mkongwe wa Hip Hop, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay na ‘mdogo wake’ Kala Jeremiah, jana walitinga katika studio za Global Tv Online na kufanya mahojiano yaliyogusa maeneo mbalimbali.

Wafanyakazi wa Global Publishers, Nyemo Chilongani (kushoto) na Andrew Calos (kulia) wakifanya yao na Kala Jeremiah.
Jay, anayechukuliwa kama ndiye aliyeshawishi umma kuukubali muziki wa kizazi kipya kutokana na mashairi yake ya kuelimisha, anasema alipofika bungeni baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Mikumi, alipokelewa na viongozi wote kwa kumhimiza kutoacha muziki, kwani ana kipaji nao.
“Mimi nilikuwa mbunge kabla sijaingia bungeni kwa sababu siku zote nyimbo zangu zilikuwa ni zenye kuelimisha, kutia moyo na kukosoa pale panapostahili, kule viongozi wengi waliniambia nisiache muziki na mimi siwezi kuacha, lakini hivi sasa nimepewa jukumu na watu wa Mikumi, la kuwa mtetezi wao pale mjengoni, kwa hiyo nitakuwa mbali kidogo na mashabiki, lakini siwezi kuwaacha kabisa, ndiyo maana nimewadondoshea hii ngoma mpya ya Kazi Kazi.”
Jay, alisema siku zote amekuwa ni mtu wa kuwapa nguvu watu waliokata tamaa, akisema yeyote anaweza kuwa yeyote.
“Ndiyo maana kichupa (video) ya wimbo huu nilienda kushutia kule Uwanja wa Fisi, kwa watu wa chini. Mimi nafahamu maisha yetu yote yalivyo magumu, lakini nimeweza kupambana na leo ni Mbunge, ndoto zangu ni kuwa Rais, kwa hiyo hata wao wanaweza kusimama katika ndoto zao na kufikia malengo bila kujali wako wapi kwa sasa,” alisema.
Kuhusu kususia kwao vikao vya bunge, Jay ambaye ni mbunge kupitia Chadema inayounda Ukawa, alisema wanafanya hivyo kwa sababu ndiyo njia pekee ya kutuma ujumbe kuwa hawaridhiki na kufungwa kwao mdomo, kwani hicho ndiyo amekuwa akikipigania siku zote.
“Mimi ni Voice of speechless yaani Sauti ya wasiosikika, kwa hiyo kama tunafungwa midomo tusiseme tulichotumwa na wapiga kura wetu siyo sawa, tumekatazwa kufanya mikutano, sasa leo mimi nimewapigania wapiga kura wangu na nimepewa fedha za maji, nitafanyaje kuwaeleza kilichotokea? Tunasusia vikao ili kupeleka ujumbe kuwa haturidhiki na kinachotokea bungeni, bunge linatakiwa kuisimamia serikali, lakini kilichopo ni serikali kulisimamia bunge.”
Wakati Jay ambaye ameachia kibao chake cha Kazi Kazi akisema hayo, Kala Jeremiah, rapa mwingine mkali nchini, naye alisema yeye ni mtetezi na mpigaji wa watoto yatima, kwani kile wanachokipata siyo mahitaji yao halisi.
“Watoto yatima waliopo katika makambi, wanachokipata ni kula, kulala na chakula, wanaohusika na watoto hawana lolote wanalojali zaidi kuwahusu, wanajadili mambo ya watoto kwenye makaratasi, kompyuta wakiwa kwenye viyoyozi, hawa viumbe wana mahitaji mengi zaidi ya hayo.
“Wanaohusika na watoto ni kama wamewatelekeza, mimi nimeshiriki na kuona matamasha mengi, yanayohusu Ukimwi na vitu vingine, lakini sijawahi kuona tamasha la watoto yatima, ndiyo maana nikatoa wimbo huu wa Wana Ndoto, kwa sababu na wao wana malengo wanayotaka kuyafikia, lakini hawapewi sapoti inayotakiwa.”
Kuhusu namna anavyoienzi lugha ya Kiswahili, alisema kwa kuanzia, aliamua kushughulika na jina la mtoto wake, kwani wazazi wengi wa Kitanzania wanawapa watoto wao majina yenye asili ya kizungu na kiarabu, yeye ameamua kumpa mtoto wake wa kwanza jina la Alama.
“Huyu akikua, akienda nje ya nchi, wenzake watamuuliza hili jina lako lina maana gani, atakapowaambia, utakuwa ndiyo mwanzo wa kukikuza Kiswahili, hili ndilo tunalotakiwa kulifanya wazazi wote, ni wajibu wetu kuhakikisha asili yetu haipotei,” alisema.   
 

No comments