Header Ads

HADITHI: Moyo Ulioumizwa - 05


MTUNZI: Nyemo Chilongani
Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha, matope yalitapakaa kila kona huku kila mtu aliyekuwa Marangu akiwa amejifungia ndani kwake. Hakukuwa na mtu aliyetoka, na hata wale waliokuwa na ulazima wa kutoka ndani ya nyumba zao, walivalia makoti makubwa kwani kwani hicho kilikuwa kipindi cha mvua kubwa ambacho wenyeji wengi wa Kilimanjaro hawakuwa wakikipenda.
Baridi liliwakung’uta, kila mtu alijikunyata, waliokuwa ndani, vitandani mwao, walivuta mablangeti na kujikunyata zaidi kwani kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo baridi lilivyozidi kuongezeka.
Wakati kila mtu akiogopa kutoka ndani ya nyumba yake, kijana masikini, mwenye sura nzuri, David alikuwa kwenye shamba la migomba. Mvua ilinyesha, alilowa mwili mzima, aliikutanisha mikono yake kwa staili ya kujikunyata lakini hakutaka kuondoka pale alipokuwa.
Hakuwa mahali hapo kwa bahati mbaya, si kwamba mvua ilimkuta ghafla bali alikuwa mahali hapo kwa sababu ya msichana aliyekuwa akimpenda, msichana aliyekuwa akimuwaza usiku mzima, msichana ambaye kila siku alimwambia wazi kwamba alikuwa akimpenda, msichana huyu aliitwa Melisa Andrew.
Moyo wake ulikuwa kwa msichana huyo, kutokana na sura nzuri aliyokuwa nayo, wasichana wengi walimpenda, kila mmoja alitaka kuwa naye, walimtongoza kila siku lakini David hakutaka kuwa nao, hakutaka kabisa kuwa na msichana yeyote yule zaidi ya Melisa aliyemuona kuwa mwanamke wake wa ndoto.
Alikaa shambani hapo kwa dakika zaidi ya arobaini huku mvua ikimnyeshea, Melisa hakutokea, hiyo haikuwa mara ya kwanza, ilikuwa ni zaidi ya mara kumi, kila siku alikuwa akizungumza na msichana huyo na kumwambia amsubiri huko kwenye migomba, alikuwa akienda, tena kwa kuwahi sana lakini mara zote hizo msichana huyo hakutokea.
Hakuchoka, kila siku alivumilia, alipoambiwa asubiri, alisubiri, kama aliambiwa wakutane saa kumi shambani hapo, yeye saa nane alikuwa hapo akimsubiri Melisa, kitu kilichomuumiza ni kwamba msichana huyo hakuwa akitokea.
Alitetemeka, meno yaligonganagonga kutokana na baridi lakini hakutaka kuondoka, bado moyo wake ulimwambia kwamba Melisa angefika hapo shambani lakini dakika zilizidi kusonga mbele na msichana huyo hakutokea.
“Nini kimempata?” alijiuliza, hakuangalia kama kulikuwa na mvua, kwa sababu alimpenda sana msichana huyo, alihisi kwamba naye alitakiwa kupendwa namna hiyo, aliona Melisa hakutakiwa kuangalia hali ya hewa, alitakiwa kufika mahali hapo hata kama kulikuwa na mvua kubwa.
Mvua ilikatika baada ya dakika thelathini. Tope lilitapakaa kila kona, alisubiri kwa saa mbili baada ya muda husika lakini msichana huyo hakutokea hivyo kurudi nyumbani kwao, vilevile kama siku nyingine, huzuni ilimshika moyoni lakini hakusema kwamba siku nyingine asingekuja, ni lazima angekuja kwa sababu alimhitaji msichana huyo.
“Melisa, utautesa moyo wangu mpaka lini? Kweli hunielewi kabisa pamoja na kujitoa sana kwa ajili yako? Ninakupenda, naomba uwe wangu, ninajitahidi kukuonyeshea kila kitu, jinsi ninavyokupenda lakini naona hunielewi, kwa nini? Au kwa sababu wewe ni mzuri sana? Au kwa sababu mimi ni masikini, labda kwa sababu mama yangu siyo Mzungu kama mama yako? Melisa, kwa nini unaifanyia hivi?” alijiuliza David huku akijilaza kitandani kwake.
