Header Ads

MOYO ULIOUMIZWA- 06


MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
Mapenzi yaliutesa moyo wa David, hakutaka kumuacha msichana Melisa kwani kila siku aliamini kwamba kuna siku msichana huyo angekuja na kuwa wake kabisa. Hakuacha kumsumbua, kila siku ilikuwa ni lazima kumtafuta na kumwambia jinsi alivyokuwa akimpenda, kwamba hakuwa akilala kwa ajili yake, hivyo alitaka awe mpenzi wake lakini msichana huyo alimkataa.
Moyo wake uliumia, kila aliposimama na msichana huyo, hisia zake zilihama kabisa, kuna wakati alijiona akiwa sehemu na msichana huyo, sehemu yenye raha kwa wapendanao kama visiwani Hawaii nchini Marekani, wakiponda raha lakini kila alipomtaka msichana huyo kuwa naye, alimkataa, tena kwa sauti ya upole kabisa.
David alijitahidi, alipoona ameshindwa kabisa, wazo alilokuja nalo kichwani lilikuwa ni kumfuatilia msichana huyo mpaka nyumbani kwao. Hakukuwa na la kujishauri, alichokifanya ni kwenda huko kwa ajili ya kukutana naye, amwambie kilekile alichokuwa akimwambia kila siku kwani moyo wake ulimwambia kwamba angefanikiwa, kama kulikuwa na wanaume waliokuwa wakiwafuatilia wasichana kwa miaka miwili, walikataliwa na mwishoni kukubaliwa, ingekuwaje kwake na wakati ndiyo kwanza ilikuwa miezi miwili.
Alipofika nyumbani kwa msichana huyo, macho yake yakatua kwa Melisa, alipomuona tu, moyo wake ukafarijika, akahisi akiwa katika ulimwengu mwingine kabisa, akahisi kukutana na mtu aliyekuwa na sura nzuri, mwenye mvuto kuliko wasichana wote katika dunia hii.
Melisa alipomuona, harakaharaka akasimama na kumfuata David, alipomkaribia, akamshika mkono na kumvuta pembeni. Kwa kumwangalia msichana huyo, alikasirika, hakutaka David afike nyumbani hapo kitu kilichomfanya kijana huyo kuumia mno.
“Umefuata nini?” aliuliza Melisa huku akimwangalia David usoni, alikunja ndita, ilionyesha ni jinsi gani alikuwa amekasirika.
“Hilo ni swali tena Melisa? Si nimekufuata wewe!” alijibu David huku akiachia tabasamu pana alilokuwa akilitumia kuwapagawisha wasichana wengine, ila kwa Melisa, tabasamu lile lilionekana kuwa chukizo.
“Hivi kwa nini hunielewi Davy?”
“Melisa! Najua hunipendi, najua unanichukia mno, ila sidhani kama chuki zako zinaweza kunifanya niachane na wewe,” alisema David.
“Nisikilize vizuri! Mimi nina mpenzi wangu! Naomba uniache,” alisema Melisa.
“Melisa! Nimeshindwa kukuacha. Umenidhalilisha vya kutosha, kama ingekuwa ni kukuacha, ningekuacha kitambo sana. Ninashindwa kabisa, kila ninapokuangalia, ninamuona msichana mwenye ndoto za kuishi nami siku moja,” alisema David.
“Kuishi na wewe! Nimekuwa chizi! David, naomba uondoke hata kabla baba hajatoka,” alisema msichana huyo. Hasira za waziwazi ziliendelea kuonekana usoni mwake.
“Kwa hiyo?”
“Kuhusu nini?”
“Unanipenda? Upo tayari kuwa nami?”
“Hivi wewe David nifanye nini ili unielewe?”
“Nipende! Just love me like the way I do,” (nipende kama ninavyofanya)
“Immposible.” (Haiwezekani)
“Lakini Melisa....”
“Kwenye hili hakuna lakini! Naomba uondoke!”
“Kweli unanifukuza?”
“Ndiyo nakufukuza! Naomba uondoke! Au unataka nikuitie mbwa?”
“Hapana! Basi sawa. Haina noma, ila nitakupenda maisha yangu yote,” alisema David huku akimwangalia msichana huyo.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kukataliwa, alikataliwa mara nyingi mpaka akazoea, kuna kipindi alikuwa akimfuata msichana huyo huku akiwa na uhakika wa kukataliwa kwa asilimia nyingi lakini hakurudi nyuma.
