Header Ads

Kanga Moja Kiunoni...Mbengembenge - 25


Mtunzi: Irene Mwamfupe Ndauka 
ILIPOISHIA : Kwa nini nisiende kumgongea yule kikongwe nimwambie nina wasiwasi mke wangu yumo chumbani mwake? Alifika mlangoni, akagonga na kuita... “Ngo ngo ngo! Wenyewe!” SASA JIACHIE KIVYAKO... BABA Mei hakuwa na wasiwasi wakati wa kugonga mlango huo kwani aliamini alichokiwaza ni kweli na kweli kabisa. Kazi ikawa kule chumbani, mama Mei na mzee Hewa walisikia sauti ya baba Mei kugonga na kuita ‘wenyewe’... “Mama weee! Mume wangu huyo anagonga,” alisema mama Mei huku machozi yakifika kwenye ncha ya kidevu chapuchapu! “Hebu tulia kwanza we binti, ngoja nikamfungulie, labda ana shida yake,” mzee Hewa alimwambia mama Mei huku na yeye akitetemeka... “Vipi, hajarudi shemeji?” Mfaume alimuuliza baba Mei alipomwona amesimama mlangoni kwa mzee Hewa akiwa amerudi kwa mara ya pili baada ya kuondoka na kurudi. Alikuwa amesahau kitu kingine...
“Hajarudi bwana, ndiyo nataka kumwachia maagizo huyu mzee akirudi ampe mimi naondoka,” alisema baba Mei maneno ambayo yalifika hadi ndani kwa wawili hao wakapata nguvu kwamba, kumbe alikuwa akigonga ili aache maagizo kwa baba mwenye nyumba. Mzee Hewa alikwenda kufungua mlango haraka sana huku akiachia tabasamu tayari kwa kuchukua maagizo. “Kwacha...kwacha...kwacha,” mzee huyo alifungua mlango wake kwa komeo. Alikutana macho na baba Mei, akazidisha tabasamu na kusema... “Karibu sana baba Mei.” Wakati huo, Mfaume alikuwa ameshachukua alichokitaka na sasa anaondoka zake na alikuwa akifunga mlango... “Mzee Hewa,” alianza kwa kuita baba Mei... “Ndiyo bwana, nakusikiliza...” “Naomba umtoe mke wangu haraka sana kabla sijaingia mwenyewe ndani,” alisema baba Mei akitumia sauti ya upole sana lakini yenye kila dalili ya hasira na maumivu ya wivu... “Khaa! Kwani amesema yupo ndani kwake?” “Yupo ndani kwako, ndani kwake wapi sasa we mzee,
umeanza kunichanganyia maneno kama kawaida yako siyo?” Mzee Hewa alianza kutetemeka, alijua kimenuka! Kumbe alichofikiria sicho. Kwa upande wake, Mfaume aliposikia maneno ya baba Mei hakutoa hata mguu mmoja pale mlangoni, aliendelea kusimama kusikia kilichopo... “Mh! Mbona madai makali sana! Ina maana huyu mzee anaweza kuwa na uhusiano na mama Mei kweli?” alijiuliza Mfaume. Yeye lengo lake lilikuwa kuhakikisha kama kweli, mama Mei anaweza kuwa na mzee huyo. Kwa uzee wake, na ujana wa mama Mei na sura yake ya utoto wa mjini na ujanja haikuwa rahisi kwa Mfaume kuamini kwamba, wawili hao wanaweza kuwa wapenzi. Kule chumbani, mama Mei alisikia kila kitu kwani mlango wa chumbani kutokea sebuleni ulikuwa wazi. Mwili wake ulilowa jasho la wasiwasi na woga. Usaliti ulimtafuna waziwazi, akakumbuka nyumba kadhaa walizoishi na mumewe huyo tangu wafunge ndoa, hazikukosa kelele za usaliti, baba Mei akimtuhumu mkewe
huyo. Mzee Hewa aliganda mlangoni, ikabidi Mfaume aingilie kati kwa kushauri... “Mzee, kama ni kweli mtoe mke wa watu, kama si kweli mwambie si kweli.” “Si kweli, hayupo,” alisema mzee Hewa kwa nusu kujiamini... “Basi mwingize mpaka chumbani kwako akahakikishe mwenyewe kwa macho yake. Maana unaweza kusema si kweli yeye akaona unamdanganya,” alisema Mfaume kwa sauti ya kimbeyambeya huku uso wake ukiwa kama anayesema... “Leo nitaona mengi.” Baba Mei alimsukuma mzee huyo bila kutaka kuweka mjadala mrefu kwani kwa uzoefu wake na usomi wake, alishajua mzee Hewa anaujua ukweli kuhusu mkewe... “Wewe mkeo hayupo humu ndani bwana...unanionea tu... toka...kama ni kodi ya nyumba naomba nikurudishie uhame mara moja,” alisema mzee huyo akimfuata kwa nyuma. Baba Mei hata kabla hajafika chumbani, mama Mei alianza kulia kwa sauti... “Nisamehe mume wangu... naomba msamaha sirudii tena jamani! Ooo! Shetani wewe
ni kwa nini mimi tu?” alisema mwanamke huyo. Sauti yake ilitoka mpaka nje, ikamfikia na Mfaume... “Hee! Ina maana kweli?” alijiuliza Mfaume... “Umenichosha we mwanamke. Hufai na wala hutakuja kufaa hata siku moja...unafanya mambo kama mtu mwenye akili pungufu! Hujitambui, hujifahamu wala hujihurumii,” baba Mei alimvurumishia maneno mazito na makali huku akimuwasha makofi kama siyo vibao... “Jamani basi....basi jamani! Baba Mei basi bwana, namna hii unaweza kuua hivihivi,” Mfaume alisema baada na yeye kuamua kuingia mpaka chumbani... “Hapana bwana, huyu mwanamke kusema ule ukweli ni matatizo juu ya matatizo... mimi ndiyo najua kila kitu. Kuaga kwangu kwamba nakwenda safari haikuwa jambo la kweli, nilitega tu,” baba Mei aliamua kufunguka... “Hodi nyumba hii,” sauti ya Jombi ilisikika akiingia...

No comments