Header Ads

Mbinu 10 ambazo mtu ataweza kuzitumia katika hali ngumu ya uchumi na ukafanikiwaZiko mbinu kumi ambazo mtu unaweza kuzitumia katika hali ngumu ya uchumi na ukafanikiwa, nilizitaja wiki iliyopita, sihitaji kuzitaja tena hapa bali nitakwenda moja kwa moja kwenye kuizungumzia moja baada ya nyingine:

1. USIBABAIKE 
(Don’t panic) Ukweli ni kwamba nyakati mbaya hutokea katika maisha ya kila mmoja wetu, mambo mabaya huwapata watu wazuri na mambo mazuri hutokea kwa watu wabaya pia. Hata kama umeokoka na unampenda Yesu, lazima katika maisha yako utakutana na kipindi kigumu maishani, kuokoka siyo kinga ya wewe kukutana na matatizo bali ni njia ya kuweza kuthibitisha uwezo ulionao kupambana na matatizo. Hivyo basi unapokutana na wakati mgumu maishani, USIBABAIKE,  tulia. Jikumbushe kwamba wewe siyo mtu wa kwanza duniani kuingia katika wakati mgumu,
si mtu wa kwanza kufiwa au kufukuzwa kazi au kufilisika, watu wengi walishapitia hali hiyo kabla yako. Lazima uelewe kwamba hakuna jambo ambalo halitapita, hili nalo pia litapita kama yalivyopita mengi huko nyuma. Hali hii ya kutulia itakusaidia kuupa ubongo wako nafasi ya kufikiria njia bora zaidi ya kulitatua tatizo unalokuta nalo, kwani ubongo uliochanganyikiwa hauwezi kutoa majibu sahihi kwa matatizo, fikra mbaya matunda
yake huwa ni maamuzi mabaya. Ukitaka kufanikiwa katika wakati mbaya, uwe ni wa uchumi au  kitu chochote, tulia, hakika utauona mlango wa kutokea na mwisho wa siku utakuja kuwa na mafanikio makubwa kuliko uliyokuwa nayo awali. 


2. PEMBUA
 Unapoingia kwenye wakati mgumu kiuchumi, ukatulia, kinachofuata ni kupembua au kuchambua ukijiuliza maswali kama “Tatizo ni nini?” “Nini kimesababisha?” “Nitafanya nini kutatua?” ukipeleka maswali haya kwenye ubongo ambayo kazi yake ni kuchakata maswali haya na kukupa majibu, hakika utapata suluhisho la matatizo yako ambalo ukilitumia ni hakika utajikuta umefanikiwa katika wakati mgumu. Katika hili lazima niweke msisitizo kidogo, nimesema PEMBUA! Siyo pembua, pembua, pembua na pembua bila kufanya chochote! Watu wengi, hasa wasomi katika maisha wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kupembua sana bila kutenda, hili ni kosa, kuna kitu kinaitwa “Upembezi yakinifu” kimewafanya watu wengi sana kushindwa kupiga hatua maishani kwa sababu hubaki kupembua na kupembua na kupembua bila kutenda chochote. Kama unataka kufanikiwa kwenye wakati mgumu,
jambo unalotakiwa kufanya ni kupembua na kugundua tatizo kisha kutafuta suluhisho na ukishajua kinachofuata ni kutenda, mengine utaendelea kujifunza mbele ya safari (take a calculated risk). 


3. BADILI MKAKATI 
Yawezekana umezoea kufanya kazi au biashara yako katika mtindo fulani, mfano wewe ni mfanyabiashara wa gazeti kama mimi, umezoea kuandaa habari zako na kuzichapa kwenye karatasi ndipo uziuze!
Ghafla wakati umebadilika, watu wanaanza kusoma magazeti kwenye simu, mauzo yako yanashuka kwa sababu ya jambo hili, je, utaendelea kuuza magazeti yako kwa mtindo uleule wa zamani? La hasha! Utalazimika kubadilisha mtindo, vinginevyo biashara yako itakufa, ndiyo maana kampuni nyingi za magazeti duniani, sababu ya ujio wa teknolojia, watu wakapunguza kununua magazeti ya kwenye karatasi, zililazimika kuanza kutengeneza magazeti mtandao au Applications (Apps) ambazo watu badala ya kununua karatasi waliyasoma magazeti moja kwa moja kupitia mtandao au simu zao kwa gharama ndogo zaidi na kwa sababu watu wengi zaidi walinunua magazeti kwa mtindo huo sababu ya bei kuwa ndogo kampuni za magazeti zilitengeneza fedha nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hata wewe yawezekana kabisa ulikuwa na biashara fulani ambayo mambo yamebadilika na huuzi tena, badilisha mkakati, lakini uzidi kusonga mbele! Usikomee hapo wala kurudi nyuma, kama ulikuwa mpiga picha, kamera yako inatumia mkanda ambao ni lazima uende kusafisha, badilisha kamera hiyo nunua nyingine ya dijitali ambayo hutumii mkanda wa kwenda kusafisha baadaye. Yawezekana ulikuwa na internet cafe, lakini kwa sababu
watu wanapata huduma za internet kwenye simu zao moja kwa moja, idadi ya watu wanaotembelea kwenye kibanda chako imepungua, mapato yako yameshuka, badilisha mkakati kwa sababu nyakati zisizo za kawaida zinahitaji matendo yasiyo ya kawaida ili kufanikiwa, usiendelee kama ulivyozoea. 


