Header Ads

HADITHI: Moyo Ulioumizwa - 04


MTUNZI: Nyemo Chilongani

Waandishi wa habari, Claire na Brian waliamini kwamba Manka angeweza kuwasimulia kile kilichokuwa kimetokea, waliandaa vitabu vyao tayari kwa kuandika kila kitu lakini mambo yalibadilika baada ya Manka kumaliza kuzungumza na Melisa kwenye simu aliyopigiwa.
Machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake, alipoulizwa kuhusu David, yeye mwenyewe alijikuta akichomwa na kitu chenye ncha kali moyoni mwake kwani hakuamini kama Melisa yuleyule leo hii angemuulizia mwanaume huyo ambaye alimpenda sana kipindi cha nyuma.
“Tunaweza kuanza?” aliuliza Claire.
“Hapana! Haiwezekani!” alijibu Manka huku akijifuta machozi.
“Kwa nini tena?”
“Basi tu! Haiwezekani! Melisa mwenyewe anakuja!” alijibu Manka.
“Manka! Naomba utusaidie, tumehangaika kwa ajili ya hili, tunaomba utuambie chochote kile,” alisema Claire huku hata uso wake ukionyesha ni jinsi gani alikuwa akimuomba Manka awaambie kile kilichokuwa kimetokea.
Manka alibadilika, hakutaka kuwahadithia kitu chochote kile zaidi ya kuwaambia kwamba melisa alikuwa njiani akija nchini Tanzania hivyo walitakiwa kumsubiria msichana huyo.
“Kwa hiyo anakuja? Ila sidhani kama atakubali! Sijui, kama alitukatalia Marekani, kweli anaweza kutukubalia huku?” aliuliza Brian huku akionekana kukata tamaa.
Siku hiyo hawakutaka kuondoka mahali hapo, walilala hapohapo huku wakimsubiri Melisa ambaye alifika nyumbani siku iliyofuata huku akifuatwa na watoto wengi waliokuwa wakiimba jina lake.
“Anakuja...” alisema Manka wakati wazee ndiyo walikuwa wameamka, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuchukua vikombe vikubwa na kuanza kunywa pombe za kienyeji.
Melisa alipowaona watu hao, alishangaa sana, hakutegemea kuwakuta mahali hapo. Walionekana kuwa na kiu ya kufahamu ni kitu gani kilitokea katika maisha ya msichana huyo. Akawasogelea na kuwasalimia.
Kama kawaida ujio wa Melisa kijijini hapo ulikuwa gumzo, kila mtu alifika mahali hapo kwa ajili ya kumuona. Walimfahamu kama bilionea mkubwa duniani lakini kitu kilichowafurahisha, kila alipokuwa akienda kwao, hakuonekana kama bilionea, alikuwa mtu wa kawaida sana.
Watu kutoka sehemu nyingine waliposikia Melisa amefika Marangu, nao wakaenda kwa ajili ya kumuona kwani walikuwa wakimuona kwenye magazeti na televisheni tu. Kwa msichana huyo ilionekana kuwa faraja sana, alijisikia furaha kwa kuwa aliona ni jinsi gani alikuwa akipendwa sana kipindi hicho.
Brian na Claire hawakutaka kumuacha, kila wakati walikuwa karibu naye kwani waliamini kwamba kwa kipindi hicho msichana huyo angeweza kuwahadithia kila kitu kilichokuwa kipindi cha nyuma katika maisha yake.
Walikaa Marangu wiki nzima huku kila siku wakimsumbua Melisa kwamba huo ndiyo ulikuwa wakati wenyewe wa kuwahadithia kila kitu kilichotokea katika maisha yake ya nyuma.
“Haiwezekani!” alisema Melisa.
“Kwa nini jamani?”
“Basi tu! Nimeamua!”
Ni kweli alimaanisha lakini hiyo haikuwa mwisho wa kumwambia lengo halisi la wao kumtafuta kwa kipindi chote hicho, waliamini kwamba kupitia maisha yake, kuna wengi wangejifunza na kupata mwanga fulani mbele ya maisha yao.
“Ila kuna mabaya pia...” aliwaambia.
“Na watu wanajifunza hata kwenye mabaya, tena ndiyo huwa wengi,” alijibu Brian huku akimwangalia msichana huyo machoni.
