Header Ads

Bi Harusi Atekwa saa chache baada ya kufanyiwa Kicheni Pati Moro!


 Bi harusi Asha Halili, mkazi wa Kichangani mkoaniMoro.
STORI:  DUSTAN SHEKIDELE, RISAJI JUMAMOSI MOROGORO: Katika hali ya kushangaza, bi harusi Asha Halili, mkazi wa Kichangani mkoani hapa ambaye alikuwa afunge pingu za maisha Agosti 12, mwaka huu (jana), amedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana ikiwa ni saa chache tu baada ya kutoka kwenye sherehe yake ya kufundwa Kicheni Pati, Risasi Jumamosi lina mkanda mzima.

TUJIUNGE NA CHANZO Kwa mujibu wa chanzo makini, mrembo huyo ambaye amehitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), hivi karibuni, alimpata mchumba aliyetajwa kwa jina la Ramadhan wakakubaliana kufunga ndoa hivyo mipango ya maandalizi ikafanyika na hatimaye siku za kufanya sherehe zikawadia.

MSIKIE HUYU “Si muda mrefu tangu amalize masomo yake, walikubaliana na mwenzake wafunge ndoa. Vikao vikaanza kuunguruma. Upande wa bwana harusi walikuwa wakiandaa harusi huku upande wa bi harusi wakiandaa sherehe ya Kicheni Pati na Send Off. “Wanandugu sambamba na majirani,  tukajichangachanga, tukahimizana kuchangisha vimichango vidogovidogo kuhakikisha tunamfanyia shughuli ya kueleweka mtoto wetu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
KICHENI YAFANYIKA VIZURI “Kicheni Pati ilifanyika vizuri Jumamosi ya Agosti 6 kwenye Ukumbi wa Road View, Area 5, waalikwa tukala, tukanywa na tukamfunda vizuri bi harusi wetu ili anapokwenda kwa mume asiwe mzigo, kisha tukampa na zawadi. Sasa tukawa tunajiandaa na sherehe ya kumuaga (Send Off) ambayo ilikuwa ifanyike kesho yake (Agosti 7).”
KHAA! KATEKWA! Chanzo hicho kilizidi kufunguka: “Baada ya bi harusi kutoka kwenye sherehe hiyo, alirudi nyumbani kwao, lakini
kesho yake (Jumapili iliyopita), walitokea watu wanaodaiwa kumfahamu, mmoja inasemekana ni mtu wake wa zamani kabla ya kuchumbiwa, yaani mchepuko, wakatokomea naye kusikojulikana.”
HAPATIKANI HEWANI! “Hali hiyo ilizua taharuki zaidi, kwani hata alipopigiwa simu yake ya mkononi, hakuwa akipatikana hewani! Ungekuwa wewe mwandishi unadhani ungesemaje? Maana kwa vyovyote vile huyo jamaa yake wa zamani anajua wazi kwamba, mwenzake anaolewa, sasa kumchukua na kuzima simu yake lengo lake nini? “Bi harusi ni msomi, tena wa chuo kikuu, naamini hakuondoka na wale watu kwa ridhaa yake kwa vile anajielewa. Pengine jamaa alimfuata kwa kumlaghai ampe zawadi, kumsalimia au kumuaga kabla ya kwenda kuanza maisha ya kuwa mke, na yeye bila kujua, akaenda. Kufika ndani ya gari, wakafunga milango, wakaondoka naye huku wakimwamuru azime simu yake.
” ILIVYOKUWA “Tunaambiwa kuwa, bi harusi akiwa nyumbani kwao siku hiyo ya kutekwa, kuna wakati alitoka nje huku akiongea na simu, akawaambia ndugu zake kwamba, anarudi muda huohuo. Ghafla likatokea gari dogo jeupe, akaingia kisha likaondoka. “Tulichanganyikiwa kwa kweli, lakini kuna baadhi ya ndugu walitutoa hofu kwa kutuambia kwamba tuvute subira huenda angerudi baadaye kwa vile waliamini anajua kuwa siku ile ilikuwa ya Send Off yake.”
NDUGU WAANGUA VILIO “Huwezi amini, baadhi ya ndugu waliangua vilio baada ya kusikia bi harusi alipoondoka na gari hakurudi na simu yake haipatikani. Walifika hatua ya kuamini
kuwa, huenda alikwenda kuuawa.
” SAFARI YA POLISI “Kuna baadhi ya majirani nao wakatoa ushauri wa kwenda polisi, lakini wakati tunatafakari hilo, tukaona bora tuwataarifu na upande wa bwana harusi ili nao wakae wakijua.
MUME APATA TAARIFA HIZI! “Wakati tunawataarifu upande wa bwana harusi, ndiyo tukaambiwa mambo ya kushtusha kwamba, muoaji alishapata taarifa kuwa, kuna mwanaume mmoja maarufu mjini Morogoro na ni dalali wa magari, amehusika na kumteka bi harusi huyo, hivyo anakwenda polisi kufungua mashitaka na kumsaka,” kilifunguka chanzo hicho.
 SEND OFF YADODA Mtoa ubuyu huyo alizidi kutiririka kuwa, sherehe ya Send Off ilidoda kama siyo kudorora kufuatia waalikwa kufika ukumbini lakini kushindwa kuendelea na shamrashamra baada ya kupata ‘za ndani’ kuwa, bi harusi hajulikani alipo licha ya meza yake kupambwa na kupambika!!! “Send Off ilikuwa ifanyike katika Ukumbi wa Midland II uliopo maeneo ya Msamvu lakini viti vingi vilikuwa vyeupe maana watu walishakata tamaa. Baadhi walikula na kunywa na ilipofika saa nne usiku, walitawanyika kila mmoja kwake huku gumzo kuu njiani ni bi harusi huyo,” kilisema chanzo hicho.
MUME AKOMAA Wakati gazeti hili linakwenda mitamboni, ilielezwa kuwa aliyekuwa mume mtarajiwa wa Asha, alifanikiwa kumkamata mchepuko huyo wa zamani ambaye anadaiwa kuhusika na tukio hilo na kumfikisha Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro. “Inadaiwa kuwa, wale jamaa walipomchukua Asha walikwenda naye Dar es Salaam. Lakini waliposikia wanatafutwa kwa udi na uvumba, wakiwa hai au wamekufa,  wakamwachia huru bi harusi, akarudi Morogoro kwa usafiri wa basi. “Lakini polisi walifanikiwa kumuweka ndani mchepuko huyo kulekule Dar na kumrudisha Moro kwa uchunguzi zaidi wa tukio,” kilisema chanzo.
 RISASI LATINGA NYUMBANI Mwanahabari wetu alifika nyumbani kwa wazazi wa binti huyo, Kichangani ili kutaka kujua tukio kwa undani zaidi lakini ndugu hao waligoma kutoa ushirikiano kwa kudai hawataki jambo hilo liripotiwe katika vyombo vya habari

No comments