Header Ads

Mo noma aikabidhi Klabu ya Simba shilingi milioni 100Dar es Salaam
MFANYABIASHARA mkubwa nchini, Mohamed Dewji (Mo), jana aliikabidhi Klabu ya Simba shilingi milioni 100 zitakazotumika kwa ajili ya usajili wa wachezaji watakaowatumia msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Hiyo ni siku chache tangu Mo autake uongozi wa timu hiyo kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo unaoongozwa na Rais Evans Aveva na kumuuzia hisa asilimia 51.
Uongozi wa timu hiyo, uliazimia kubadilisha mfumo huo wa uendeshaji wa klabu baada ya wanachama kushinikiza kwenye Mkutano Mkuu uliofanyika wikiendi iliyopita.
Akizungumza na Championi Jumatano kwenye Ukumbi wa Jubilee Tower, Posta jijini Dar zilipo ofisi zake, Mo alisema fedha hizo amezitoa kama mwanachama wa kawaida katika kuhakikisha timu yao inafanya vyema msimu ujao wa ligi.
Mo alisema kama Simba wangekubali mapema mapendekezo ya uboreshaji wa uendeshaji wa klabu hiyo, basi angetoa Sh bilioni moja kwenye usajili huo, lakini kutokana na kubaki siku sita kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, ni ngumu kwake kutoa fedha hizo.
Alisema kuwa msimu ujao wa ligi kuu, amepanga kutumia Sh bilioni moja kwa ajili ya usajili kama uongozi Simba utampa timu hiyo kuhakikisha wanasajili wachezaji wenye uwezo watakaokidhi vigezo vya kucheza Msimbazi.
Aliongeza kuwa, pia atatafuta maskauti wazuri watakaozunguka Afrika nzima kwa ajili ya kutafuta wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuichezea Simba ili wafikie malengo yao ya kuwa mabingwa wa Afrika.
“Simba wenyewe wameyataka kwa kuchelewesha mipango yangu ya kusajili wachezaji wazuri, kama viongozi wangekubali mapema kupitisha mfumo huo wa uendeshaji wa timu, basi ningetoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya usajili.
“Lakini kutokana na kuchelewa kwao wakati zimebaki siku sita kabla ya usajili kufungwa, nimeona niwapatie shilingi milioni 100 kwa ajili ya usajili, fedha hizo nimechangia kama mwanachama wa kawaida tu.
“Pia nimepanga kutafuta maskauti wanne watakaozunguka Afrika nzima kwa ajili ya kutafuta wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuichezea Simba kama wakimaliza mchakato huo wa mfumo wa uendeshaji wa klabu yetu na kunikabidhi timu ndani ya miezi mitatu.
“Sh bilioni 20 kwa mfanyabiashara si kidogo, hata baba yangu ameshangaa, unajua yeye ni mfanyabiashara na anajiuliza fedha zote hizi naziingiza Simba? alisema Mo na kuongeza. “Lakini mimi nasisitiza, haya ni mapenzi.”
Kwa upande wa Aveva alisema kuwa, wanamshukuru Mo kwa mchango huo alioutoa, wenye malengo ya kuitengeneza Simba yenye mafanikio.
Aveva alisema fedha hizo walizozipata zitatumika kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji mmoja Muivory Coast, Fedric Blagnon anayehitaji zaidi ya shilingi milioni 100.
“Hizi fedha tulizokabidhiwa leo (jana) na Mo, tumepanga kuzitumia kwa ajili ya wachezaji na mchezaji tunayeanza naye ni Muivory Coast (Blagnon) ambaye anahitaji zaidi ya shilingi milioni 100, tunatoa nafasi kwa wanachama wengine kujitokeza kuichangia Simba.
“Pia niwaambie tu kuwa uongozi wangu umepanga kuanza haraka mchakato wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu kuhakikisha ninafanikisha hilo,” alisema Aveva.

No comments