Header Ads

Kasi ya Yanga uwanjani yawatisha Azam FC


LICHA ya ushindi wa penalti 4-1 walioupata katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Jumatano iliyopita, nyota wa Azam FC wamekiri kuwa Yanga ilicheza mpira mwingi uwanjani na kasi yao itasumbua msimu huu wa Ligi Kuu Bara unaoanza leo Jumamosi.
Katika mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, dakika 90 zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2 lakini Azam wakashinda kwa mikwaju ya penalti.
Mara baada ya mchezo huo, beki wa kutumainiwa wa Azam FC, Shomari Kapombe, alisema kasi kubwa ya Yanga katika kutandaza soka waliyoionyesha kipindi cha kwanza cha mechi hiyo ni balaa.
Alisema kama Yanga watakuwa wakicheza hivyo kwenye mechi zao zote za ligi kuu, basi timu zote zinazoshiriki ligi hiyo, zijiandae kwa changamoto ya kukabiliana nayo, la sivyo zinaweza kukumbana na balaa kubwa.
“Yanga walikuwa na kasi kubwa, kama mchezaji haupo vizuri, unaweza kuomba kutoka, hata hivyo tulipambana kwa nguvu zaidi na mwisho wa siku tukaibuka na ushindi.
“Kutokana na hali hiyo, naitazama timu hiyo kwa jicho tofauti kabisa kwani itasumbua sana ligi kuu kama timu hazitakuwa na maandalizi ya kutosha,” alisema Kapombe.

No comments