Header Ads

Lowassa aibukia Simba SC na Mabadiliko!

Waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa (kushoto) akiwa Rais wa Simba Evance Aveva katika ofisi.

Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge
EDWARD Lowassa jana aliibukia kwenye Mkutano Mkuu wa Simba, hakufika kwa umbo lakini staili yake ilifika. Unaikumbuka ile staili ya ushangiliaji iliyokuwa inatumiwa na mgombea huyo wa urais katika uchaguzi uliopita kupitia Chadema kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)? Basi aina yake ya ushangiliaji iliteka mkutano huo.
Simba walifanya mkutano wao huo jana kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Masaki jijini Dar es Salaam uliohudhuriwa na wanachama 700.
Katika mkutano huo uliokuwa wa vituko na vioja vingi kutoka kwa wanachama hao, walikubaliana kupitisha ajenda kumi ambazo zote zilipitishwa chini ya Rais, Evans Aveva.
Simba (7)
Wanachama wa Klabu ya Simba wakiwa katika mkutano mkuu.

Lakini kabla hata mkutano haujaanza watu walionekana wanataka mabadiliko. Mkutano huo ulianza saa 5:08 asubuhi huku baadhi ya wanachama wakionekana kutaka mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa timu hiyo.
Dalili hizo za wanachama hao kutaka mabadiliko zilianza mapema kabla ya rais wa timu hiyo kuanza kupitia ajenda pale alipotoa salamu kwa kutamka Simba na wenyewe wanachama wakatamka mabadilikoo, huku wakiichezesha mikono yao kama ile staili ya mabadiliko iliyoanzishwa na Ukawa baada ya kumpata Lowassa.
Simba (6)
Rais wa Simba, Evans Aveva wakati akiwasili jana.

Lowassa alivuma sana kwa staili hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba, mwaka jana. Lilipokuwa likitamkwa jina lake Lowassaaaa, watu waliitikia mabadilikooo, ilipotamkwa mabadilikooo, waliitikia Lowassaaa. Sasa jana ilikuwa ni “Simbaaa” halafu watu wanaitikia mabadilikooo.”
Kimsingi, wanachama karibu wote waliohudhuria mkutano huo wa jana, walitaka timu hiyo apewe Mohammed Dewji, maarufu kwa jina la Mo ambaye anataka kununua hisa asilimia 51 za klabu hiyo kwa dau la Sh bilioni 20.
Kitendo hicho cha staili ya Lowassa hakikutokea kwa Aveva pekee, pia ilitokea kwa Mwakilishi wa TFF, Wallace Karia aliyepita mbele na akatoa salamu kwa kutamka Simbaaa na wanachama wakaitikia mabadilikooo.
Hali hiyo, ilikuwa ikitokea kila wakati pale wanachama au viongozi wakipita mbele ya ukumbi kwa ajili ya kutoa salamu ya kutamka Simba badala ya kuitikia oyeee, wanachama wakawa wanatamka mabadilikooo.
Aina hiyo ya ushangiliaji iliendelea hadi mwisho wa mkutano huo saa 7:00 mchana mara baada ya Aveva kufunga mkutano huo.
simba (1)
Rais wa Simba SC, Evans Aveva akizungumza na wanachama wa timu hiyo leo wakati wa mkutano mkuu.

Lowassa yupo karibu na uongozi wa Simba, mwaka jana Aveva aliwahi kumtembelea ofisini kwake na kufanya mazungumzo.
MO njiapanda
Suala la Mo kupewa timu, lilionekana kuungwa mkono na wanachama wengi kutokana na timu kuwa katika hali mbaya ya kiuchumi. Wanataka timu ifanye usajili wa kutisha na uwekezaji wa kiwango cha juu ili kuendana na kasi ya wapinzani wao Yanga na Azam FC.
Katika msimu wa 2014/15, klabu hiyo ilifanikiwa kujikusanyia Sh bilioni 2.09 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya mapato lakini ikatumia Sh bilioni 2.1 na kujikuta ikidaiwa Sh mil 4.3
Lakini pia katika bajeti yake ya msimu ujao wa 2016/17 uongozi huo unatarajia kukusanya kiasi cha Sh bilioni 3. 5 kutoka katika vyanzo vyake vya mapato, lakini matumizi yake yanatarajiwa kuwa Sh bilioni 4. 4, hivyo itakuwa ikidaiwa Sh milioni 828.
Kutokana na hali hiyo wanachama hao waliutaka uongozi huo, kukubali kumpatia Mo timu kwani wanataka mabadiliko na wamechoshwa na hali hiyo ya ukata wa kila wakati ambao umekuwa ukiwatesa na kuwakosesha amani kila siku.
Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo chini ya rais wake, Evans Aveva, haukuwa tayari kufanya hivyo licha ya kelele za wanachama hao ambao kila wakati walikuwa wakiimba na kulitaja jina la Mo.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano huo uliomalizika kwa makubaliano ya mabadiliko, Aveva alisema: “Hivi karibuni tuliunda kamati ya kukusanya maoni kutoka kwa wanachama wetu ili kupata maoni yao ni jinsi gani wanataka klabu yetu ijiendeshe, mapendekezo yao yalikuwa ni ya aina mbili, ya kwanza yalikuwa ni yale ya kujiendesha kwa mfumo wa ufadhili na ya pili yalikuwa kwa mfumo wa hisa.
“Baada ya kamati hiyo kutupatia maoni hayo ndipo tulipoamua kuyaleta katika mkutano huu, hivyo kwa pamoja Wanasimba wameridhia kuwepo kwa mabadiliko, hata hivyo bado hatujajua tutajiendesha kwa mfumo gani, ule wa hisa au wa ufadhili kwa sababu ripoti hiyo bado haijakamilika.
“Kilichopitishwa ni kwamba kweli tunataka mabadiliko lakini hatujajua kama ni ya hisa au ya ufadhili, kamati itakapomaliza zoezi hilo tutakuja tena kulizungumzia suala hilo katika mkutano mwingine utakaofanyika hapo baadaye. “Ukiangalia pia hata watu waliohojiwa na kamati hiyo kupata maoni ni 23 tu, kwa ukubwa wa Simba watu hao ni wachache sana, hivyo tutaipa muda kamati hiyo ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi na baada ya hapo ndipo tutakapokuja na jibu sahihi ya namna gani tutajiendesha baada ya leo hii kupata ridhaa ya kufanya mabadiliko.
“Nawaomba Wanasimba wenzangu wasiwe na hofu juu ya hilo, kwani ni lazima mabadiliko yafanyike kwa sababu hata mfumo wa soka la kisasa wa klabu kuwa na leseni unatufunga,” alisema Aveva.
Kuhusiana na Mo, Aveva alisema: “Mpaka sasa bado hatujapata barua ya Mo kuhusiana na kuitaka timu yetu ila ambacho amekuwa akizungumzia ni adhima yake ya kuitaka Simba.
“Lakini ninachoweza kusema ni kwamba, Mo ni Mwanasimba mwenzetu, tutakaa naye na tutazungumza naye na tukifikia makubaliano basi tunaweza kumkabidhi timu.”
Kauli hiyo inaonyesha bado suala la Mo kukabidhiwa timu lipo njia panda, kwani kama barua tu haijafika, linaweza kuchukua muda. Pia Simba bado haijaamua ni mabadiliko gani itayafanya, je, itatumia wafadhili au hisa? Hivyo inaonyesha suala hilo bado lina muda mrefu wa kuchambuliwa na si la leo wala kesho.

CHANZO; CHAMPIONI

No comments