Header Ads

MOYO ULIOUMIZWA-2
ILIPOISHIA

Melisa hakutaka kubaki kitini, hapohapo akasimama na kuanza kuondoka huku akimchukua mbwa wake aliyempa jina la Bobby. Mwandishi yule alibaki akimwangalia Melisa, hakuamini kama kweli kile kilichokuwa kikitokea, kilimtokea msichana huyo.
Aliwaona wanawake wengi wakifanya mapenzi na mbwa, hao walikuwa kwenye filamu za kikubwa, walifanya hivyo kwa kuwa walihitaji fedha, sasa ilikuwaje kwa Melisa aamue kufanya kitu kama hicho? Kama ni fedha, alikuwa nazo, sasa kwa nini aolewe na mbwa?
Hilo lilikuwa swali lisilokuwa na majibu.

SONGA NAYO

Wanawake waliona kama wamedhalilishwa, kile kilichokuwa kimetokea kiliwakera sana, wengi wakataka kuandamana na kumtaka Melisa aachane na mbwa wake na atafute mwanaume wa kumuoa kwani kulikuwa na wanaume wengi waliokuwa wakimpenda.
Hawakuishia kwa maneno tu bali wakapanga kuingia mitaani, kuandamana mpaka kuhakikisha msichana huyo anaachana na mbwa wake na kuolewa na mwanaume mwingine. Wakaanza kutafuta vibali vya kuwaruhusu kuandamana, walipovipata, wakaingia mitaani.
Ni kama walikuwa wameambiana, wanawake kutoka New York, Los Angeles, Miami, New Orleans, Texas, Washington DC na sehemu nyingine wakaingia mitaani huku wakiwa na mabango yao makubwa yaliyomtaka Melisa aachane na mbwa wake na hatimaye aolewe na mwanaume.
“Haiwezekani...ni lazima aachane na huyo mbwa,” alisema msichana mmoja huku akilishikilia bango lake vizuri, tena alisimama mstari wa mbele kabisa.
Maandamano hayo yakawa stori nyingine, hakukuwa na mtu aliyetamani kuona msichana Melisa akiwa na mbwa yule. Wengine wakatamani kwenda mpaka nyumbani kwake na kuzungumza naye, walijua kwamba kulikuwa na kitu kilichoendelea kwani ilikuwa vigumu kwa mtu mwenye pesa, umaarufu wa kutosha kufunga ndoa na mbwa.
Baada ya siku kadhaa kupita ndipo waandishi wa habari wa Gazeti la New York Times wakaanza kufuatilia maisha ya Melisa tangu alipokuwa akisoma kwa kuamini kwamba huko ndipo kulipokuwa na mzizi wa kile alichokiamua Melisa.
Taarifa za awali zilisema kwamba Melisa alikuwa akisoma katika Chuo cha Havard nchini Marekani katika Jiji la Boston. Wakaelekea huko ambapo wakakutana na maprofesa wa chuo hicho ambao walikiri kumfahamu msichana huyo, ili kujua mambo mengi alitakiwa kutafutwa msichana mmoja aliyeitwa Catherine Born, msichana raia wa Ujerumani ndiye alikuwa swahiba wake mkubwa.
Hilo halikuwa tatizo, walichokifanya ni kuanza kumtafuta msichana huyo, walikuwa na kiu ya kutaka kujua maisha ya Melisa huko nyuma yalikuwaje kwani kile alichokuwa amekifanya, hakikuwa uamuzi wa haraka au bila sababu, kulikuwa na kitu nyuma ya pazia, walitaka kujua kitu hicho kilikuwa nini na kwa jinsi gani wangeweza kumsaidia msichana huyo mrembo.
“Alikuwa akiishi hapa miaka mitatu iliyopita lakini aliondoka kwenda Ujerumani, ila tumemuona kwenye vyombo vya habari kwamba kwa sasa hivi ni mwanamitindo katika kampuni moja iitwayo Sophia Designing And Modeling,” alijibu mwanamke aliyekuwa akimiliki apantimenti moja iliyokuwa New York.
“Sehemu gani?”
“Berlin.”
Hilo halikuwa tatizo, walichokuwa wakikitaka ni kupata ukweli juu ya kile walichotaka kukisikia. Japokuwa huko kulikuwa na waandishi lakini wakaamua kuwatuma waandishi wao kutoka nchini Marekani, msichana aliyeitwa Claire Shawn na mwanaume aliyeitwa Brian Powell.
