Header Ads

Wanafunzi 7,805 waliofukuzwa, 382 tu kurudi UDOM


Wanafunzi ambao watarejea kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) baada ya uchambuzi kumalizika na kupatikana idadi ya wanafunzi ambao wana sifa za kuendelea na masomo, serikali imetangaza orodha ya

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako asema kuwa kwa kipindi chote serikali ilikuwa ikifanya uchambuzi ili kuona ni wanafunzi gani walikuwa na sifa za kusoma kozi hiyo maalum ambayo ilianzishwa kutokana na tatizo la walimu wa Sayansi.
Baada ya uchambuzi wa kina serikali imebaini kuwa takriban wanafunzi 290 waliokuwa wakisoma stashahada ya ualimu wa sekodari na wengine 1,181 wa stashahada ya ualimu wa shule ya msingi, wakiwa hawana sifa kabisa ya kuendelea na programu hiyo na wameshauriwa kuomba programu nyingine katika vyuo vingine zinazoendana na sifa zao.
Ifuatayo ni sehemu ya taarifa iliyotolewa na Wazir Ndalichako..
MAAMUZI YA SERIKALI
Kundi la Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari
(i) Kwa kuwa uchambuzi umebainisha kuwa Wanafunzi wenye ufaulu wa Daraja la I na la II ambao pia wamefaulu masomo mawili ya Sayansi kwa kiwango cha C-A ni 382 (mwaka wa I -134 na mwaka wa II - 248), wanafunzi hao ndiyo pekee watakaorudishwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma ili wakamalizie mafunzo yao katika Chuo hicho.
(ii) Wanafunzi 4,586 wa mwaka wa I wa Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika Vyuo vya Ualimu vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo yao.
(iii) Wanafunzi 1,337 wa Mwaka II watahamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Korogwe na Kasulu kumalizia masomo yao.
(iv) Wanafunzi 290 waliokuwa wamedahiliwa kusoma Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari Masomo ya Sayansi na Hisabati ambao hawana sifa stahiki wanashauriwa kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizo nazo kwenye chuo chochote wanachotaka wao.
Kundi la Programu ya Ualimu wa Elimu ya Msingi
Wanafunzi katika kundi hili hawakuwa sehemu ya program maalum ya kupunguza uhaba wa walimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati. Walikuwa wanaandaliwa kufundisha shule za msingi wakati lengo la Programu Maalum ilikuwa ni kukabiliana na tatizo za uhaba wa walimu wa Sekondari. Maudhui ya program waliyokuwa wanasoma hayakuwa sawasawa na yale ya Programu ya Ualimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati.
(v) Wanafunzi 29 wa mwaka wa II wenye Cheti cha Daraja IIIA waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Ualimu wa Shule za Msingi watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo yao kwa gharama zao wenyewe.
(vi) Wanafunzi 1,181 waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Kawaida ya Ualimu wa Elimu ya Msingi waombe mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo mahali popote watakapotaka wao.
GHARAMA ZA MASOMO
Serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM. Aidha, wanafunzi watakaohamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Serikali watapewa mkopo wa kiasi cha Sh. 600,000/= kwa mwaka ambayo ni ada ya Mafunzo ya Ualimu itakayolipwa moja kwa moja Chuoni.
HITIMISHO
(i) Wanafunzi wote wanaorejeshwa Chuo Kikuu cha Dodoma wataanza masomo mwezi Oktoba 2016.
(ii) Wanafunzi watakaohamia katika Vyuo vya Ualimu wataendelea na mafunzo yao mwezi Septemba mwaka 2016.
(iii) Wanafunzi wote watatakiwa kuripoti wakiwa na vyeti vyao halisi vya Kidato cha Nne ambavyo vitahakikiwa kabla hawajapokelewa rasmi kwenye vyuo walivyopangiwa.

No comments