• Latest News

  August 20, 2016

  MESSI NI MAISHA YA WANA BARCELONA

      Kipenzi cha watu wa Barcelona, Lionel Jorge Messi. 
  Na Saleh Ally, Barcelona
  LIGI Kuu Hispania maarufu kama La Liga imeanza kutimua vumbi huku kukiwa na mengi ya kuwaza au kubashiri, lakini hauwezi ukaizungumzia bila ya kumtaja Lionel Jorge Messi raia wa Argentina.

  Messi ndiye kipenzi cha watu wa Barcelona, mji wenye wakazi wapatao milioni mbili kwa sasa ambao pamoja na kuwa na kila aina ya biashara, wanaamini maisha yao kwa kiasi kikubwa yanaendeshwa na kikosi cha Barcelona na tegemeo lao kubwa kwa miaka mingi sasa, wanamtegemea zaidi Messi.
  efcb1b57-dafc-4611-93eb-1706a47a7f7e

  Baadhi ya wafanyabiashara ambao wamefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka kumi katika Jiji la Barcelona, wanasema hata wakati Luis Figo anatamba au Ronaldinho, hawakuwahi kuwa na biashara nzuri kama kipindi hiki cha Muargentina huyo ambaye heshima yake ni kubwa kuliko mtu yeyote anayeishi katika mji huu.
  kandambiliza messi na barcelona
  Inajulikana, adui namba moja wa Mji wa Barcelona ni Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na shujaa ni Messi. Kwani kila anapofanya vizuri uwanjani, anaisaidia klabu yake ya Barcelona kuingiza mamilioni ya fedha kupitia wageni wanaotembelea Camp Nou, wananunua bidhaa na kadhalika, yote ni fedha.
  Kufanya kazi vizuri kwa Messi, kunaposaidia kuongeza wageni ndiyo faida kubwa kwa wafanyabishara wa jiji hili la Barcelona ambalo ni kati ya miji inayovutia sana barani Ulaya kutokana na kuwa na mpangilio mzuri sana na mvuto wa juu kabisa.
  leo 2
  Wanaouza jezi au fulana za Messi baada ya kuzinunua kihalali kwenye Klabu ya Barcelona, wamekuwa wakipata faida kubwa ingawa inaelezwa kuna katazo kutoka Kampuni ya Adidas inayomdhamini Messi. Haitaki kutoa fulana nyingi kwa kuwa inaona zitachangia kuchuja kwake.
  Watu wanashindwa kufyatua kwa kuwa ukikamatwa huku hakuna mchezo, ni jela au faini inayoweza kukulazimisha kuuza magari yako au kukumaliza kabisa kibiashara.
  Wafanyabiashara wa jezi za Messi ambazo ni halali nao wanapata biashara na zimekuwa ni ‘hot cake’ kwao au biashara inayotoka sana kuliko nyingine yoyote.
  leo 4
  Awali Barcelona ilitenga hadi euro 650,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.5) kwa ajili ya promosheni ya biadhaa zake, lakini iliamua kuzitoa jezi au vifaa vya Messi kwa kuwa vimekuwa vikijitangaza, kujiuza na hata kuvitangaza vingine.
  Dereva taksi wa eneo la Sans katika jiji hili, Alejandro Garcia anasema wateja wake wengi wamekuwa wakimzungumzia Messi kila wanapoingia katika taksi yake.
  Amesema anapenda mpira, lakini katika miaka yake yote 44 sasa ya kuishi Barcelona, hajawahi kumuona Messi ambaye alifika jijini hapo akiwa na miaka 13.
  “Amenikuta hapa, lakini sijawahi kumuona. Ni vigumu sana kumuona lakini kila mtu anamuulizia. Anasaidia sana biashara yetu, tunaamini watu wengi hufurahia kufika hapa wakiamini ni sehemu anayoishi Messi,” anasema.
  Messi ni mfalme wa Barcelona, hakuna anayeweza kukataa. Ukiachana na wauza jezi, hata wenye mahoteli, wanasema watu wengi hufika katika Mji wa Barcelona ili kuutembelea Uwanja wa Camp Nou lakini gumzo kubwa limekuwa ni Messi.
  Inaonekana pamoja na uwezo wa soka, Messi amegeuka kuwa msaada kibiashara katika maisha ya wakazi wengi wa Barcelona kutokana na kuwa na tabia ya aina yake kabisa.
  Anapenda kujificha, hapendi makuu, zaidi ya mpenzi wake, Antonio Rucuzzo waliokua pamoja katika Mji wa Rosario kwao, Argentina, hajawahi kusikika hata kubadilisha tu mpenzi.
  Hii kwa wazazi wengi wa Ulaya hupenda kuona watoto wao wanakuwa kama Messi. Hivyo kufanya idadi kubwa ya wazazi kughalimika kutoka katika nchi mbalimbali ili kuwatembeza katika Jiji la Barcelona na makao makuu ya Barcelona.
  Msimu uliopita, Messi alitengeneza hadi dola milioni 41.3 (zaidi ya Sh bilioni 88), ni bilionea lakini si rahisi kumuona akifanya mbwembwe, hili linazidisha umaarufu wake kwa kuonekana si mpenda makuu.
  wanachagua jezi ya messi
  Kupitia wadhamini tu mfano wa Gillette, Samsung, Gatorade na sasa Huawei, Messi anaingiza zaidi ya dola milioni 22.5 kupitia matangazo hayo tu. Yaani nje ya mpira na kumfanya kuwa kati ya wanamichezo wanaoingiza fedha nyingi sana katika matangazo.
  Kumbuka, Adidas wanamlipa dola milioni 4 (zaidi ya Sh bilioni 8.5) kwa mwaka na kumfanya kuwa mwanamichezo anayelipwa zaidi na kampuni hiyo kubwa ya michezo ambayo inawadhamini wanamichezo mbalimbali duniani.
  Thamani yake kama klabu yoyote ikitaka kumnunua ni dola milioni 340, Barcelona iliwahi kutangaza. Huenda kusiwe na klabu nyingine yoyote inaweza kumnunua.
  Lakini hata kubaki naye tu, Barcelona haina shida wala shaka kwa kuwa inaendelea kuingiza mamilioni ya fedha ikimtumia yeye kama chanzo cha biashara.
  Messi ni faida kwa klabu yake ya Barcelona, lakini ni faida kubwa kwa wakazi wa Jiji la Barcelona ambao wanafaidika kwa yeye tu kuwa mkazi wa jiji hili.
  FIN.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MESSI NI MAISHA YA WANA BARCELONA Rating: 5 Reviewed By: 2jiachie
  Scroll to Top