Siku zikaendelea kukatika, hakutaka kuzificha hisia zake, alichokifanya ni kuwaambia wazazi wake. Hakutaka kujali wangesemaje au wangemuonaje, alichokitaka ni kuwaambia ili kama kuna msaada wowote wangeweza kumpa, basi wampe.
Wazazi hao wakamshangaa, hawakutaka kumuona kijana wao akiingia kwenye maisha ya uhusiano wa kimapenzi, walimtaka asome ili baadaye aje kuwa na maisha mazuri, waliamini kwamba mara atakapoingia kwenye mapenza angechanganyikiwa, mapenzi yangemuumiza na hatimaye kufanya vibaya katika maomo yake.
“Ila nimehitaji ushauri! Kama kusoma nitaendelea kusoma, mnanilalamikia ili iweje?” aliuliza David huku akiwaangalia wazazi wake ambapo baada ya kuwashirikisha tu, wote wakaonekana kumkasirikia.
“Tena achana na hiyo tabia David. Angalia maisha yetu, angalia jinsi tulivyo masikini, badala ya kusoma ili mwisho wa siku utusaidie katika maisha yetu, unatuletea habari za mapenzi, tena na mtoto yule wa Mzungu!” alisema mama yake huku akionekana kukasirika.
David hakutaka kubaki mahali hapo, alikasirika kwani alitamani kila mtu atakayemwambia kuhusu Melisa basi amuunge mkono na kumpa kile alichokuwa akikihitaji.
Wazazi wake walikuwa masikini, baba yake alikuwa mkulima na mama yake alikuwa muuza pombe za kienyeji. Walikuwa wakiishi kwenye maisha magumu mno, kila siku maisha yao yalitawaliwa na umasikini mkubwa, walipambana kwa nguvu zote kutoka katika maisha waliyokuwa nayo na kumsomesha David kwa kuamini angewasaidia hapo baadaye.
Japokuwa alikuwa akiteswa katika mapenzi, lakini kwa upande wa darasani, David ndiye alikuwa kichwa chao. Hakuwa msomaji, alipenda sana kusikiliza muziki na hata kutembea huku na huko ila kitu cha ajabu kabisa, darasani alikuwa moto. Kwa kifupi alikuwa genius.
Mbali na sura yake nzuri, hilo likawafanya wasichana wengi kumtetemekea lakini kitu cha ajabu kabisa moyo wake haukuwa kwa msichana mwingine zaidi ya Melisa ambaye wala hakuwa na habari naye.
Aliwakataa wasichana wengi kwa sababu ya Melisa, wakati mwingine alipofuatwa na wasichana hao aliwaambia kwamba alikuwa na mpenzi wake aitwaye Melisa hivyo asisumbuliwe.
Kauli hiyo iliwaumiza wasichana wengi kwani miongoni mwa wanaume waliokuwa na sura nzuri hapo Marangu, David alikuwa namba moja, si wasichana wa Marangu tu, wengine kutoka Machame, Kahe na sehemu nyingine waliposikia kuhusu David, walifika Marangu kwa ajili ya kumuona huyo David.
“Ipo siku tu huyu Melisa atanikubali! Hapo ndipo nitakapouonyeshea ulimwengu kwamba nina uwezo mkubwa wa kumfurahisha msichana kuliko mwanaume yeyote yule.
****
“Ngo! Ngo! Ngo!” ulisikika mlango ukigongwa huku ikiwa ni saa nane usiku.
Msichana wa kazi alikuwa amesimama mbele ya mlango wa chumba cha mzee Kimbonaga, baba yake Melisa. Hakuwa na nguo yoyote mwilini zaidi ya khanga aliyokuwa ameivaa kwa mtindo wa lubega. Hakuishia kugonga tu bali kadiri alivyokuwa akigonga ndivyo alivyokuwa akimtaka mzee huyo aufungue mlango haraka iwezekanavyo.
Baada ya dakika moja, mlango ukafunguliwa na mzee huyo aliyekuwa amevaa pensi, alipomuona msichana huyo, alishangaa kwani haikuwahi kutokea akaja kugonga mlango muda kama huo.
“Kuna nini Sofia?”
