Header Ads

HADITHI: Moyo Ulioumizwa - 01


Mtunzi: Nyemo Chilongani.
“Where are you at?” (upo wapi?)
“I’m on my way home!” (nipo njiani narudi nyumbani)
“Did you see a CNN’s Breaking News?” (umeona Habari Iliyotokea sasa hivi kwenye televisheni ya CNN?)
“No! What is it about?” (hapana! Inahusu nini?)
“Just visit CNN website and see what it is,” (ingia katika tovuti ya CNN uangalie ni kitu gani)
Yalikuwa ni maongezi kati ya msichana aliyekuwa ametulia sebuleni akiangalia televisheni na mwingine ambaye alikuwa njiani akielekea nyumbani kwake. Taarifa kubwa ya habari iliyoingia katika kipindi hicho ilionekana katika televisheni ilimshtua mno.
Msichana huyo hakuamini alichokuwa akikiangalia, akainuka kutoka katika kochi alilokaa na kuisogelea vizuri televisheni na kuangalia kwa karibu kwa kuhisi kama kule alipokaa aliona vibaya kile kilichokuwa kimeandikwa kwa maandishi makubwa kabisa.
‘MELISA HAS GOT MARRIED TO A DOG’ (Melisa ameolewa na mbwa) yalikuwa maneno yaliyosomeka vizuri katika televisheni ile. Msichana yule hakuamini, aliikodolea televisheni ile na kuyasoma vizuri maandishi yale, hayakuwa yamebadilika, vile alivyokuwa ameyasoma alipokuwa mbali ndivyo yalivyokuwa hata pale aliposogea karibu na kuyaangalia.
Alihisi mapigo yake ya moyo yakidunda kwa nguvu kubwa, alimfahamu Melisa, alikuwa miongoni mwa mabilionea wakubwa kipindi hicho. Maisha yake ya nyuma hakukuwa na mtu aliyeyafahamu, walishtukia akiinuka na kuwa tajiri mkubwa.
Melisa Andrew Kimbonaga alikuwa msichana mwenye asili ya Kitanzania, aliishi kwa kipindi fulani nchini Tanzania ndani ya Jiji la Dar es Salaam na baba yake mpaka pale alipoamua kuondoka na kwenda kuishi kwa mama yake, Mzungu aliyekuwa akiishi nchini Marekani, Kattie Williamson.
Aliheshimika kila kona nchini Marekani, alikuwa mwanamke mrembo mno, kila alipokuwa katika mikutano ya mabilionea wakubwa duniani, naye alikuwepo na wanaume wote walikuwa wakimwangalia kwa macho ya matamanio, walimpenda na kumtamani na kila mmoja alitamani kuwa naye.
Wasichana wengi wakatamani kuwa kama yeye, wapo waliojiita jina lake katika mitandao ya kijamii, picha zake zilitawala katika simu za wasichana wengi, kila kitu alichokifanya, wasichana wengi nao wakaiga kufanya kama yeye.
Kwa kifupi alipendwa, alikuwa na biashara nyingi za kuuza vitu vya wanawake, alijua kucheza na soko, alijikuta akiingiza kiasi kikubwa cha fedha na kumfanya kuwa tajiri mkubwa tu, tena aliyetikisa nchini Marekani.
Japokuwa alikuwa na fedha, alikula alichotaka huku akienda popote alipotaka lakini moyo wa Melisa haukuwa na amani, kila alipokaa, alionekana mnyonge, alicheka usoni, alitoa tabasamu lake zuri lakini moyo wake uliwaka kwa maumivu makali.
Wengi wakagundua hilo, walitamani kumuuliza lakini hakukuwa na mtu aliyefanikiwa kufanya hivyo kutokana na ubize mkubwa aliokuwa nao. Stori za huzuni yake ndiyo ilikuwa gumzo katika mitandao ya kijamii na hata kwenye magazeti, watu walitaka kufahamu, kipi kilimpa huzuni? Na nini kilikuwa kikiendelea katika maisha yake?
