Header Ads

WAUZA SURA WAMEHARIBU SOKO LA FILAMU BONGO

 
MSANII mkongwe katika filamu Bongo, Sabrina Rupia ‘Cathy’ ambaye amejihusisha na sanaa hiyo tangu mwaka 1998 akiwa na Kundi la Nyota Ensemble (Mambo Hayo), amekutana na Risasi Mchanganyiko na kufunguka mambo mbalimbali juu ya tasnia hiyo inayoonekana kuyumba.
Aliwatupia lawama wadau wa filamu, aliodai wamekuwa wakiwaingiza wasichana  wanaokutana nao katika maeneo ya starehe au baada ya kuvutiwa na muonekano wao. Cathy alisema wasichana wanaoingia katika filamu wanaitumia tasnia hiyo kama sehemu ya kutangaza biashara zao chafu, maana wamekuwa wakivaa mavazi ya nusu utupu. Yafuatayo ni mahojiano kamili na msanii huyo mkongwe.
Risasi: Ni vipi unaweza kusema filamu imevamiwa na machangudoa? Cathy: Kiukweli kwa sasa kuna watu wengi wasio na vipaji, wameingia kwenye fani hii kutokana na muonekano wao tu ambao wamegeuza kama sehemu ya kuuza sura na mapaja yao, kitu ambacho kimevuruga kabisa tasnia na kusababisha soko kuporomoka. Risasi: Unafikiri hao wanaoharibu tasnia wametoka wapi? Cathy: Hawa wanatokana na wale maprodyuza wanaowaona wasichana wazuri kimuonekano tu barabarani au sehemu za starehe na kuwaweka kwenye filamu wakiwa hawajapitia kwenye vikundi ili waijue sanaa ni kazi kama kazi nyingine kwamba wanatakiwa waiheshimu.


Risasi: Nini kifanyike ili kutokomeza hali hii? Cathy: Nawaomba waondoke tu wenyewe watuachie sanaa tunaojua maana yake, pia hawa kaka zetu wanashoboka na muonekano barabarani, wanaua soko. Risasi: Umecheza filamu ngapi mpaka sasa? Cathy: Zipo nyingi ambazo ni za kushirikishwa, lakini zangu mwenyewe ni kama sita hivi. Risasi: Kuna skendo ilivuma sana kwamba unatoka kimapenzi na msanii mwenzako, Vincent Kigosi ‘Ray’, hii ikoje? Cathy: Sijawahi kutoka naye, Ray ni rafiki yangu wa kawaida, pia ni rafiki wa mume wangu,  sijawahi kutoka nje ya ndoa, mume wangu ananiridhisha kwa kila kitu. Risasi: Una muda gani kwenye ndoa? Cathy: Huu ni mwaka wa 14 sasa, watoto ninao wa kunitosha, siwezi kusema idadi yake maana huwa sipendi. Risasi: Nini siri ya kudumu kwenye ndoa? Cathy: Siri kubwa mimi ni msikivu, muwazi na siishi maisha ya kuigiza. Risasi: Unafikiri kwa nini ndoa za wasanii wenzako mara nyingi hazidumu? Cathy: Wengi wanaolewa kwa fasheni ili nao waonekane wako kwenye ndoa kwa sababu f’lani ameolewa au kuoa, kifupi wanakurupuka. Risasi: Wasanii wa kike wanatajwa kujihusisha na usagaji, wewe ukiwa mmojawapo, unasemaje? Cathy: Sijawahi na siwezi kufanya hivyo maana hiyo ni laana, nimelelewa kidini, wengi wanaofanya hivyo ni wale waliosoma shule za ‘boarding’ na waliolelewa hovyohovyo. Risasi: Lakini ni kweli kuna wasanii wanaofanya mambo hayo? Cathy: Lisemwalo lipo, huwezi kuwatambua kirahisi. Risasi: Ni kitu gani unafanya kwa watoto wako ili wasije kujiingiza kwenye tabia kama hizo? Cathy: Wanangu wako shule ya kwenda na kurudi ‘day’ na sipendi kuwapeleka ya kulala maana wengi wanaoharibika na usagaji na ushoga ni wale wanaosoma shule za kulala maana uangalizi unakuwa mdogo. Risasi: Kumeibuka tabia ya mastaa wa kike kuwa kimapenzi na wasanii wa kiume ambao kiumri ni wadogo kwao, unalizungumziaje? Cathy: Kama wao wanaona sawa siwezi kuwazungumzia, ila ninashangazwa sana maana kipindi cha usichana wangu nilikuwa nawaona wanawake wakiolewa na wanaume wanaowazidi umri, hata mume wangu ni mkubwa kwangu,
naona ni kizazi cha kidijitali. Risasi: Vipi kuhusu wale wanaobadilisha mabwana ili kupata umaarufu? Cathy: Naona wamepoteza mwelekeo, wanataka ‘shortcut’, hawataki kufanya kazi ili ziwatangaze bali wanabadili mabwana ili wawe mastaa kitu ambacho siyo kizuri. Risasi: Nini unachojivunia katika fani? Cathy: Kwanza sanaa imenipatia mume, imenitangaza ndani na nje ya nchi. Risasi: Unawashauri nini wasanii wenzako kwa jumla? Cathy: Waiheshimu kazi hii maana ndiyo kazi yetu na wale wavamizi waondoke watuache wasanii wa kweli


CREDIT: RISASI MCHANGANYIKO

No comments