Header Ads

HADITHI: Moyo Ulioumizwa - 03


MTUNZI: Nyemo Chilongani

Ilipotoka
Msichana mwenye pesa, bilionea mkubwa duniani, Melisa Andrew anaamua kufunga ndoa na mbwa. Kila mtu anashtuka, hakuna aliyeamini kile alichokifanya msichana huyo kwani kulikuwa na wanaume wengi waliokuwa wakimtaka, ila wote hao, hakuona kama walistahili kumuoa zaidi ya mbwa wake aliyeitwa Bobby.
Jambo hilo linazua minong'ono mingi, watu wanahisi kwamba nyuma ya pazia kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea hivyo waandishi kuamua kumtafuta Melisa kwa ajili ya kujua kilichotokea.
Wanapompata, anakataa kuhadithia nini kilitokea mpaka kufanya hivyo. Waandishi hao hawakuchoka, waliamini kwamba kuna mtu anajua sababu hivyo wanaamua kumfuata Catherine, msichana aliyewahi kusoma naye chuoni Havard, msichana huyo alikuwa nchini Ujerumani.
Wanafunga safari kutoka Marekani na kwenda huko, wanamkuta ila mbaya zaidi msichana huyo anakataa kuwasimulia. Wanakata tamaa, ila wanachokifanya ni kuelekea Tanzania ambapo huko wanakwenda Kilimanjaro na kukutana na msichana Manka ambaye alikua na Melisa utotoni. Kuna vitu anavijua msichana huyo na kuahidi kuwasimulia kilichotokea.
Unajua ni nini?
Je, msichana huyo aliwasimulia?
Ungana na mtunzi chipukizi, Nyemo Chilongani.

