Header Ads

Shoga, mung’unya likikomaa haliliki!

Mmh! Makubwa madogo yana nafuu, kwa kweli katika tunda ambalo hunisikitisha maishani mwangu ni Mung’unya. Tunda hili ukitaka kulila liwahi bado changa, lakini likikomaa haliliki tena na hugeuka kata ya maji. Basi mwakwetu kuna watu hawana haya, waliopinda tangu udogoni na kujificha katika mavazi ya heshima na maneno matamu, lakini tabia zao ni rangi ya kaniki hata ukifua vipi haiwezi kuwa nyeupe kwa vile weusi ni rangi yake ya asili.
Ndiyo maana nilimueleza shoga  yangu kuwa asimlaumu dobi kwa rangi ya kaniki kwa kuamini anaweza kuifua na kufanya weusi kuwa weupe. Nilimweleza ukitoka weusi si kaniki tena na siku zote asili ya kaniki ni weusi.
Mmh! Naona mimacho imekutoka pima kutaka kujua  na kuniona kama nakulisha chakula cha Kihindi chenye pilipili nyingi!
Usikonde shoga yangu,  nitakutonya mambo ya kutia aibu yanayofanywa na wanawake wenzetu walio ndani ya ndoa. Kuna mama mtu mzima ambaye alitakiwa kutulia ndani ya ndoa yake, amekuwa akimdhalilisha mumewe kwa kutembea nje ya ndoa yake na wanaume zaidi ya mmoja bila aibu tena kujiona kufanya vile ni haki yake.
Shoga yangu mmoja ambaye ni jirani yake na ni mtu wake wa karibu sana, tabia ile ilimchefua sana na kuamua kumwambia unayofanya siyo mazuri unamuaibisha mumewe. Japo mama huyu mtu mzima anayetakiwa kuwa na wajukuu alisingizia mumewe hamfikishi.
Ha! Jamani mpaka leo mna watoto unasema hakufikishi? Unataka kuniambia kuugawa mwili wako kama pipi ni njia ya kukidhi haja zako?
Shoga yangu aliendelea kunipasha mtoto wa mwanamke mwenzake kuwa, majibu ya mtu mzima huyu asiye na haya wala kujua vibaya ambaye akimuangalia vibaya utasema ni mtu wa swala tano.
Eti  kuwa amwache yeye inamhusu nini, kwa vile anachotumia kipo mwilini mwake wala si cha mtu. Mmh! Makubwa jamani kama kitu kikiwa mwilini mwako unakitoa tu bila hata kujiheshimu kuwa wewe mke wa mtu?
Kama ni hivyo basi vua hiyo hijabu uliyoifanya kichaka cha kukuonesha kondoo, kumbe ndani ni chui mbaya kwa wanaume ili uungane na makahaba wenzako wauza miili yao, kuliko kutudhalilisha wanawake tunaojua nini maana ya ndoa kwa kuziheshimu ndoa zetu.
Najua nimekugusa na wewe mwenye tabia kama hii, ushapinda mdomo kama kiatu cha mwanajeshi mstaafu  kilichokwisha, ndiyo tabia yako ya kuugawa mwili kwa wanaume ovyo kama mapokezi ya nyumba ya wageni kila mgeni lazima apitie.
Kwa hili siwezi kukuacheni mchafue sifa za ndoa kama una hamu ya wanaume kwa nini usiombe talaka kuliko kumtafutia magonjwa mwenzio?
 Nasema sipendi na sitaki kuisikia tena tabia hii, nasema na wewe unayejijua na kujibu majibu ya kifedhuli tena nakwambia ukome kumdhalilisha mumeo. Mbona wenzako wametulia kwenye ndoa zao kwani miili yao wameazima kwa watu? Si yao.
Inawezekana haya ninayoyasema yataingilia kulia na kutokea kushoto, siwezi kukulaumu kwa vile umeshaharibika ukubwani kama mung’unya na tabia yako kama rangi ya kaniki hata ukimaliza bahari nzima na sabuni zote za duniani bado rangi yako itabakia nyeusi.
Kweli nimeamini makahaba si wauza miili usiku wengine tunao ndani ya ndoa zetu. Unashtuka nini? Hebu mchunguze mwenzako sasa utaniambia kuwa mkeo ni jina ila kahaba baridi ambaye ni hatari na bomu likipasuka litakuua.

No comments