Huyo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Marangu. Shuleni hapo alikuwa akisoma na msichana Melisa, tena darasa moja kiasi kwamba ilikuwa rahisi kumfuatilia kila siku.
Alijaribu kumwambia Melisa jinsi alivyokuwa akimpenda lakini msichana huyo hakutaka kuelewa, kila siku ilikuwa ni visingizio tu. Wavulana wengi waliendelea kumfutualia, hivyo hata David alivyomfuata na kumwambia kwamba alikuwa akimpenda, alimchukulia kama wavulana wengine.
Usiku wa siku hiyo ulikuwa ni wa mateso makubwa kwa David, kila wakati alikuwa akimfikiria Melisa, uzuri wake ulimdatisha kila mwanaume aliyemwangalia. Alikuwa na mawazo mengi juu ya msichana huyo kiasi kwamba kuna kipindi aliona kama angechanganyikiwa kwani kama kupenda, alipenda kwa kiwango cha juu kabisa.
Siku iliyofuata, akajiandaa na kwenda shuleni kama kawaida. Alipofika huko, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtafuta Melisa, alitaka kuonana naye na kuzungumza naye kwa ukaribu, kumwambia namna alivyomsubiri siku iliyopita, mvua ilivyompiga kwa ajili yake tu.
Alimuona msichana huyo akiwa katika kundi na wasichana wengine. Alimwangalia, siku hiyo Melisa alionekana tofauti machoni mwake, uzuri aliokuwa nao uliongezeka maradufu. Akabaki amesimama huku akijifikiria kama ilikuwa sahihi kumfuata na kuzungumza naye mahali pale au angemfuata akiwa darasani.
“Ngoja nimfuate!” alisema David, hakutaka kubaki mahali hapo, akaanza kupiga hatua kumfuata Melisa.
“Naweza kuzungumza nawe?” aliuliza David huku akimwangalia msichana huyo, wasichana wote wakanyamaza na kumwangalia David, kisha macho yao wakayageuzia kwa Melisa.
“Zungumza hapahapa!” alijibu msichana huyo huku akitoa tabasamu pana lililomchanganya mno David.
“Nakuomba Melisa, tusogee pembeni kidogo!”
“Hujiamini?” aliingilia msichana mwingine, huyo aliitwa Manka.
“Najiamini!”
“Basi zungumza!” alisema Melisa.
David hakuzungumza kitu chochote kile, alibaki kimya huku wasichana wote wakimwangalia. Hakutaka kuzungumza chochote mahali hapo, ujumbe mkubwa uliobeba moyo wake alitakiwa kuambiwa Melisa tu, tena kisiri na hakutakiwa msichana yeyote ajue kilichokuwa kikiendelea.
Wasichana wote walikuwa wakimwangalia David, walitaka kumsikia alichotaka kumwambia Melisa. Mvulana huyo akajiumauma na kupiga moyo konde kwani kama msichana huyo hakutaka kwenda pembeni, basi ilikuwa ni lazima kumwambia hapohapo.
“Ninakupenda Melisa,” alisema David huku akimwangalia msichana huyo.
Wasichana wote wakaanza kucheka chinichini, si wao tu, hata Melisa mwenyewe akaanza kucheka, alimwangalia David, macho yake tu yalionyesha kila kitu kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.
Huyo hakuwa mvulana wa kwanza kumwambia hivyo, maneno yale yalizoeleka masikioni mwake kama wimbo wa taifa. Wala hakushtuka, alichokifanya ni kupiga hatua kumsogelea David.
“Unanipenda mimi?” aliuliza msichana huyo huku akitoa tabasamu pana.
“Ndiyo!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Kwa nini mimi?”
“Melisa...”
“Si nimekuuliza! Kwa nini siyo Manka? Kwa nini siyo Neema? Kwa nini siyo Upendo? Kwa nini mimi?” aliuliza Melisa huku akionekana kujiamini.
