Header Ads

Inasikitisha! Mama mkwe anapogeuka tatizo kwenye ndoa ya Mwanae!

MPENZI msomaji tuanze kwa kumshukuru Mungu kwa kuiona siku hii nyingine njema yenye kupendeza kwangu na kwako pia. Mada ya leo inawazungumzia baadhi ya wakwe wanaogeuka tatizo kwenye ndoa za watoto wao. Siyo siri, uchunguzi unaonesha kuwa kuna akina mama wakwe wanaoshindwa kuwa wastaarabu au waungwana kwa kutulia nyumbani kwao na kufanya mambo yao na waume zao yaani baba wakwe. Kitendo cha mama mkwe kumfuatilia mwanaye kwa kila kitu, hakipendezi. Na Gabriel NG’OSHA SIMU; +255 657 486745
Mama mkwe lazima ujue kuwa mwanao ameshakuwa mtu mzima na anajitegemea, Mungu amemjalia kupata mume au mke. Sasa mbona unakuwa mchonganishi wa ndoa yao? Hata kama ulikuwa hupendi kijana au binti yako aolewe naye, kwa nini uliruhusu ndoa ifungwe? Si ungeweka kipingamizi? Nasema hivyo kwa sababu ndiyo maana baadhi ya dini na madhehebu hutoa nafasi kwa mtu au watu wenye kipingamizi kupinga uhalali wa ndoa kabla ya kufungwa. 

Kwa nini hukufanya hivyo mapema? Kwa tabia yako ni kama kipingamizi kwenye ndoa ya mtoto wako. Hivi ungekuwa wewe ndiye unatendewa hivyo ungefanyeje au ungechukua hatua gani? Bila shaka usingependa mzazi wako awe tatizo kwenye ndoa yako. 


Sasa kwa nini wewe unakuwa kikwazo kwa mwanao? Kuna wakati hata mtoto wako mwenyewe wa kumzaa anakushangaa kwa tabia yako. Anakuona kama mama ni king’ang’anizi kwa namna ambavyo unataka kumuongoza. 

Anatamani hata akubwatukie ila anahisi atapata laana. Anahisi atakuchukiza wewe mzazi wake hivyo anaamua kukuvumilia. Nimejikita zaidi kwa baadhi ya akina mama wakwe kwa sababu wao ndiyo hasa wanaongoza kwa tabia hizo, ingawa hata baba wakwe ambao ni vichomi kwa watoto wao wapo. Unakuta binti au mke wa mwanao anajitahidi kukuvumilia, kujipendekeza na kujishusha lakini bado mama mkwe unakuwa hutosheki. Hela ya matumizi unataka mwanao akuachie wewe, bajeti au chakula cha siku hiyo unataka wewe ndiyo uwe mpangaji. Kweli ni sawa? Hivi umeolewa wewe au ameolewa mwanao? Hii ni aibu. 

Ni aibu kwa watoto wako wengine na kwa tabia hiyo unaweza kufanya watoto wako washindwe kuolewa au kuoa mabinti wa mtaani au wanaojua tabia yako kwa kuhofia kutokudumu kwenye ndoa kwa sababu tu ya kero na gubu zako. Kama uliridhia mwanao kuolewa au kumuoa mwanamke au mwanaume aliyenaye, basi wape nafasi. Hata kama umeenda kutibiwa, kuwa mpole. Fuata utaratibu wa nyumba ya mwanao kwani kila mtu ana mamlaka na nyumbani kwake. Subiri mwanao na mkewe wakija kwako uwape masharti utakayo. Ni hayo tu kwa wiki hii.

CHANZO: IJUMAA WIKIENDA

No comments