4.USIPOTEZE  MWELEKEO 
(Don’t loose focus) Hali ngumu ya uchumi mara nyingi hutuvuruga na kutufanya tupoteze mwelekeo au tupotee njia maishani, ulikuwa na lengo la kufanya jambo fulani, ukalianza kwa mafanikio makubwa lakini ghafla mambo yakabadilika na kuwa mabaya. Watu wengi wanapokuwa katika hali hii, jambo pekee ambalo hulifikiria ni kuacha na kuanzisha kitu kingine, matokeo yake hujikuta wamepoteza mwelekeo na ndoto zao za mwanzo! Ni vizuri kung’ang’ana kama bado unaendelea kuamini kwenye jambo unalolifanya, huku ukiendelea kubadilisha mikakati kila mara ilimradi tu usonge mbele. Ni ukweli kwamba hakuna kitu ambacho hufanikiwa kirahisi, lazima kutakuwa na vikwazo vingi njiani ambavyo mara nyingi vimemaanishwa kutuimarisha na si kutubomoa kama ambavyo watu wengi wanaweza kutafsiri. Lengo kubwa ni kufanya vizuri, kufanikiwa! Hivyo unapokutana na changamoto ni vizuri kubaki kwenye reli, badala ya kukubali kudondoshwa mtaroni, ni kweli unaweza kuanguka lakini nyanyuka, rejea kwenye reli na usonge mbele na safari yako. 

5. HAKIKISHA UNAENDELEA KUWA BORA 
Wakati wa hali ngumu ya uchumi, mambo yanapoanza kwenda vibaya, watu wengi sana huanza kupunguza ubora katika shughuli zao ili wapate faida zaidi! Hili ni kosa kubwa sana kulifanya katika maisha ya biashara, kamwe usipunguze thamani ya bidhaa au huduma zako wakati watu wengine wote wanafanya hivyo, hii itakufanya wewe ung’are kuliko wengine na sifa zako zitasambaa na wateja wataelekezana ofisini kwako matokeo yake utatengeneza fedha nyingi kuliko washindani wako. Ingawa hali ya uchumi itakuvuruga, endelea kuboresha huduma zako, sehemu yako ya kazi ipake rangi upya, namna unavyofunga bidhaa zako tumia vifungashio vipya, wakati wenzako wamenuna wewe vaa tabasamu usoni, wateja wote watakimbilia kwako na hakikisha unaimarisha uhusiano na wateja wako kwa kuwauliza mambo mbalimbali kuhusu biashara zao, familia nk. Anzisha utaratibu wa kuwasiliana nao mara kwa mara, kwani biashara si tu kuuziana bali mahusiano kati ya mfanyabiashara na mteja. Waite wateja wako kwa majina yao mfano “Karibu sana Rashid, za nyumbani? Shemeji hajambo? Vipi mtoto wako wa kwanza anaendeleaje na shule? Karibu sana aisee, vipi leo tukupimie nini?” maswali ya aina hii yanaweza kuonekana madogo na yasiyo na maana lakini ni gundi au nta ya kumnasa mteja moja kwa moja. Mtu anayehudumiwa kwa mtindo huu, hawezi hata siku moja kufanya biashara na mtu anayemhudumia akiwa amenuna, hata kama alikuwa amehama, atarejea alikokuwa akiulizwa maswali hayo na kueleza siri zote za upande wa mshindani. Nitaendelea na sehemu ya sita hadi ya kumi wiki ijayo

No comments