Header Ads

Mke wa Mzee Yusuf anena mazito!

 
 Wakati tangazo la Mfalme wa Muziki wa Taarab ‘Mwambao’, Mzee Yusuf kuacha muziki kisha kumrejea Mungu wake likiwa limezua gumzo kubwa, mmoja wa wakeze, Leila Rashid amenena mazito akiweka wazi madhara yatakayoikumba bendi yao ya Jahazi Modern Taarab na familia kwa jumla. Ilikuwa Ijumaa iliyopita ya Agosti 12, mwaka huu, muda mfupi baada ya kumaliza Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ilala-Bungoni (Masjid Taqwa) jijini Dar, huku akibubujikwa na machozi ndipo Mzee akatangaza rasmi kuachana na muziki akiwaomba waumini wamuombee msamaha kwa Allah kwa kipindi chote alichokuwa amemuasi Mungu. Baada ya tamko hilo, Wikienda lilitaka mahojiano maalum na Mzee Yusuf ili afunguke zaidi juu ya uamuzi wake huo lakini alijibu: “Siwezi kuongea na mwandishi mmojammoja badala yake nitaitisha mkutano na vyombo vya habari kwa sababu
kwa utaratibu wa dini yangu, siwezi kuongea na huyu kisha nikaongea na huyu kwa jambo hilohilo.” WIKIENDA LAMGEUKIA LEILA Kwa upande wake mkewe alilifungukia Wikienda mambo mengi ya nini kinafuata baada ya tangazo la mumewe huyo. Leila alisema, ishu ya mumewe kuacha muziki imeathiri mambo mengi kwake na kubwa zaidi ni ndani ya Jahazi ambayo muda wote ilikuwa ikitegemea huduma yake kwa kila jambo ikiwemo kutunga na kutengeneza nyimbo. “Imeniathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu ni mtu ambaye nilikuwa nimemzoea kuwa naye kila mahali hasa kwenye shoo. “Ukiachana na mimi, kuna Timu ya Jahazi. Hawa nao ni waathirika wakubwa sana kwani tutakosa vitu vingi kutoka kwake. “Mzee amekuwa akitunga kila kitu kwenye nyimbo za Jahazi. Hata pale ilipotokea mtu mwingine akatunga, basi jukumu la kuuandaa wimbo hadi unatoka alikuwa akihusika kwa asilimia zote. “Ukiwaza kwa kina utaona ni kwa kiasi kikubwa sana Jahazi itayumba, japokuwa tunaamini kutatokea mtu
mwingine wa kusaidia kutunga na kuandaa nyimbo nzuri. Wikienda: Ukiachilia mbali bendi, kwa upande wako kama mke wake umeathirikaje? Leila: Sina athari sana maana wazo la kuacha muziki amekuwa akiniambia zaidi ya miaka mitatu nyuma. Hivyo, alipofikia uamuzi huo, mimi sijashtuka maana ninaamini muda wake umefika na siwezi kumpinga hivyo ndivyo Allah alivyomjalia. Wikienda: Hakuna masharti yoyote aliyokupa? Leila: Hakuna. Wikienda: Huoni kwa kuwa mumeo ameacha muziki, ili usimuingize kwenye dhambi na wewe inabidi uache kuimba? Leila: Hahaha…niache kuimba? Kha! Kwa lipi sasa? Maana yeye ameacha muziki kwa sababu imani imemtuma hivyo. Ndiyo maana utaona hata mimi hajanikataza, sidhani kama ninaweza kuacha kwa sasa. Wikienda: Nasikia tangu Mzee amrudie Mungu amekuwa akilala msikitini na muda mwingi anashinda huko, hilo likoje? Leila: Hapana. Hakuna ishu ya kulala msikitini, zaidi anahudhuria kwenye ibada kama ilivyo siku zote na akitoka anakuwa nyumbani tu. Wikienda: Inasemekana amekupiga marufuku kumpigia simu hadi yeye akupigie, je, ni kweli? Leila: Khaaa…kwa nini anikataze kumpigia wakati mimi ni mkewe? Shida za nyumbani tutatatua vipi sasa? Hapana aisee, sema tu, hivi karibuni alisafiri kwenda vijijini, huko ‘network’ ilikuwa inasumbua hivyo akalazimika kuwa ananipigia yeye anapokuwa hewani. Wikienda: Pia amepiga marufuku nyimbo zake kupigwa kwenye vyombo vya habari na sehemu zote, hilo likoje? Leila: Hapana, hajapiga marufuku isipokuwa anatamani watu waache kabisa kupiga nyimbo zake ila hawezi kuwazuia maana hata sisi (Jahazi), nyimbo nyingi tunazoimba ametunga yeye na kama hajatunga kuna nyimbo ambazo ameimba nasi tunazidi kuziimba. Sasa akikataza, Jahazi itaimba nini? Wikienda: Je, wewe hufikirii kumuunga mkono kwa kuachana na muziki, ushike imani kama yeye? Leila: Kusema kweli kwa sasa siwezi maana suala la kuacha na kushika imani kali kama yeye ni wito wa Mungu na hata yeye hajataka mwenyewe ila nguvu ya Mungu ndiyo imemtaka. Kwa upande wangu nafanya ibada zote na ninamuamini sana Mungu. Ikitokea siku moja Mungu akataka niwe hivyo, Inshaallah nitamfuata. Wikienda: Nyimbo zake kwa sasa ndani ya Jahazi ataziimba nani? Leila: Tangu mwanzo kulikuwa na watu wanaziimba ila ninaamini menejimenti itakaa na kujua nani atatunga na atakuwa akiimba kwenye nafasi zake.

No comments