Hiyo ndiyo ilikuwa hali yake kila siku, hakuonekana kuwa na furaha kabisa, wakati watu walipokuwa wakitamani kuwa mabilionea kama yeye ili wawe na furaha lakini yeye mwenyewe, mwenye pesa zake hakuwa na furaha kabisa.
Hapo ndipo watu walipogundua kwamba unaweza ukawa na fedha nyingi lakini usiwe na uwezo wa kununua kila kitu. Kama mtu alikuwa na fedha, alifanya chochote alichotaka, sasa kwa nini asiwe na furaha?
“Kuna kitu!” alisema jamaa mmoja huku akiwa ameshika picha ya Melisa.
“Kitu gani?”
“Hebu iangalie vizuri hii picha, unaionaje?’ aliuliza jamaa mmoja huku akimuonyeshea mwenzake picha ile.
“Kawaida.”
“Hebu angalia uso wa Melisa. Upo sawa?”
“Mmh! Nimegundua kitu! Mbona yupo hivi?” aliuliza jamaa huyo.
“Ndiyo kitu ninachotaka kukwambia. Huyu msichana inaonekana hana furaha kabisa, kuna kitu kinaendelea, inaonekana moyo wake unaungua kwa ndani,” alisema jamaa huyo huku akiiangalia picha ya Melisa vizuri.
Hilo ndilo lililokuwa likiendelea moyoni mwake, hakuwa na amani, hakuwa na furaha, moyo wake ulijaza maumivu na chuki kali. Kila mmoja alitamani kujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea moyoni mwa msichana huyo mrembo, labda wale ambao wangekuwa na nguvu ya kumsaidia wangemsaidia lakini yeye mwenyewe hakutaka kuweka wazi.
Baada ya miaka kadhaa kupita ndipo watu wakaona taarifa hiyo kwenye televisheni kwamba msichana huyo mrembo, bilionea aliamua kufunga ndoa na mbwa wake. Kila mmoja alishtuka, hawakuamini kama kweli Melisa angeweza kufanya kitu kama hicho.
Maswali kibao yakawajia vichwani mwao, ilikuwaje msichana huyo aamue kuchukua uamuzi huo? Yaani kuolewa na mbwa na wakati kulikuwa na wanaume wengi! tena wenye uchu na usongo wa kuwa na msichana mrembo kama yeye!
Hilo likawakera watu wengi, wengine wakahisi kwamba inawezekana alikuwa akitafuta kiki, asikike zaidi lakini huo haukuwa ukweli, ukweli wenyewe ni kwamba hakuwa na furaha kabisa moyoni mwake.
“Ni bora niolewe na mbwa,” alisema Melisa alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari kutoka BBC.
“Lakini kwa nini umeamua hivyo?”
“Kwa sababu nampenda mbwa wangu, amekuwa karibu yangu, sidhani kama natakiwa kuolewa na mwanaume yeyote, huyu mbwa ananifaa,” alijibu Melisa huku mbwa akiwa pembeni yake.
“Lakini unaonaje kam...”
“Nadhani maswali yametosha mwandishi, naomba utuache tukapumzike,” alisema Melisa, aliamua kumkatisha mwandishi asiulize maswali zaidi.
“Lakini nim...”
Melisa hakutaka kubaki kitini, hapohapo akasimama na kuanza kuondoka huku akimchukua mbwa wake aliyempa jina la Bobby. Mwandishi yule alibaki akimwangalia Melisa, hakuamini kama kweli kile kilichokuwa kikitokea, kilimtokea msichana huyo.
Aliwaona wanawake wengi wakifanya mapenzi na mbwa, hao walikuwa kwenye filamu za kikubwa, walifanya hivyo kwa kuwa walihitaji fedha, sasa ilikuwaje kwa Melisa aamue kufanya kitu kama hicho? Kama ni fedha, alikuwa nazo, sasa kwa nini aolewe na mbwa?
Hilo lilikuwa swali lisilokuwa na majibu.
Je, nini kitaendelea?
Je, ni kitu gani kilichojificha nyuma ya msichana Melisa?
Tukutane wiki ijayo mahali hapa.
Unaweza kushare kwa ajili ya marafiki zako!

No comments