Aliamua kuwakatalia lakini baada ya kulazimishwa sana, hatimaye akawakubalia. Alichokifanya ni kuwachukua na kisha kuanza kuzunguka nao hapo Marangu, kulikuwa na sehemu alizotaka kuwaonyeshea, sehemu ambazo zilihusika katika historia ya maisha yake ya nyuma.
“Nilikuwa na mpenzi wangu, huyu aliitwa David,” aliwaambia huku akiwaangalia.
“Yupo wapi?” aliuliza Brian, Melisa hakulijibu swali hilo, akanyamaza na kuendelea:
“Nilimpenda sana, sidhani kama angetokea mwanaume katika maisha yangu ambaye ningempenda kama nilivyompenda David,” alisema, machozi yakaanza kujikusanya machoni mwake na kuanza kumtiririka mashavuni mwake.
Wakati wakiyazungumza hayo, tayari walifika katika shamba la migomba ambapo kulikuwa na tope jingi kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha mara kwa mara kipindi hicho. Wakatembea huko, walipofika sehemu fulani, wakasimama.
“Mnapaona hapa?” aliwauliza.
“Ndiyo!”
“Hii ni sehemu ambayo mara kwa mara nilikuwa nakutania na David. Hatukuwa na sehemu nyingine ya siri ya kukaa na kuzungumza, nitawahadithia kuhusu sehemu hii pia,” alisema Melisa huku akiiangalia sehemu hiyo kwa umakini.
“Ilikuwaje? Mlikuwa mkikaa chini au kusimama?”
“Tulikuwa tunafanya vyote, kwenye kipindi cha mvua tulikuwa tunasimama lakini kipindi cha kiangazi tulikuwa tunakaa. Hii ndiyo ilikuwa sehemu ya kwanza kubusiwa mdomoni, ndiyo ilikuwa sehemu ya kwanza mdomo wangu kubadilishana mate na mwanaume,” alisema Melisa.
Alichokifanya Claire ni kuipiga picha sehemu ile, baada ya hapo wakaondoka na kuelekea sehemu moja iliyokuwa na mti mkubwa wa mnazi. Melisa akawaambia wausogelee, wakausogelea na kuwaonyesha kitu fulani katika mti wa mnazi ule, kulikuwa na maneno yaliyosomeka D And M Forever yakiwa na maana ya D Na M Milele.
“Hii ilimaanisha nini?” aliuliza Brian.
“Ni sehemu ambayo niliweka ahadi na David kwamba tusingeachana miaka yote. Tukaandika herufi za kwanza za majina yetu kuonyesha kwamba tungeishi milele,” alisema Melisa.
Asubuhi hiyo ilikuwa ni asubuhi ya kuwaonyesha baadhi ya sehemu ambazo walitakiwa kuziona hata kabla ya kuanza kuwasimulia ni kitu gani kilitokea katika maisha yake ya nyuma.
Walizunguka sehemu mbalimbali na baadaye kurudi nyumbani. Kabla ya kuwaambia kitu chochote kile, akawapa kitabu kile na kuwataka kukisoma japo kwa dakika chache kabla ya kuanza kuhadithia kwa undani juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea.
“Kumbe una kitabu!”
“Ndiyo! Nilikiandika na kuwa siri yangu peke yangu, kitabu hiki kina historia nzima ya maisha yangu!” alisema Melisa.
Claire na Brian wakaanza kukipitia kitabu kile kwa dakika kadhaa, baada ya hapo Melisa akakichukua na kisha kutulia kwenye kiti, alibaki akiwaangalia watu hao huku machozi yakianza kumtoka kama kawaida.
Alionekana kuwa mtu mwenye maumivu makali moyoni mwake, kila alipokumbuka kule alipopitia, moyo wake ulimuuma mno.
“David...David mpenzi naomba unisamehe!” alijikuta akisema Melisa, baada ya kusema hivyo tu, hapohapo akayafuta machozi yake na kuanza kuhadithia kilichotokea, hakutaka kuficha tena, kila kitu alitaka kukiweka wazi huku waandishi hao wakianza kazi yao ya kurekodi na kuandika kila kitu watakachoambiwa.

Je, nini kitaendelea?
Nini kilitokea katika maisha ya msichana Melisa?
Huyu David ni nani?

No comments