Walipofika nchini Ujerumani, wakachukua vyumba katika Hoteli kubwa ya Casanova na kisha kutulia hapo mpaka siku inayofuata ambapo walipanga kwenda kumuona msichana huyo mahali walipoelekezwa.
Kila mmoja alikuwa na hamu ya kusikia kile kilichotokea katika maisha ya chuo ya msichana huyo. Mwenyewe hakuwa radhi kabisa kuzungumzia kitu kilichokuwa kimetokea huko nyuma na ndiyo maana waliamua kumtafuta Christina na kuujua ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
Usiku wa siku hiyo wakalala na siku iliyofuatia wakaanza kumfuata msichana huyo katika jengo kubwa la kampuni ya mitindo ya Sophia Designing And Modeling. Walipofika huko, hilo halikuwa tatizo lolote, wakamuona msichana huyo.
Kwanza Catherine akaogopa, hakuamini kama waandishi walitoka nchini Marekani na kwenda kumuona yeye, hakujua ni kitu gani kilitokea kwani haikuwa kawaida yeye kufuatwa na waandishi wa habari ambao walitaka kuzungumza naye.
Alichokifanya ni kwenda kuwasikiliza. Wakaelekea katika mgahawa mmoja na kisha kutulia hapo na kuanza kumuuliza maswali juu ya kile walichotaka kumuuliza.
“Unamkumbuka Melisa?” aliuliza Claire.
“Melisa bilionea, ni rafiki yangu mkubwa sana, ninamfahamu! Mmekuja kuniuliza kuhusu suala lake la kuolewa na mbwa?’ aliuliza Claire huku akiwaangalia.
“Ndiyo! Tunajua kwamba ulisoma naye kitambo na hata uamuzi wake wa kuolewa na mbwa inawezekana unatokana na historia yake kipindi alichokuwa akiishi chuo. Tumekuja kupata mawili matatu juu ya hilo,” alisema Claire.
“Mimi mbona sijui kitu.”
“Utakuwa unajua tu Cathy! Naomba utuambie. Jua tumetoka Marekani mpaka hapa Ujerumani kwa ajili ya hili tu, naomba utuambie japo kwa kifupi,” alisema Brian.
“Ili iweje?”
“Tupate kujua tu.”
“Ila suala la kuolewa na mbwa ni lake, nyie mnalitakia nini?”
“Yeye ni staa, ni bilionea pia nahisi si vibaya kama tukijua kilichotokea,” alisema Claire.
“Sawa ila sidhani kama mimi ni mtu sahihi wa kuwaambia chochote kile,” alisema Catherine.
“Catherine! Tunahitaji utusaidie.”
“Haiwezekani!” alijibu msichana huyo.
Ni kweli aliamua, hakutaka kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea huko nyuma, alipanga kunyamaza kwani ni kama kulikuwa na makubaliano baina yao juu ya kutaka kuficha suala hilo. Claire na Brian walimbembeleza mno, walitaka kujua kile kilichotokea mpaka kuchukua uamuzi huo.
“Sawa. Nimekubali,” alisema Catherine lakini hata kabla hajaanza kuwaambia kilichotokea, simu yake ikaanza kuita, alipoangalia kwenye kioo, mpigaji alikuwa Melisa. Harakaharaka akaipeleka simu sikioni.
“Usimwambie mtu kitu chochote kilichotokea,” aliisikia sauti ya msichana Melisa sikioni mwake. Hata kabla hajatoa jibu, simu ikakatwa.
Catherine akashusha pumzi nzito. Alielewa ni jinsi gani msichana huyo hakutaka kuiweka wazi historia ya maisha yake iliyokuwa imetokea. Akayapeleka macho yake nyusoni mwa watu wale waliomfuata, akabadilika.
“Nimekatazwa, siwezi kuzungumza chochote kile,” alisema Catherine.
“Tunakuomba Catherine! Tusaidie.”
“Haiwezekani!” alisema msichana huyo, hapohapo akasimama na kuanza kuondoka mgahawani hapo kitu kilichowaacha hoi waandishi hao.
“Ila ni nini kilitokea? Mbona ishu hii inakuwa ngumu sana?” alijiuliza Claire huku akishusha pumzi nzito.
Wote walichanganyikiwa, waliondoka nchini Marekani na kwenda Ujerumani kwa kuamini kwamba msichana huyo angewaambia kila kitu kilichotokea hivyo kupata stori kubwa ambayo waliamini kwamba ingewavutia watu wengi na hatimaye kutoa habari iliyoshiba.
Hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya, walitamani kurudi nchini Marekani na kuanza kumuomba Melisa awahadithie kile kilichotokea kwani walitumia kiasi kikubwa cha fedha na matokeo yake hawakufanikiwa kupata kile walichotakiwa kupata.
