Header Ads

MZIMBABWE AZAM FC: HUYU CHIRWA HATARI SANA


MNAOBEZA uwezo wa mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa sikieni hii! Beki wa kimataifa wa Zimbabwe anayeichezea Azam FC, Bruce Kangwa, ameweka wazi kuwa mshambuliaji huyo ni hatari kutokana na kuwa na uwezo wa hali ya juu, tofauti na watu wanavyomchukulia.

Chirwa aliyesajiliwa Yanga kwa dola laki moja (zaidi ya Sh milioni 200 za Kitanzania) akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kuonyesha kiwango cha kawaida kwenye michezo mbalimbali ya timu hiyo na mpaka sasa hajaifungia bao lolote licha ya kupewa nafasi mara kwa mara.

Akizungumza Kangwa anayecheza nafasi ya beki ya kushoto, amesema anamjua Chirwa kuwa ni mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa na kama akipewa muda zaidi, anaweza kuibeba timu hiyo kwenye michezo ijayo.

“Namjua Chirwa kwa sababu tumecheza wote kule Zimbabwe na ni mshambuliaji hatari, pia ni msumbufu kwa mabeki tofauti na watu wanavyomchukulia.

“Siamini kama ameshindwa kuonyesha kiwango kwa sababu hana uwezo, nadhani labda bado anaendelea kuzoea mazingira ya hapa na kama akipewa muda zaidi, basi watakuja kumkoma kwenye michezo ijayo,” alisema Kangwa ambaye ametokea timu ya Highlander ya Zimbabwe.

No comments