Header Ads

Omog: Yanga hii moto ...Bado wanaweza kuchukua ubingwa

PAMOJA na kuboronga kwao kwenye michuano ya kimataifa, Kocha wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, anaamini bado Yanga ni timu ambayo itafanya vema msimu ujao kutokana na uwepo wa Mdachi, Hans van Der Pluijm.

Yanga ilianza vibaya kampeni yake ya kusaka tiketi ya kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo katika mechi nne iliambulia moja kabla ya juzi Jumamosi kupata ushindi wa kwanza kwa kuichapa MO Bejaia ya Algeria bao 1-0.

Katika mahojiano na Championi Jumatatu kuhusu anavyoijua Yanga ya sasa chini ya Pluijm, Omog hakutaka kuwa mnafiki, badala yake alimmwagia sifa Pluijm na timu yake akidai inafanikiwa kutokana na kuwa na kocha mzuri.

“Timu kutwaa ligi mara mbili na kuchukua makombe matatu kwa pamoja siyo jambo dogo. Binafsi niwe mkweli Pluijm ni kocha mzuri sana,” alisema kocha huyo wa zamani wa Azam.

Omog anaamini takwimu hizo zinawafanya Yanga kuwa wapinzani wakuu katika msimu mpya unaoanza wikiendi hii ambapo Simba watakata utepe na Ndanda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Yanga imefufua shangwe za mashabiki wake baada ya kupata ushindi huo wa juzi.

Msimu ujao unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa, hasa kutokana na Simba na Azam nazo kujipanga huku Yanga ikionekana kuwa na makali yaleyale.

CHANZO: CHAMPIONI

No comments