“Kwa hiyo tufanye nini?” aliuliza Claire huku akionekana kutokuelewa ni kitu gani walitakiwa kufanya baada ya hapo.
Hawakuwa na jinsi, waliona kwamba kama wangeendelea kumlazimisha Catherine kuwaambia kilichotokea wasingeweza kufanikiwa. Walichokifanya ni kuingia Google na kisha kuingia katika wikipedia ya msichana Melisa, huko wakaona kwamba msichana huyo alizaliwa Tanzania katika Mkoa uitwao Kilimanjaro, alikulia huko mpaka alipomaliza kidato cha sita ndipo akaondoka na kwenda kusoma masomo ya chuoni katika Chuo cha Havard nchini Marekani.
Wakahisi kwamba huko wangeweza kupata kitu chochote kile, hawakutaka kuchelewa, wakawasiliana na mabosi zao na kuwaambia wazi kila kitu kilichotokea hivyo ilikuwa ni lazima kuondoka kuelekea nchini Tanzania kwa kuona kwamba huko wangeweza kupata kitu chochote ambacho kingekuwa msaada katika maisha yao.
Ofisi ikawaruhusu na kuwapa kiasi kikubwa cha fedha. Ilikuwa ni afadhali kupoteza gharama kubwa ya fedha lakini mwisho wa siku wapate kile walichotakiwa kukipata. Wakaanza kufanya harakati zote za safari, kwa sababu walikuwa wakielekea huko kwa ajili ya kazi, wala hawakupata usumbufu wa kutumiwa vibali na kuanza safari ya kuelekea nchini Tanzania.
Ndege ilichukua saa kumi na sita mpaka kufika nchini Tanzania, ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakateremka na kuelekea nje ya uwanja huo. Hawakutaka kuunganisha safari ya kuelekea Kilimanjaro, kwanza wakaenda hotelini na kutulia huko.
Usiku kucha walikuwa wakifikiria ni kwa jinsi gani wangeweza kufanikiwa katika suala zima la kupata kile kilichokuwa kimetokea nyuma katika maisha ya msichana Melisa. Kila mtu duniani alitaka kusikia kile kilichotokea, hawakuamini kama msichana mrembo na bilionea mkubwa kama alivyokuwa aliamua kuchukua uamuzi huo bila kuwa na sababu, walihisi kwamba nyuma ya kile kilichotokea kulikuwa na mambo mengi.
Siku hiyohiyo wakakata tiketi ya kwenda mkoani Kilimanjaro na asubuhi ilipofika, walikuwa ndani ya ndege hiyo na kuanza safari ya kuelekea huko. Waliamini kwamba kama wangefanikiwa kufika huko salama basi ingekuwa rahisi kwao kupata kile walichokuwa wakikitaka, waliamini hilo kwani kwa miaka yote msichana huyo alivyoishi huko, wangepata chochote kile, hata kama si kitu chote, wangepata hata nusu yake.
Walichukua saa mbili angani ndipo ndege hiyo ikaanza kutua katika Uwanja wa KIA. Ndege iliposimama, wakateremka na kuelekea nje ambapo wakakuta magari mengi ya kukodi na kuchukua moja ambalo liliwapeleka mpaka katika Hoteli ya Lion King iliyokuwa Moshi Mjini.
“Tumefika hatimaye!” alisema Claire.
Wakachukua vyumba na kutulia huko. Walipanga siku inayofuatia ndiyo waanze kazi ya kujua mahali alipokuwa akiishi Melisa hata kabla hajaelekea nchini Marekani. Hawakupajua nyumbani kwao lakini waliamini kwamba kama wangeulizia, lingekuwa jambo jepesi sana kupafahamu alipokuwa akiishi msichana huyo kipindi cha nyuma.
Siku hiyohiyo jioni wakamuuliza mhudumu kama alikuwa akipafahamu alipokuwa akikaa Melisa kipindi cha nyuma. Hilo halikuwa tatizo, kila mtu mkoani Kilimanjaro alifahamu alipokuwa akiishi msichana huyo zamani.
Alichokisema mhudumu yule ni kwamba kesho yake angewapeleka alipokuwa akishi msichana huyo sehemu iitwayo Marangu kama tu wangemuombea ruhusa kwa bosi wake wa hoteli hiyo.
Hilo halikuwa tatizo, Claire na mwenzake wakamuombea ruhusa kijana huyo, tena kwa kulipia dola elfu moja na kisha siku iliyofuata kuanza safari ya kuelekea Marangu huku kila mmoja akiwa na hamu ya kutaka kufahamu kwa kina kile kilichokuwa kimetokea.
