Header Ads

Hivi Ndivyo Kupatwa Kwa Jua Kutakavyokuwa ...litanekana Tanzania, Rujewa mkoani Mbeya ambako giza nene litatanda kwa takriban dakika tatu

TAIFA la Tanzania, kesho linatarajiwa kuandika historia ya aina yake baada ya mambo makubwa matatu kujitokeza kwa siku moja huku kivutio kikubwa zaidi ikiwa ni kupatwa kwa jua, tukio ambalo litaonekana kwa ufasaha zaidi katika mji wa Rujewa ulioko mkoani Mbeya ambako giza nene litatanda kwa takriban dakika tatu. 


Kwa mara ya kwanza, Waziri Mkuu wa Tanzania atahamishia rasmi makazi yake mkoani Dodoma ambako pia shughuli zake zote za kiserikali zitafanyika katika mji huo mkuu wa nchi, ikiwa inafanyika baada ya miaka 43 baada ya tamko kutolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Kambarage Nyerere. K u h a m i a Dodoma kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kunafuatia agizo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la kuwataka watendaji wote wa serikali kuu kuwa wamehamia katika mji huo kabla ya kumalizika kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano. 

Mara baada ya kutoa kauli hiyo, siku chache baadaye Majaliwa alisema atakuwa ametangulia katika mji huo ambao ni ngome ya Chama Cha Mapinduzi ifikapo
Septemba Mosi mwaka huu, tukio ambalo linaweka historia kwani tangu uhuru, Dar es Salaam ndiyo ilikuwa makao makuu ya shughuli zote za serikali kuu. Wakati hali ikiwa hivyo mkoani Dodoma, katika mji mdogo wa Rujewa huko Mbeya, dunia itashuhudia kupatwa kwa jua, ambapo mwezi utalifunika kabisa jua kwa takriban dakika tatu na kuufanya mji huo na mingine nchini, kuwa na giza totoro. 


Baadhi ya wanasayansi mahiri duniani, wakiwemo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Anga ya Marekani (NASA) wapo mkoani Mbeya ili kushuhudia tukio hilo, ambalo hata hivyo, baadhi ya maeneo duniani hayataona kinachoendelea. Kutokana na tukio hilo Mkoa wa Mbeya umepata wageni wengi, kitu ambacho k i t a w a v u t i a pia wahalifu, wakiwemo vibaka, ambao huenda wakatumia nafasi ya uwepo wa giza kufanya uhalifu kwa baadhi ya maeneo. Kuhusu suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, DCP Dhahir Athuman Kidavashari, alisema jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha kila kitu kinakuwa shwari na tukio hilo la aina yake linamalizika salama.
 


“Niseme kwamba hili ni jambo jema kwa nchi yetu kwa sababu ni wakati muafaka wa kujitangaza kiutalii, sasa unajua neema yoyote lazima iwe na upande wa pili, tunatambua kuna watu watataka nao kufaidika kupitia kwa wageni na tukio lenyewe, niwape onyo kuwa vijana wetu wamejipanga kuhakikisha hakuna kitakachoharibika,” alisema kamanda huyo. Juu ya tishio la uwepo wa maandamano na mikutano ya chama kikuu cha upinzani maarufu kama Ukuta, kamanda huyo alisema hawezi kuzungumzia kitu ambacho hakipo, ingawa alisisitiza kuwa endapo itatokea, watashughulika nalo kwa mujibu wa sheria. 

Tukio jingine kubwa la kihistoria linalotarajiwa kujitokeza hapo kesho ni kuwepo mitaani kwa Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) watakaofanya usafi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 52 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo kubwa nchini. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na jeshi hilo, badala ya kufanya gwaride na maandamano ya ukakamavu, askari wa vikosi vyote nchi nzima, wataingia mitaani kushiriki zoezi la kufanya usafi, ikiwa ni kuunga mkono harakati za usafi wa mazingira zilizoanzishwa na Rais Magufuli tangu aliposhika madaraka Novemba 5, mwaka jana.

No comments