Header Ads

Kanga Moja Kiunoni... MBENGEMBEGE-22

 
 ILIPOISHIA : Hamadi! Sura ya baba Mei hii hapa! Mzee Hewa akashtuka kwani wakati mlango unafunguliwa alishaweka sura ya tabasamu akijua atamwona mama Mei. Kwa hiyo alipokutana na sura ya baba Mei ghafla, alikunja sura ghafla... SASA TAMBAA NAYO MWENYEWE...
“HAA! Hujambo bwana mdogo?” mzee Hewa alisalimia huku uso wake ukiwa haujakaa sawasawa... “Sijambo mzee, shikamoo...” “Marhaba, za safari bwana?” “Ni njema mzee wangu...vipi, nikusaidie nini?” Mzee huyo alibabaika kwa mbali hali iliyomshangaza sana baba Mei...“Nilitaka kujua kama kuna gesi maana jiko langu la gesi lime...aaah! Nataka kuazima kibiriti kwa mama! Oooh! Nimepitiwa, kuna maji ya baridi ya moto? Ha! Mimi naye kwa kusahausahau sijambo kidogo...naulizia milango kama mmefunga.” Baba Mei alibaki akimtumbulia macho tu huku akijiuliza ni kitu gani kinamfanya mzee huyo ababaike kusema kama kweli aligonga mlango akiwa na shida ndani kwake... “Mzee wangu kwani kuna nini, sikuelewi...” “Haa! Nilikosea kijana kugonga kwako, nilikusudia mlango ule,” alisema mzee Hewa huku akiondoka kurudi kwake. Ile baba Mei anageuka tu, mama Mei anatoka chumbani... “Vipi, ni nani?” alimuuliza mume wake... “Ah! Mimi sijamwelewa mzee wako...nadhani kuna kitu zaidi ya ujio wake,” alijibu baba Mei huku akiingia chumbani moja kwa moja. Mama Mei naye alifuata na kumkuta mume wake akiwa amelala akiangalia juu kwa mawazo... “Yule mzee asitake kuleta longolongo, kwa vyovyote vile alimfuata mke wangu. Inaonekana hakujua kama mimi nimerudi,” alisema moyoni baba Mei... “Baba Mei kwani kasemaje?” “Nani?”
“Mzee mwenye nyumba?” “Ah! Mimi sijamwelewa hata kidogo. Kwanza nahisi shida yake kubwa ni wewe ila mimi niliingilia kwa bahati mbaya tu...” “Kwani amesemaje?” “Hakuna kilichoeleweka... alipokutana macho na mimi, kwanza akashtuka sana. baada ya salamu akaniuliza habari za safari nikamwambia nzuri, akasema nilitaka kujua kama kuna gesi maana jiko langu la gesi lime...akasita, kisha akasema nataka kuazima kibiriti kwa mama! Akaacha, akasema oooh! Nimepitiwa, kuna maji ya baridi ya moto? Pia akaacha akasema naulizia milango kama mmefunga...” “Khaa! Ndiyo nini sasa?” aliuliza mama Mei huku akionesha kushangaa. Lakini moyoni alijua moja kwa moja kwamba, mzee huyo alikuwa na shida na yeye ila hakujua kama mume wake alisharejea... “Mimi sijui ndiyo nini!” alisema kwa mkato baba Mei na kugeukia kwingine hali iliyompa ishara mkewe kwamba, kuna jambo mumewe amejifunza kuhusu ujio wa mzee mwenye nyumba.
Mama Mei alibaki kimya. Alitamani sana kumsemesha mume wake lakini angemsemesha nini wakati mumewe amehisi jambo? Kumsemesha kungemfanya ajulikane kwa undani zaidi. Usiku wa manane, baba Mei alishtuka na kujikuta akimuwaza mzee Hewa, lakini pia akapata na mawazo kuhusu ule ukaribu aliouona kati ya mkewe na mpangaji mwenzao, Mfaume... “Inaonekana kuna kitu kilikuwa kikiendelea wakati mimi sipo. Mbona huyu mke wangu kama amekuwa mwenyeji sana na hawa watu?” alijiuliza. Kitabia, baba Mei si mtu wa kukurupuka! Mambo yake mengi hupenda kuyafanya kwa polepole na utaratibu huku akihakikisha kama ni jambo analipata kwa ukamilifu akitumia mahesabu ya mwaka! Alijichanga akili, akaamua kuweka mtego wa makusudi ili kujua kama kweli mke wake ana jambo la ziada au la, ni mawazo yake tu! *** Kulipokucha, mama Mei alitoka kitandani na kuendelea na kazi nyingine za kila siku za nyumbani kwake.
Asubuhi hiyo, alikuwa amekunja sura vibaya sana. hakumchangamkia mtu yeyote ndani ya nyumba ile maana alijua wanataka kumweka pabaya! Baba Mei alipoamka, alikwenda kuoga na kurudi ndani. Alivaa, akaenda sebuleni kunywa chai! Hapo alimwita mkewe... “Abee...” “Njoo mara moja.” Mama Mei alipofika alikaa akimwangalia mume wake kwa macho yaliyojaa wasiwasi... “Mimi jioni leo nasafiri tena, nakwenda Tanga halafu Arusha,” alisema baba Mei kisha akamwangalia mkewe ambaye aliachia sura ya tabasamu kutoka ile ya wasiwasi... “He! Yaani unaunga mume wangu?” “Ndiyo kazi sasa mke wangu, nitafanyaje?” “Kweli lakini,” alisema mama Mei huku akiachia tabasamu pana... “Kwa hiyo nilitaka ulijue hilo tu mke wangu maana nikiondoka nikirudi jioni ni safari,” alisema baba Mei na kuendelea kunywa chai... “Sawa mume wangu, safari njema,” alisema mama Mei naye huku akiondoka. Baba Mei alimwangalia mkewe akatingisha kichwa huku moyoni akisema... ITAENDELEA IJUMAA ....MTUNZI IRENE NDAUKA

No comments