Header Ads

Kiungo wa MO Bejaia aivuruga kambi ya YangaDar es Salaam
 YANGA leo wataingia uwanjani kuvaana na MO Bejaia kwa tahadhari kubwa ya kumdhibiti kiungo mshambuliaji, Soumaïla Sidibé raia wa Mali baada ya benchi la ufundi la timu hiyo kupata taarifa zake.
Timu hizo, zinatarajiwa kuvaana leo kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumamosi limezipata, timu hiyo ilifanya kikao kambini kwao pamoja na kuangalia video za mechi za MO Bejaia ambazo imecheza na kumuona kiungo huyo ndiye mwenye madhara makubwa.
Taarifa hizo zinazema kuwa, kiungo huyo mwenye umbile kubwa, ana uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya vichwa, hivyo wamepanga kumdhibiti nyota huyo kwa kutoruhusu mipira ya krosi.
Akizungumzia hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, alikiri kuwepo kiungo huyo hatari ambaye tayari ameweka mikakati ya kumdhibiti kwa kuwaanzisha mabeki na viungo wakabaji wenye uwezo wa kuruka vichwa.
“Huyo mchezaji mweusi ninamjua ana umbile moja kubwa hivi, ni mchezaji mwenye madhara anayehitaji uangalizi wa hali ya juu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga vichwa.
“Tayari tumemuona kupitia video za mechi ambazo amezicheza, hivyo tutaingia uwanjani kwa kasi kubwa ya kupata ushindi na siyo kitu kingine,” alisema Pluijm.

No comments