Header Ads

MOYO ULIOUMIZWA- 07


MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
Mzee Andrew alikuwa kwenye majonzi tele, hali ya binti yake ilimuuma mno, alihisi moyo wake umechomwa na kitu chenye ncha kali, maumivu aliyoyapata kipindi hicho hayakuweza kusimulika.
Pale benchini alipokuwa, aliikutanisha mikono yake na kuanza kumuomba Mungu. Alijua kwamba hakukuwa na daktari ambaye angeweza kumponya binti yake zaidi ya yeye hivyo kitu pekee alichokuwa akikifanya ni kumuomba Mungu tu.
Mlango wa chumba cha upasuaji haukufunguliwa, daktari alikuwa humo huku akimshughulikia Melisa ambaye alikuwa kwenye hali mbaya, mwili wake ulivimba sana kiasi kwamba hata kama mtu angesema msichana huyo alikuwa mwembamba, lazima angebishiwa.
“Mungu! Naomba umsaidie binti yangu,” alisema mzee Andrew na machozi kuanza kutiririka mashavuni mwake.
Dakika zilizidi kusonga mbele, ilikuwa ni usiku wa manane lakini mzee huyo hakutaka kuondoka kurudi nyumbani, hakulala pale benchini, alichokuwa akihitaji kujua ni hali ya binti yake, ingeendelea vipi? Angekufa kama wengine au angekuwa hai.
Ilipofika saa kumi alfajiri, mlango ukafunguliwa na daktari kutoka ndani ya chumba kile. Harakaharaka mzee Andrew akasimama na kuanza kumfuata daktari huyo. Kwa muonekano aliouonyesha daktari, alionekana kutokuwa sawa kabisa, alionekana kuwa na majonzi tele, uso wake ulionyesha kwamba kile kilichokuwa kimetokea chumbani, hakikuwa kizuri.
“Kuna nini daktari? Binti yangu amekufa?” aliuliza mzee huyo huku akimwangalia dokta.
“Naomba twende ofisini!”
“Niambie kwanza, naomba uniambie!”
“Nitakwambia, twende ofisini tu.”
Wakaondoka na kuelekea ofisini, muda wote mzee Andrew alionekana kuwa na huzuni kubwa moyoni mwake, alikuwa mnyonge kiasi kwamba aliiona dunia nzima ikiwa imemuelemea.
Walipofika ofisini, wakaingia na kutulia kitini. Bado mzee huyo alikuwa na hofu tele moyoni mwake, aliisikia sauti ikimwambia kwamba binti yake alikuwa amefariki na daktari hakutaka kumwambia ukweli akiwa mbele ya chumba kile na ndiyo maana akamuita kuelekea mbali kabisa ili mwili wa binti yake utolewe na kupelekwa mochwari.
“Niambie nini kinaendelea!”
“Hali ya binti yako ni mbaya sana! Sasa hivi hali imekuja kwa kasi kubwa tofauti na tulivyozoea, kinachotakiwa hapa ni lazima asafirishwe na kupelekwa katika hospitali ya Muhimbili!” alisema daktari huyo.
“Kufanya nini? Matibabu mpaka huko?”
“Ndiyo! Ila cha muhimu kabisa ni kwamba lazima binti yako apandikizwe figo nyingine. Zile zilizokuwepo hazifanyi kazi vizuri, ni lazima itafutwe figo nyingine na kuwekewa yeye, vinginevyo, binti yako atakufa ndani ya mwezi mmoja tu,” alisema daktari huyo huku akimwangalia mzee huyo kwa macho yaliyoonyesha kumaanisha kile alichokisema.
“Atakufa?”
“Kama jambo hili halitofanyika ndani ya mwezi mmoja!”
Mzee Andrew alishtuka, hakutaka kuchelewa, hapohapo akampigia simu mwanamke aliyezaa naye, Kattie aliyekuwa akiishi nchini Marekani. Simu wala haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya mwanamke huyo kusikika.
“I will be there by tomorrow,” (nitakuwa huko kesho) alisikika kwenye simu.
Mara baada ya kuzungumza, wakatoka ndani ya chumba kile na kuelekea katika chumba cha upasuaji alichokuwa Melisa. Kule hakuwepo, alikuwa amekwishatolewa na kupelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi na kupumzika huko.
