Header Ads

MAVUGO AONGEZEWA MAJUKUMU SIMBA

TOFAUTI na ilivyotarajiwa na wengi kuwa straika mpya wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, atasimama kama straika wa mwisho na kazi yake ni kufunga tu, hiyo kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog haipo hivyo na tayari straika huyo
ameongezewa majukumu mengine tofauti na hilo kikosini hapo.

Omog ameliambia Championi Jumamosi kuwa, kwake hakuna straika atakayecheza sehemu moja, ndiyo maana hata Mavugo aliyetua Simba hivi karibuni akitokea Vital’O ya Burundi, tayari ameshaanza kumnoa kucheza kama straika wa pili, winga na hata mpikaji wa mabao kwa wenzake.

Kauli hiyo ya Omog, raia wa Cameroon, inashabihiana na mazoezi waliyofanya timu hiyo wiki hii kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya leo dhidi ya Ndanda FC ambapo Mavugo alionekana kufanya mashambulizi akitokea pembeni kwa kupiga mashuti ya mbali na ‘kufosi’ kuingia na mpira
ndani ya boksi la wapinzani.

Mbali na Mavugo, Muivory Coast, Fredric Blagnon na Danny Lyanga ambao nao ni washambuliaji wa kati, walionekana wakifanya mashambulizi kutokea pembeni na
wakati mwingine kama straika wa pili, nafasi ambazo walizimudu kwa ufanisi mkubwa.
“Kwangu unapokuwa mshambuliaji ni lazima ucheze na uguse nafasi zote za mbele, yaani unaweza kuhama kati na kusogea kushambulia kwa kutokea pembeni na bado ukacheza vizuri na kuisaidia timu.

“Lakini hiyo pia ina maana ya mastraika wote kucheza kwa ushirikiano kwamba mwingine akienda kushoto kushambulia basi aliyekuwa kushoto atarudi kati kusubiri mipira na kufunga, vivyo hivyo kwa aliyekuwa kulia anaweza kuhama kuingia kati na kwenda kushoto na kisiharibike kitu, ndiyo maana ukaona Mavugo pia nimemweka pembeni na amecheza vizuri,” alisema Omog ambaye aliwahi kuwa kocha wa Azam FC.

No comments