Kutokana na ubovu wa barabara, wakachukua saa moja na nusu mpaka kufika huko. Ilikuwa ni kijijini, watu walikuwepo wengi, huku sehemu kubwa ya Marangu ikiwa na mashamba makubwa ya ndizi.
Kulikuwa na hali ya hewa iliyowafurahisha, kulikuwa na baridi ambalo kwa kiasi fulani likawafanya kuona kama walikuwa nchini Marekani. Nyuma nyingi zilikuwa za tepe, walitembea kwa mwendo wa dakika tano huku wakiongea mambo mengi kuhusu msichana Melisa.
Baada ya dakika kadhaa, wakafika katika eneo lililokuwa na nyumba nyingi za tepe, wakaifuata nyumba moja ambayo ilikuwa na mwanamke mzee aliyekuwa amekaa nje huku mbele yake kukiwa na kopo kubwa la kijani lililokuwa na pombe ya kienyeji, wakamsalimia na kisha kutulia.
Kijana yule akaanza kuwatambulisha watu wale kwamba walitoka nchini Marekani ambapo waliamua kufika Marangu kwa sababu walitaka kufahamu mengi kuhusu msichana Melisa, bilionea aliyekuwa akitikisa duniani kwa kipindi hicho.
“Ila si mnemfuata mama yake mmuulize mengi kuhusu yeye!” alisema bibi yule.
“Yeye anaishi wapi?”
“Anaishi Majengo!” alijibu bibi yule.
“Lakini si alikuwa akiishi hapa kabla?”
“Ndiyo! Melisa aliishi hapa kwa miaka mingi tu! Wazazi wake walihamia Majengo baada ya kupata utajiri!” alisema bibi yule.
“Ndiyo tunataka tujue kuhusu maisha yake alipokuwa hapa!”
“Kipi mnataka kukijua?”
“Vyote!”
“Basi wasilianeni na Manka, atakuwa anajua kila kitu.”
“Manka ndiye nani?”
“Msichana fulani alikuwa rafiki yake. Tena mna bahati sana kwani nimesikia aliingia jana kutoka Mjini Dar es Salaam,” alisema bibi yule huku akiachia tabasamu, mapengo yake yakaonekana.
“Anaishi wapi?”
“Nyumbani kwao pale,” aliwaonyeshea nyumba nyingine ya tepe.
Alichokifanya jamaa yule akaelekea katika nyumba hiyo. Nje kulikuwa na watu wengine, alipofika akawasalimia na kisha kumuulizia Manka ambaye akaitwa, yeye mwenyewe alipotoka na macho yake kugongana na macho ya kijana huyo, akashtuka hasa alipoambiwa kwamba Wazungu wale waliokuwa wakionekana walikuwa wageni wake.
“Kuna nini?” aliuliza Manka.
“Sijui! Twende ukazungumze nao.”
Hakuwa na jinsi, akaelekea huko, akakaa chini na kuwasalimia ambapo moja kwa moja akaanza kuzungumza nao. Walimwambia ukweli juu ya kile walichokuwa wakitaka kukisikia kwani walijaribu kwa nguvu zote kumshawishi Melisa awaambie kilichokuwa kimetokea lakini alikataa.
“Mh!” aliguna Manka.
“Inashindikana pia?” aliuliza Claire.
“Hapana ila nashangaa kwa nini alikataa!”
“Hata sisi hatujui!”
“Duh! Kwa hiyo mnataka niwahadithie kila kilichotokea?” aliuliza Manka huku akiwaangalia watu hao, nyuso zao zilionyesha ni jinsi gani walikuwa na hamu ya kusikia kile kilichowatoka Marekani mpaka Tanzania, tena Marangu mkoani Kilimanjaro.
“Itakuwa vizuri zaidi.”
“Sawa. Mataka nianze na nini?”
“Chochote unachokifahamu kuhusu Melisa. Tunajua ulikuwa rafiki yake na ulikuwa ukifahamu mengi sana kuhusu yeye! Tunaomba utuambie kila kitu,” alisema Brian huku akimwangalia Manka usoni.
“Sawa. Nitawahadithia kila kitu, nahisi mtapata kitu ambacho kitakuwa msaada kwenu.”
“Sawa! Tunashukuru!” waliitiki kwa pamoja na kisha msichana Manka kuanza kuhadithia kile kilichokuwa kimetokea miaka mingi iliyopita kati yake na msichana Melisa.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa mahali hapa.

No comments