Mzee Andrew akapelekwa huko, alipofika, kitendo cha kumuona binti yake kitandani pale huku akiwa hajitambui, moyo wake ulimuuma mno na machozi yaliyokuwa yakimtiririka mashavuni mwake yakaongezeka.
Akapiga hatua kumsogelea, alipomkaribia, akaupeleka mkono wake shavuni mwa binti yake na kuanza kuongea maneno ambayo aliamini kwamba Melisa alikuwa akiyasikia maneno hayo.
“Binti yangu naomba usiniache, nitaumia, naomba urudi tena! Ninaumia moyoni kukuona ukiwa hivi Melisa, please come back to the world,” alisema mzee Andrew huku machozi yakiendelea kumtiririka mashavuni mwake, maumivu aliyoyasikia hayakusimulika.
Alilia sana, alihuzunika lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika, binti yake aliyempenda, Melisa alikuwa kimya kitandani pale huku akipumua kwa kutumia mashine ya oksijeni. Aliendelea kukaa pembeni ya kitanda chake mpaka ilipofika asubuhi ambapo ndege ikaandaliwa na hivyo kutakiwa kusafirishwa na kupelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Ndani ya ndege, bado mawazo yake yalikuwa kwa binti yake. Alikuwa na fedha nyingi alizokuwa akizipata kutoka katika mgodi wake mmoja uliokuwa Mererani, mbali na hiyo bado mkewe alikuwa akituma fedha kutoka nchini Marekani kila mwezi kwa ajili ya binti yake.
Alikuwa tajiri kiasi cha kuweza kuchukua ndege yote yeye na binti yake tu. Hawakuchukua saa nyingi angani, wakafika jijini Dar es Salaam ambapo tayari kulikuwa na gari la wagonjwa kutoka Muhimbili lilifika mahali hapo kwa ajili ya kumchukua msichana huyo.
“Yupo kwenye hali mbaya sana,” alisema daktari mmoja huku akimwangalia Melisa aliyekuwa kitandani.
Wakampakiza Melisa ndani ya gari na safari ya kuelekea hospitalini ikaanza mara moja. Muda wote wa safari kutoka Kilimanjaro mpaka Dar es Salaam, uwanja wa ndege mpaka hospitali, mzee Andrew alikuwa pembeni ya binti yake, hakutaka kumuacha, kazi yake ilikuwa ni kutulia pembeni yake na kuzungumza maneno yaliyomtaka Melisa aamke na kumwangalia tena.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hospitali hiyo ambapo moja kwa moja akateremshwa na kuanza kupelekwa ndani ya chumba cha mapumziko kwani kitu ambacho madaktari walitaka kukifanya ni kusoma ripoti ya mgonjwa kutoka katika hospitali aliyotoka ili kujua ni kitu gani kilikuwa kikimsumbua.
Baada ya dakika ishirini, jopo la madaktari wakakutana ndani ya chumba kidogo cha mkutano, walikuwa madaktari wanne ambao baada ya kuipitia ripoti hiyo, ilionyesha ni lazima mgonjwa huyo apandikizwe figo nyingine kwani vinginevyo angekufa kutokana na figo zote mbili kuharibika.
“Ripoti inasema huyu binti ana mwezi mmoja wa kuishi kama tu figo nyingine isipopandikizwa kwake,” alisema Dk. Malik.
“Ndiyo! Kwa hiyo tufanyeje?”
“Tutangaze kama kuna mtu anahitaji kutoa figo yake kumsaidia huyu binti!”
“Ila watakubali kweli?”
“Tujaribu!”
Kabla ya kufanya hivyo wakajadiliana na mzee Andrew ambaye bila kipingamizi, akakubali kwamba kama kungetokea mtu atakayekuwa tayari basi angetoa kiasi cha shilingi milioni ishirini.
Tangazo likawekwa. Kipindi hicho kilikuwa kabla ya serikali haijapiga marufuku juu ya watu kutangaza kuhitaji figo au ini. Matangazo yakawekwa kila kona, watu waliposikia kwamba mtu aliyekuwa akihitaji figo aliweka mezani kiasi cha shilingi milioni ishirini, wengi wakajitokeza.