“Melisa ameanza tena...” alijibu msichana huyo.
Mzee Kimbonaga aliposikia hivyo, harakaharaka akachomoka kutoka hapo alipokuwa na kwenda chumbani kwa binti yake, alipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwasha taa na macho yake kutua kwa binti yake aliyekuwa kitandani.
Melisa alibadilika, mwili wake ulivimba mno, alikuwa akitetemeka pale kitandani huku hata kupumua kwake kukiwa kwa shida sana. Muda wote alikuwa akitoa sauti nzito, kama mtu aliyekuwa akikoroma kwa sauti kubwa.
Mzee Kimbonaga alivyoona binti yake yupo kwenye hali hiyo, akamfuata na kupiga magoti. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuweka vizuri kitandani pale. Hakujua afanye nini kwani mara zote hali kama hiyo ilipokuwa ikimtokea, daktari wake alikuwa mahali hapo.
“Mpige simu daktari...” alisema mzee Kimbonaga kwa sauti huku akionekana kuchanganyikiwa.
Mfanyakazi yule akaelekea chumbani kwa mzee Kimbonaga kisha kuchukua simu yake. Akaanza kulitafuta jina la daktari huyo, alipoliona, akampigia, simu ikaanza kuita, iliita na kukata, akapiga tena, ikapokelewa.
“Melisa amerudi vilevile, amevimba kitandani...” alisema msichana huyo, tayari mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakimtiririka.
“Mpelekeni hospitali! Nitawakuta huko!” ilisikika sauti ya daktari na hivyo mfanyakazi kumrudia mzee Kimbonaga na kumwambia kile alichoambiwa na daktari huyo.
Hakukuwa na kitu cha kusubiri, alichokifanya ni kumbeba binti yake, akaondoka naye mpaka nje ambapo akampakiza ndani ya gari, mfanyakazi naye akaingia na kisha kumwambia mlinzi afungue geti.
“Fungua geti...” alimwambia mlinzi kwa sauti.
Mlinzi akafungua harakaharaka na kisha mzee huyo kuliwasha gari na kuondoka nyumbani hapo kuelekea hospitalini. Njiani, ndani ya gari bado Melisa alikuwa akikoroma tu, mwili wake ulizidi kuvimba na kuwa wa moto sana, macho yake yaligeuka na kwa jinsi alivyoonekana, ilikuwa rahisi kusema kwamba msichana huyo alikuwa kwenye hatua za mwisho kuvuta pumzi ya dunia hii.
Hawakuchukua muda mrefu, wakafika katika hospitali hiyo. Ilikuwa kimya, alichokifanya mzee Kimbonaga ni kwenda ndani, akachukua machela na kisha kutoka nayo, akampakiza Melisa na kuanza kuisukuma kuelekea ndani ambapo wakawakuta manesi wakiwa wamelala.
“Jamani! Nini tena?” aliuliza nesi mmoja.
“Kama siku nyingine!” alijibu mzee Kimbonaga.
Wakamchukua na kumpeleka katika chumba cha upasuaji ambapo huko kama kawaida ilikuwa ni lazima ahudumiwe na daktari ambaye kwa muda huo alikuwa amelala katika ofisi yake. Nesi mmoja akamfuata daktari huyo na kumwambia kuhusu Melisa.
“Jamani! Huyu binti atakuja kufa sasa! Kwa nini wazazi wasichukue hatua zaidi?” alijiuliza daktari huyo huku akivalia koti lake kubwa na kwenda kule alipolazwa Melisa. Alipofika tu, yeye mwenyewe alishangaa, siku hiyo mwili wa Melisa ulivimba sana tofauti na siku nyingine.
“Mungu wangu!” alijikuta akisema daktari, japokuwa Melisa alikuwa binti mwembamba, ila hapo kitandani alionekana mnene sana. Ugonjwa aliokuwa akiumwa, ulikuwa ukimtesa tangu alipozaliwa.
Je, nini kitaendelea?
Je, ni ugonjwa gani unaomsumbua Melisa mpaka kutaka kumuua?
Tukutane Ijumaa kwa muendelezo wa hadithi hii
Kwa wanaotaka kuweka oda ya vitabu vya mwandishi huyu ambavyo vinatarajiwa kutolewa mwezi wa 10, wanaweza kuandika namba zao.

No comments