SONGA NAYO
Melisa alikuwa nyumbani kwake, pembeni alikuwepo mbwa wake, Bobby, alikuwa akimpenda kuliko kitu chochote kile, alikuwa ametulia huku mawazo yake yakifikiria mbali kabisa.
Alijua fika kwamba ulimwengu ulimshangaa kwa sababu tu aliamua kufunga ndoa na mbwa lakini hakukuwa na mtu aliyejua sababu iliyompelekea kuchukua uamuzi kama ule. Hakutaka dunia ijue kilichokuwa kimetokea, alijua fika kwamba historia ambayo ilikuwa nyuma ya maisha yake ilimuumiza mno.
Alitaka iwe siri kwa sababu hakuwa Melisa yule wa kipindi cha nyuma, huyu alikuwa mpya hivyo hata maumivu ambayo aliwahi kupitia nyuma yake alitaka yabaki na kuwa stori ambayo kamwe isingeweza kujirudia.
Hakutaka mtu yeyote afahamu kilichokuwa kimetokea, alijua kwamba kila mtu alikuwa na hamu ya kuufahamu ukweli ila hilo hakutaka kuliweka wazi kabisa. Alichokifanya ni kuwapigia simu marafiki zake na kuwaambia kwamba hawakutakiwa kuwaambia waandishi juu ya kile kilichokuwa kimetokea kipindi cha nyuma katika maisha yake, kwani marafiki haohao, aliamua kuwaahadithia hata kabla maisha yake hayajabadilika na kuwa bilionea.
Alimkumbuka Catherine, rafiki yake ambaye katika kipindi hicho alikuwa mwanamitindo nchini Ujerumani. Alijua fika kabisa kwamba ilikuwa ni lazima waandishi waanze na huyo, hivyo alichokifanya ni kumwambia kwamba asiwaambie waandishi chochote kile ambacho wangemuuliza kuhusu yeye.
Hilo likafanikiwa, mtu wa pili ambaye alikuja kichwani mwake alikuwa rafiki yake mwingine ambaye kipindi hicho alikuwa nchini Tanzania, rafiki huyo aliitwa Manka. Aliwajua waandishi wa mashirika makubwa ya habari, walipokuwa wakiamua kutafuta habari, walijitoa, walikuwa tayari kufanya kila kitu kinachowezekana ili wapate ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea, wapate fedha kwa kuuza habari hiyo, tena ikiwa na mwendelezo kama kitabu cha hadithi.
Hilo lilimnyima raha hivyo alichokifanya ni kumpigia simu rafiki yake huyo. Hakujali kama ilikuwa ni usiku wa manane, akaamka, akaifuata simu yake na kisha kutafuta jina la Manka, alipolipata, hapohapo akampigia simu.
Upande wa pili wakati Manka akiwa amejiandaa tayari kwa kuwasimulia waandishi wa habari kile kilichokuwa kimetokea katika maisha ya rafiki yake, mara simu yake ikaanza kuita, alipoliangalia jina, alikuwa Melisa, moyo wake ukapiga paaa!
“Manka!” aliita Melisa.
“Niambie!”
“Naomba unisaidie kitu kimoja rafiki yangu!”
“Kitu gani?”
“Upo wapi?”
“Nipo Kilimanjaro!”
“Sawa! Nashukuru! Nataka nikutumie bilioni moja,” alisikika Manka.
“Za nini?”
“Nataka umtafute David popote pale alipo na umpe kiasi hicho cha fedha! Mwambie anisamehe! Nilifanya kila kitu nilichofanya kwa sababu sikuwa na jinsi,” alisema Melisa, kwa mbali alisikika kama mtu aliyekuwa akikaribia kulia.
“Melisa!”
“Naomba unisaidie Manka! Nakuomba mpenzi!”
“Sawa ila.....” alisema Manka, hapohapo akanyamaza.
“Ila nini? Nini kinaendelea Manka! Naomba uniambie, nini kinaendelea huko?” aliuliza Melisa huku akianza kulia.
“Kuhusu David...”
“Amefanyaje? Amekufa?” aliuliza Manka mara nyinginyingi kama mtu asiyeamini kile alichotakiwa kuambiwa mahali hapo.
Manka alikuwa kimya, alionekana kama mtu aliyekuwa akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kukiongea mahali hapo. Alimjua rafiki yake, alikuwa mtu wa kulia, hata alipokuwa akifanyiwa kitu kibaya au mtu aliyekuwa akimpenda kuwa kwenye hali mbaya, alikuwa akilia tu.
Hakujua kama alitakiwa kumwambia kile alichotaka kumwambia wakati huo. Akashusha pumzi nzito, baada ya hapo, akaona ilikuwa bora kumwambia ili afahamu kila kitu kilichotokea nchini Tanzania kuliko kumficha kama alivyotaka kufanya.
“David alikufa...” alisema Manka.
“Unasemaje?”
“Pole sana Melisa. David alikufa miezi sita iliyopita, sikutaka kukwambia kwa sababu sikujua kama ulikuwa ukimpenda na hivyo kupewa taarifa zake,” alisema Manka kwa sauti ya chini, yeye mwenyewe machozi yakaanza kumtoka.
“Manka! Manka! Haiwezekani! Haiwezekani,” alisema Melisa, hapohapo akakata simu.
Moyo wake ulimchoma, hakuamini kile alichoambiwa kwamba mwanaume aliyejulikana kwa jina la David alikuwa amekufa. Machozi yalilowanisha mashavu yake, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake mpaka ndani kabisa.
Akaanza kuzungukazunguka kitandani pale huku akiongea peke yake kama mtu aliyechanganyikiwa. Kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kabisa, kipindi ambacho alikuwa na mwanaume huyo mpaka alipoamua kuachana naye, moyo wake ulimuuma sana.
“Haiwezekani! David hawezi kufa!” alisema Melisa.
Hapohapo akalifuata kabati la vitabu, akapekuapekua harakaharaka na kutoa kitabu kimoja kilichoandikwa Melisa Andrew ‘The New Era Billionaire’ (Melisa Andrew ‘Bilionea wa Kizazi Kipya)
Hicho kilikuwa kitabu alichokiandika yeye mwenyewe, kilikuwa na kurasa zaidi ya elfu moja na kilihusu maisha yake. Kila kitu kilichotokea kipindi cha nyuma, alikiandika ndani ya kitabu hicho.
Hakuwa amekitoa, kilikuwa kopi moja tu ambayo alikaa nayo chumbani kwake. Mara kwa mara alikuwa akikipitia kitabu hicho cha maisha yake, hakutaka mtu yeyote akisome na ndiyo maana alikuwa amekificha ka ndani sana.
Alikichukua na kuanza kufunua kila ukurasa, machozi yalikuwa yakimbubujika kwani kila alipoziangalia kurasa za kitabu hicho ndivyo ambavyo maisha yake ya nyuma yalivyoanza kujirudia kichwani mwake kama mkanda wa filamu.
“Ni lazima niende Tanzania, ni lazima nikalione kaburi la David,” alisema Melisa.
Usiku huohuo akampigia simu rubani wake na kumwambia kwamba usiku huohuo walitakiwa kuondoka kuelekea nchini Tanzania. Ilikuwa ni safari ya ghafla sana lakini kile alichokitaka ni kwenda kwenye kaburi la David na kuliangalia, alijua kilichotokea, alijua ni jinsi gani alimuumiza kijana huyo, hivyo alitaka kuomba msamaha, hata kama yeye mwenyewe hakuwepo, alitaka kuomba hata mbele ya kaburi la mwanaume huyo.
Usiku huohuo safari ya kuelekea Tanzania ikaanza huku akiwa na mbwa wake. Alikuwa ndani ya ndege yake na wafanyakazi watatu na marubani wawili. Kila mmoja alimwangalia Melisa, alionekana kuwa tofauti sana, hakuwa Melisa yule waliyemzoea, yule aliyekuwa akicheka nao kila siku, siku hiyo alionekana tofauti kabisa kama mtu aliyekuwa amefiwa.
“Boss! Are you okey,” (bosi! Upo sawa?) aliuliza mfanyakazi wake huku akimwangalia.
“Yeah!” alijibu Melisa huku akimchezea mbwa wake aliyekuwa akijaribu kulala.
“But you look weird today, what is going on?” (lakini unaonekana kutokuwa kawaida, nini kinaendelea?) aliendelea kuuliza msichana huyo.
Melisa hakujibu kitu, alitulia, akachukua kitabu alichokuwa nacho na kuendelea kufunua baadhi ya kurasa. Aliendelea kulia, machozi yalimtiririka mashavuni mwake, kila kilichokuwa kimetokea kilimuumiza kweli, alimfikiria David, mwanaume ambaye alijua fika kwamba alimkosea, na alitaka kuonana naye na kumuomba msamaha.
Ndege ilichukua saa thelathini ndipo ikatua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Akateremka huku mmoja wa wafanyakazi wake akichukua begi lake, wakatoka nje ambapo wakapanda katika Gari la Hoteli ya Johannesburg na kuanza kuelekea katika hoteli hiyo.
Baada ya dakika kadhaa wakafika katika hoteli hiyo na kutulia. Usiku wa siku hiyo Melisa alibaki akikiangalia kitabu kile huku akisoma baadhi ya sehemu ambazo zilimuumiza mno na kumfanya kulia usiku kucha.
“David...naomba unisamehe! Nisamehe david...” alisema Melisa huku akijifuta machozi.

Je, nini kitaendelea?

No comments