“Baba! Ninakufa baba!” alisema Melisa huku akimwangalia baba yake, bado mwili wake ulivimba, mzee Andrew akabaki akimwangalia binti yake huku machozi yakianza kumtiririka mashavuni mwake, yeye mwenyewe aliumizwa na kile alichokuwa akikizungumza binti yake.
“Huwezi kufa binti yangu! Huwezi kufa!”
“Baba! Nimekuwa kwenye hali mbaya mno, mwili unawaka moto! Baba! Ninakufa!” alisema Melisa.
Mwili wake ulizidi kuvimba, madaktari na watu wengine waliokuwa wakiingia ndani na kumwangalia walimshangaa, alionekana kuwa binti mdogo lakini kwa jinsi mwili wake ulivyokuwa umevimba, ilimshangaza kila mmoja.
Watu waliendelea kukusanyika hospitalini hapo, kabla ya kutolewa figo ilikuwa ni lazima madaktari waangalie vinasaba vyao kama vilifanana na vya Melisa. Kazi hiyo ikafanyika na baada ya watu 205 kupimwa, ni wawili tu ndiyo ambao vinasaba vyao vilifanana na vya Melisa.
“Asante Mungu! Kwa hiyo upasuaji utafanyika lini?” aliuliza mzee Andrew.
“Hata kesho! Ila kuna kitu nataka tuzungumze!”
“Kitu gani?”
“Njoo ofisini kwangu!”
Mzee Andrew alionekana kuogopa, kitendo cha kuitwa ndani ya ofisi ya daktari hakikuwa kitu kizuri hata kidogo, moyo wake ulikuwa na hofu kubwa, baada ya kuingia ndani ya ofisi hiyo wakatulia kwenye viti na kuanza kuzungumza.
“Tumempima binti yako, hakika tumefanikiwa kupata watu wawili wenye vinasaba...” alisema daktari.
“Basi fanyeni upasuaji!”
“Hapana! Tatizo tuliloliona ni kwamba watu hao wawili, mmoja anaugua UKIMWI na mwingine ana kansa ya damu na walikuwa wakihitaji kiasi hicho kwa ajili ya kuwasaidia. Ni vigumu sana sisi kama madaktari kukubali,” alisema daktari huyo.
“Mmh!”
“Ndiyo hivyo! Kama inashindikana basi jua kwamba hakuna aliyepatikana ambaye ana vinasaba vinavyofanana na binti yako!” alisema daktari.
****
Taarifa za kuugua kwa Melisa zilifika shuleni asubuhi. Mtu wa kwanza kuzisikia alikuwa rafiki yake kipenzi, Manka. Zilikuwa taarifa zilizomshtua kila mmoja, hakukuwa na aliyeamini kwamba msichana huyo mrembo alikuwa akiumwa vibaya namna hiyo.
Wengi walihisi kwamba hizo zilikuwa siku za mwisho za msichana huyo kwani kitendo cha mwili wake kuvimba kuliko siku nyingine ilionyesha ni jinsi gani siku hizo zilihesabika.
Shuleni kukawa na majonzi, wavulana wengi waliumia kwa kuwa walimpenda msichana huyo mcheshi, mzuri ambaye alikuwa mzungumzaji na kila mtu na wala hakujali ni uzuri kiasi gani alikuwa nao.
Taarifa hizo zilipomfikia David, kwanza hakuamini, alimuuliza mara mbilimbili mtu aliyemwambia hivyo lakini mtu huyo majibu yake yalikuwa yaleyale kwamba Melisa alikuwa kwenye hali mbaya.
Hakukuwa na mtu aliyejua sababu ya msichana huyo kuwa namna hiyo hivyo yeye kama yeye akafuatilia mpaka nyumbani kwa msichana huyo, alipomkuta mfanyakazi, akamwambia ukweli kwamba Melisa alikuwa akihitaji figo na kama asipopata figo basi angefariki dunia.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo!”
“Baba yake yupo wapi?”
“Wamekwenda Dar wote wawili!”
David alisikia moyo wake ukiwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile alichokisikia kwamba kama msichana aliyekuwa akimpenda asipopata figo nyingine basi angeweza kufariki dunia.
Akarudi nyumbani huku akiwa na mawazo tele, siku hiyo hakula, alijifungia chumbani kwake huku akimuomba Mungu amuwezeshe Melisa kupata figo.
