Header Ads

Mavugo, Ajibu waandaliwa kuwapoteza Ngoma, TambweMASTRAIKA wa Simba, Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo, wanaandaliwa kuja kuwa wafungaji wazuri kwenye Ligi Kuu Bara huku wakibebeshwa zigo la kuvunja utawala wa mastraika wa Yanga, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Kikosi cha Simba msimu uliopita kilikuwa kikimtegemea zaidi Mganda, Hamisi Kiiza katika safu yao ya ushambuliaji. Nyota huyo  alimaliza msimu akiwa na mabao 19, nyuma ya Tambwe aliyeibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 21.

Mpaka sasa tayari Kocha wa Simba, Joseph Omog, ameshatengeneza kombinesheni ya hatari ya safu yake ya ushambuliaji ambapo Ajib na Mavugo ndio watakuwa wakicheza pamoja kwa muda mwingi huku Muivory Coast, Fredric Blagnon na Danny Lyanga wakisubiri.

Katika kuitengeneza kombinesheni hiyo, Omog amekuwa akiwafundisha mabeki wake wa pembeni pamoja na mawinga kupiga krosi nyingi kuwafikia washambuliaji hao. Kwenye mazoezi yao ya kila siku, wamekuwa wakifanya hivyo na zoezi hilo kuonekana kueleweka.
Omog ameliambia Championi Jumatatu kuwa, kila siku anaangalia namna gani timu yake itakuwa inapata ushindi kwa urahisi na kugundua kwamba mipira ya krosi itawabeba zaidi.
“Kuna njia nyingi za kusaka ushindi, mara kwa mara nimekuwa nikiwafundisha hivi na kuonekana kuelewa zaidi, hivyo naamini hii ndiyo itakuwa rahisi kwetu kupata mafanikio msimu ukianza. Nataka kutengeneza safu bora zaidi ya ushambuliaji kwenye ligi,” alisema Omog.

No comments