Header Ads

Wawa arudi kwao, kuikosa Yanga Ngao ya Jamii


BEKI tegemeo wa Azam FC, Pascal Wawa ataendelea kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi miwili akiuguza majeraha ya goti. Kwa hiyo, Wawa anatarajia kuukosa mchezo wa Ngao ya Jamii utakaoikutanisha timu yake na Yanga mwezi ujao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Wawa aliondoka usiku wa kuamkia jana saa 8:25 kwenda kwao Ivory Coast kwa mapumziko maalum ya kuuguza goti lake.
Beki huyo alikuwa nje ya uwanja tangu Aprili, mwaka huu. Akizungumza na Championi Jumamosi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) usiku huo, Wawa alisema atakosa mechi hiyo baada ya kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu nchini Afrika Kusini alipokwenda kutibiwa na Shomari Kapombe.
“Ninatarajia kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi miwili, hiyo ni baada ya kufanyiwa vipimo na kugundulika matatizo yangu, hivyo hivi sasa nipo nje nikiendelea na matibabu.

“Naelekea nyumbani Ivory Coast kwa ajili ya kupumzika na kuiangalia familia yangu, kikubwa ninataka nirejee uwanjani nikiwa nipo fi ti,” alisema Wawa. Daktari Mkuu wa Azam, Juma Kwimbe alithibitisha Wawa kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili huku akitarajiwa kuanza mazoezi mepesi Septemba, mwaka huu.
“Wawa anatarajiwa kuukosa mchezo wetu wa Ngao ya Jamii tutakaoucheza Agosti, pia na baadhi za mechi za mwanzoni za ligi kuu kwani anauguza majeraha ya goti,” alisema Kwimbe.
CHANZO:CHAMPIONI

No comments