Header Ads

Mwarabu hatoki leo Taifa lazima ushindi upatikane leo


HAKUNA namna, lazima ushindi upatikane leo ili kufufua matumaini ya Yanga kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha Hans van Der Pluijm ameamua kuchenji gia ili kuhakikisha anapata ushindi kwa namna yoyote ile.
Yanga inaingia kwenye mchezo wa leo wa tano kwao katika Kombe la Shirikisho, ikipambana na Waarabu MO Bejaia kutoka Algeria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar lakini Pluijm ameamua kuwabadilishia kikosi na kutamba kuwa Mwarabu huyo hatoki leo Taifa.
Yanga imepoteza mechi tatu na kutoka sare moja katika hatua hii. Ipo mkiani mwa Kundi A lakini ina nafasi ya kusonga mbele kama itashinda mechi zake mbili zilizobaki huku ikiomba wapinzani wao Bejaia na Medeama ya Ghana wasipate zaidi ya pointi moja katika mechi mbili walizobakiza.

Katika mchezo wa leo, Pluijm amebadilisha safu ya ulinzi wa kati. Amewaondoa mabeki wake wakongwe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani huku akiwapa mikoba Mtogo, Vincent Bossou na Andrew Vincent ‘Dante’.

Pia, safu ya ulinzi wa pembeni inatarajiwa kuwa na mabadiliko katika namba tatu iliyokuwa ikichezwa na Oscar Joshua ambayo leo Haji Mwinyi anatarajiwa kuanza. Utakumbuka katika mchezo wa kwanza dhidi ya Bejaia nchini Algeria, beki huyu alipewa kadi nyekundu.
Katika mazoezi ya juzi jioni yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, kocha huyo alionekana kutenga vikosi viwili huku kimoja akionekana kukipa maelekezo ya jinsi ya kulinda goli lao na kushambulia ndani ya wakati mmoja.

Wakati mazoezi hayo yanaendelea, kocha alionekana akiwapa mbinu washambuliaji na viungo jinsi ya kutengeneza nafasi na kufunga huku msaidizi wake Juma Mwambusi akipewa mabeki.

Mara baada ya mazoezi hayo kumalizika, Pluijm alisema katika mechi hiyo wanahitaji ushindi wa aina yoyote ili wajiwekee mazingira mazuri ya kufuzu.
Pluijm alisema, tayari amekifanyia marekebisho kikosi chake kwenye nafasi zenye upungufu ikiwemo safu ya ulinzi iliyokuwa inaruhusu mabao ya kizembe na ushambuliaji inayokosa mabao mengi. Safu hiyo ya ushambuliaji leo itakuwa bila Mzimbabwe, Donald Ngoma ambaye anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

“Tumekuwa tukifungwa mabao ya kizembe kwenye mechi za Kombe la Shirikisho, hiyo yote ni kutokana na mabeki kukosa umakini pindi wapinzani wanapofika kwenye lango letu.
“Pia, safu ya ushambuliaji nayo imekuwa ikikosa umakini kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi zinazotengenezwa na viungo, hivyo hayo yote tayari nimeyafanyia kazi, tutaingia uwanjani kwa kazi moja ya ushindi pekee na siyo kitu kingine.
“Kikosi changu kinatarajiwa kuwepo na mabadiliko kwenye baadhi ya sehemu ambazo nisingependa kuzitaja kwa hofu ya wapinzani wangu, hivyo subiria Jumamosi (leo) utakiona kikiwa uwanjani,” alisema Pluijm.

Katika mazoezi hayo ya juzi, Cannavaro alishindwa kufanya pamoja na wenzake kutokana na majeraha ya enka na badala yake alijifua binafsi kwa kukimbia uwanjani tu huku Yondani akitoka uwanjani akishindwa kumalizia mazoezi baada ya kujitonyesha nyonga lakini katika mazoezi ya jana nyota hao waliungana na wenzao.

Akizungumzia majeruhi hao, Daktari Mkuu wa Yanga, Edward Bavu alisema, hatma ya wachezaji kucheza au kutocheza ilitarajiwa kujulikana jana baada ya mazoezi ya mwisho kumalizika, lakini Championi Jumamosi linafahamu mabeki hao hawatacheza kutokana na majeraha hayo.

Kikosi cha leo cha Yanga kitakachoanza kinatarajiwa kuwa hivi; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi, Bossou, Dante, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.
Waandishi: Wilbert Molandi, Sweetbert Lukonge, Said Ally, Omary Mdose na Nicodemus Jonas

No comments