“Kwa sababu...Melisa, nakupenda....” alisema David huku akibabaika.
Melisa alijiamini kwa kila kitu, alifundishwa jinsi ya kuzungumza na mvulana. Baba yake alijua jinsi binti yake alivyokuwa mrembo hivyo akamtengenezea mazingira ya kupambana na wanaume waliokuwa wakimtongoza.
Ililimpa kiburi, hakuwa mtu wa kujishtukia, kila alipokuwa akizungumza na mvulana, alisimama kwa kujiamini, hakuangalia pembeni, alikuwa akimwangalia mvulana machoni na bila kuteteleka alikuwa akizungumza naye.
Wengi walimuogopa Melisa, alionekana kuwa mwerevu hata zaidi ya baadhi ya wavulana waliokuwa wakimfuata na kumtongoza. Alimwangalia David, kwa jinsi alivyokuwa akimkazia macho, wakati mwingine mvulana huyo alikuwa akijishtukia na kuangalia pembeni, hilo tu lilimpa moyo Melisa kwamba aliweza kummudu mvulana huyo.
“Mimi sikupendi!” alisema msichana huyo.
“Unasemaje?”
“Kwani hujasikia! Manka! Hebu nisaidie,” alisema Melisa.
“Amesema hakutaki!” alisema Manka kwa sauti kubwa mpaka wanafunzi wengi wakasikia.
David akanyong’onyea, hakuamini alichokisikia, baridi lililokuwepo likaongezeka mwilini mwake, miguu ikaanza kumtetemeka na cha kushangaza kabisa, kijasho chembamba kikaanza kumtiririka.
Hakuamini, kila siku alikuwa akijitoa kwa ajili ya msichana huyo, alimuonyeshea upendo wa dhati lakini mwisho wa siku msichana huyo akaamua kumwambia ukweli kwamba hakuwa akimpenda, kama alimuweka moyoni, alimaanisha amtoe kwani hakuwa katika mipango yake kabisa.
“Kweli hunipendi?” aliuliza David.
“Ndiyo! Au kwa sababu kila msichana anakupenda basi unahisi na mimi nitakupenda? Wala sikupendi, halafu nashangaa jinsi unavyonifuatilia. Mbona wasichana wapo wengi tu David!” alisema Melisa, wakati akizungumza hayo, uso wake ulitawaliwa na tabasamu pana kitu kilichomfanya Davidi kuhisi kwamba msichana huyo alikuwa akifurahia kile kitu alichokiongea, hakujali ni jinsi gani aliumia moyoni.
Wakati Melisa ameyazungumza hayo, kengele ikagongwa na wote kuanza kwenda darasani. David alibaki akiwa amesimama, alichoambiwa kilimsikitisha sana, kiliuumiza moyo wake kupita kawaida.
Hata kwenda darasani hakutaka kwenda, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea nyumbani. Njiani alikuwa na mawazo tele, alibaki akiongea peke yake kama mtu aliyechanganyikiwa.
Bila kutarajia, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake, hakurudi nyumbani, alichokifanya ni kuunganisha safari yake kwenda kwenye kilima kidogo kilichokuwa mbali kidogo na nyumbani kwao.
Huko, akakaa chini na kuanza kufikiria maisha yake, alimpenda sana Melisa, hakuwa tayari kumpenda msichana mwingine zaidi ya Melisa ambaye ndiye yuleyule aliyesema kwamba hampendi.
“Nitafanya nini sasa? Haiwezekani! Kama hanipendi nitamlazimisha mpaka anipende,” alisema David huku akijiwekea nadhiri kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mwisho wa siku Melisa ampende.
Je, nini kitaendelea?
Je, David alifanikiwa kumpata Melisa?
Je, kwa nini msichana huyo ameamua kufunga ndoa na mbwa?
Tukutane Jumatatu kwa mwendelezo wa hadithi hii!
Pia unaweza kuipata Instagram kwa username nyemochilongani

No comments