Siku hiyo ikakatika, siku ya pili ikaingia na kukatika, ilipofika siku ya tatu akarudi tena nyumbani kwa kina Melisa na kuulizia hali yake, akaambiwa kwamba watu walipatikana ila hakukuwa na mtu ambaye vinasaba vyake vilifanana na msichana huyo.
“Haiwezekani! Yaani watu mia mbili wote havifanani?” aliuliza David.
“Ndiyo hivyo!”
“Ila nahisi vyangu vinafanana na vyake, naamini hilo,” alisema David.
“Umepima?”
“Hapana!”
“Sasa kwa nini uamini hivyo?”
“Sijajua kwa nini! Ila nahisi vinafanana!”
Alichokifanya David ni kutaka kuwasiliana na mzee Andrew ambaye akapigiwa simu na mfanyakazi na kisha kupewa simu David na kuanza kuzungumza naye. Kwanza kitu cha kwanza alimwambia mzee huyo alivyokuwa akimpenda Melisa lakini la pili la msingi kabisa ilikuwa ni kumueleza dhamuni lake la kutaka kutoa figo yake.
“Sasa vinasaba vinafanana kweli?” aliuliza mzee huyo.
“Ndiyo jambo la kupima, visipofanana, basi sawa, ila vikifanana, naomba nimtolee figo yangu moja,” alisema David.
“Utahitaji kiasi gani?”
“Bure kabisa. Kwa ajili ya Melisa, sihitaji chochote kile,” alijibu David.
Alichokifanya mzee Andrew ni kumkatika tiketi ya ndege na siku hiyohiyo David akatoroka kwao na kwenda Dar es Salaam. Ndani ya ndege alikuwa na mawazo tele, kichwa chake kilimfikiria Melisa na aliona akiwa na kila sababu ya kumsaidia msichana huyo kwa kuamini kwamba hapo ndipo angejua kwamba alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
Mara baada ya kufika Dar es Salaam, akapokelewa na mzee huyo na kupelekwa katika hoteli moja ya kifahari na kutulia huko. Moyo wake kwa kipindi hicho ulikuwa ni kutaka kumuona msichana huyo tu na si kingine.
Asubuhi ilipofika, safari ya kuelekea hospitalini ikaanza. Hawakuchukua muda mrefu wakafika huko ambapo wakaelekea mpaka katika chumba alicholazwa Melisa, walipoingia tu, macho ya David yakagongana na ya msichana huyo, kwa jinsi alivyokuwa kitandani pale, machozi yakaanza kumtiririka.
“Pole sana Melisa,” alisema David huku akimwangalia msichana huyo.
“Umekuja kufanya nini David?” aliuliza Melisa.
“Nimekuja kukusaidia Melisa. Nilikwambia kwamba nakupenda, upendo wangu si kitu kama nitakuacha katika hali uliyokuwa nayo. Moyo wangu haujakamilika pasipo kukusaidia, kwanza nataka nikusaidie, nata uwe katika hali yako ya kawaida,” alisema David huku akiwa amemuinamia msichana huyo kitandani, hata machozi yaliyokuwa yakimtoka, yalimdondokea Melisa.
“David nakuo...” alisema Melisa.
“Huwezi kunizuia katika hili Melisa. Nimedhamiria kuukusaidia, ninahitaji kukuona ukisimama tena,” alisema David.
Alibaki akizungumza na Melisa mpaka madaktari walipomuhitaji ambapo akachukuliwa na kwenda kwenye chumba cha vipimo, huko, akafanyiwa vipimo vya kuangalia vinasaba vyake, kitu kilichomfurahisha kila mtu ni kwamba vinasaba vyake vilifanana na vya Melisa.
“Unasemaje daktari?”
“Vinasaba vya David vinafanana na vya binti yako!” alijibu daktari huku akionyesha sura iliyojaa tabasamu pana.
Je, nini kitaendelea?
Je David atafanikiwa kutoa figo yake?
Vipi kuhusu wazazi wake?
Je, kwa nini mpaka siku hiyo bi Kattie hajafika nchini Tanzania?
Tukutane Jumatatu mahali hapa.
Hairuhusiwi kukopi hadithi za page hii na kuziweka sehemu yoyote ile iwe humu Facebook au WhatsApp. ZIpo chini ya Global Publishers na hatua kali za kisheria zitachukuliwa mara moja kwa mtu atakayefanya hivyo.

No comments