Header Ads

Manji: Nimechoka, napumzika


Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
TAARIFA zinazodai kuwa mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ameachia ngazi kwenye klabu hiyo zimezidi kuitafuna nchini nzima, huku mwenyewe akilieleza Championi: “Nimechoka nataka kupumzika.”

Manji amekuwa nguzo ya umoja kwenye Klabu ya Yanga kwa muda mrefu sasa, huku uwepo wake klabuni hapo ukimaliza migogoro yote ambayo ilikuwa ikitokea siku za nyuma.
Lakini pia mwenyekiti huyo amepata mafanikio kadhaa kwenye timu hiyo ikiwa ni pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu kwa kipindi chake chote cha uongozi tangu mwaka 2012.
Bado mwenyekiti huyo hajaweka wazi asilimia 100, nia yake ya kuachana na timu hiyo, lakini dalili zinaonyesha kuwa kuna jambo kama hilo baada ya viongozi mbalimbali pamoja na Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali kupinga suala lake la kutaka kuikodi nembo ya timu hiyo kwa miaka kumi.
Mara baada ya kuzuka kwa taarifa hiyo juzi ambayo iliwashtua mashabiki wengi wa soka, siyo wa Yanga tu bali Tanzania nzima kutokana na mchango wa kiongozi huyo, Championi liliwasiliana naye ambapo hakuweka wazi kuwa ameachia ngazi lakini akasema kwa ufupi:
 “Ndugu yangu ningependa uniache, mimi pia ni binadamu. Wakati mwingine napenda kupumzika.
“Haiwezekani mimi nikawa mbaya kwa kila kitu, muda wangu, fedha na mambo mengi nafanya kwa ajili ya Yanga. Lakini watu wananipiga vita sana, hadi inafikia nakata tamaa.”
 “Naomba uniache ndugu yangu, nimechoka, nataka kupumzika,” alimalizia Manji huku akiongea kwa majonzi.
Hata hivyo, tangu taarifa hii itoke kumekuwa na kauli tata za mara kwa mara, huku jana viongozi  wa matawi wa klabu hiyo wakikutana na kutaka Mzee Akilimali avuliwe uanachama wake kutokana na kauli ile aliyoitoa kuwa Manji amekurupuka kutokana na kitendo chake cha kuitaka Yanga kwa miaka kumi.
Lakini waliomba kwa nguvu zote kama mwenyekiti huyo ana nia hiyo, basi aachane nayo mara moja.
Wanachama hao walisema wanataka Katibu Mkuu wa Yanga,  Baraka Deusdedit, apeleke suala hilo kwenye sekretarieti ya Yanga ili mzee huyo asimamishwe uanachama.
Kuonyesha kuwa Manji ana umuhimu mkubwa kwenye klabu hiyo, wanachama wa klabu hiyo walijazana klabuni hapo tangu juzi mara tu baada ya taarifa hizo na jana walikuwa wengi mpaka kusababisha baadhi ya shughuli kusimama.

No comments