Header Ads

Mzee Yusuph Atangaza Kuacha Kuimba Taarabu..Amrudia Mungu wake!

Mzee Yussuf amesisitiza kuwa ameachana rasmi na muziki na hana maskhara na hatua aliyoichukua ya kumtumikia Mwenyezi Mungu. Akiongea na Saluti5, Mzee alisema sanaa pekee atakayoshiriki ni ile itakayohusiana na dini yake ya Kiislam kama vile kuandaa nyimbo za kaswida na kucheza filamu za maadili ya dini. 

“Nimeshatengeneza nyimbo mbili za kaswida, lengo langu ni kukamilisha albam pamoja na video yake na baada ya hapo nitafanya mkutano na waandishi wa habari na kuweka wazi malengo yangu nje ya muziki wa kidunia,” alisema Mzee Yussuf. Mzee aliyekuwa mtunzi, mwimbaji na mmiliki wa Jahazi Modern Taarab, amesema ameshawaambia viongozi waliobakia kuwa wasiendelee kutumia jina lake na picha zake kwenye matangazo ya bendi kwa sababu kufanya hivyo ni kuwaongopea watu. 

“Najua yako matangazo ambayo yameshatengenezwa kwaajili ya maonyesho mengi yajayo yakihusisha jina langu, sina tatizo na hilo lakini kwa matangazo mapya yatakayofanywa kuanzia sasa sitahitaji jina na picha zangu zitumike,” alifafanua Mzee Yussuf na kongeza kuwa hiyo ni hatua ya kwanza na kwamba kuna mambo mengine ya msingi yatafuata baadae. 

Akizungumzia namna anavyojiskia baada ya kuamua kuzama kwenye ibada na kuachana na muziki, Mzee Yussuf alisema: “Kwa kweli najiskia raha sana, sasa ni nina wingi wa utulivu na amani. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuniongoza kwenye njia ya haki. “Hii ni vita kubwa, kuishinda vita hii sio jambo la mchezo, namuomba Mungu aniepushe na vishawishi vitakavyokuja mbele yangu. 

Sitaki kurejea kwenye muziki.” Aidha, Mzee Yussuf amesema si kweli kuwa amebadili dhehebu kama ilivyoripotiwa na baadhi ya watu kuwa ameijiunga na dhehebu la Answar Sunna.

CHANZO: SALUTI 5

No comments