Header Ads

Rais asema fedha si tatizo kuhamia Dodoma

RAIS John Magufuli amesema fedha kwa ajili ya kuhamia makao makuu Dodoma siyo tatizo na kwamba suala la kuhamia huko halina mjadala na wanaosema haliwezekani wanatakiwa kutambua kuwa jambo hilo mbele yake litawezekana.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais John Magufuli. 

Alisema jambo hilo mbele yake haliwezi kukwama, kwani michakato ya kuhamishia serikali Dodoma imezungumzwa kwa miaka mingi, hivyo yeye anafanya utekelezaji huo kwa kufikisha michakato hiyo katika tamati.
Akizungumza baada ya kuwasili katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Magufuli alisema haiingii akilini tangu mwaka 1973 jambo hilo linazungumzwa, lakini halitekelezeki.
“Wanasema eti kuhamia Dodoma haiwezekani, hee! Mbele ya Magufuli itawezekana tu. Michakato imetosha… nitahakikisha tunahamia Dodoma,” alisema na kuongeza: “Wapo wanaosema hela (fedha) tutatoa wapi, mbona kipindi cha Bunge huwa tunakaa na hata wakati wa Bunge la Bajeti tunakwenda huko mpaka watendaji… tunakwenda kule na ukisikia waziri amekuja Dar unamwambia kazi hamna.”
Alisema anatambua kuwa kuna wizara zinazotazamana na bahari, hivyo atatangaza zabuni ya kujenga hoteli katika maeneo hayo ili aone nani atakayeendelea kukaa huko.
Aliongeza fedha zitakazopatikana kwa kujenga hoteli hizo atazipeleka Dodoma kwa ajili ya kujenga majengo mengine.
Kuhusu uvumi kuwa majengo ya Ikulu yatauzwa, alisema si kweli kwa kuwa majengo hayo hayawezi kuuzwa, kwani ni ya heshima ila yatabaki kama makumbusho.
Alisema katika kipindi cha utawala wake atahakikisha serikali inahamia Dodoma, kwani hakuna kinachoshindikana ila ilikuwa imeshindikana kwenye akili za watu.
Aliongeza kuwa, hata kwa mambo ya kiusalama hakuna mji unaojengwa pembezoni mwa bahari, ni lazima uwe katikati na wakihamia Dodoma miji ya Iringa, Babati, Singida na maeneo mengine ya jirani itapanuka.
Wakati akitoa hotuba ya shukrani kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk Magufuli alitangaza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itahamia Dodoma ndani ya miaka yake minne na ushee iliyobaki sasa kabla ya kumaliza muhula wake.
Alirudia suala hilo kwenye sherehe za Mashujaa mjini humo Dodoma, Julai 25; na kuungwa mkono na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyetangaza kuwa yeye atahamia mjini humo mwezi ujao, uamuzi ambao una maana kuwa serikali yote sasa itapaswa kuwa makao makuu hayo ya nchi. Dk Magufuli alizungumzia pia masuala mengine ya serikali yake hadi sasa akisema imefanikisha elimu bure na hilo limejionesha kwa idadi ya watoto walioandikishwa darasa la kwanza kuongezeka maradufu.
Alisema alipoingia madarakani alianza utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi kwa kutoa elimu bure, kwani ilifika mahali watoto wa masikini walikuwa wakidaiwa ada na wengine walishindwa kusoma kwa kukosa ada lakini sasa wengi wanasoma kwa kuwa elimu ni bure.
“Nilipanga hela lazima nizitafute, mimi sina hela mfukoni mwangu ila hela tutazipata kwa mafisadi ndio maana mimi na serikali yangu tunawatumbua ili tupate hela za kusomesha watoto wetu. Nataka kujenga nidhamu ndani ya serikali,” alisema.
Alisema alipoingia alikuta makusanyo ya mapato ni Sh bilioni 850, lakini baada ya kubana mapato yaliongezeka hadi Sh trilioni 1.5, akisema makusanyo hayo yalikuwa yakiliwa na wachache wachache walioko ngazi ya juu.
Aliongeza kuwa spidi yake ya kufanya kazi ni kubwa hivyo hataki kuona mtu anamkwamisha kwa kuwa amepanga kufanya mambo mazuri. Alisema ndio maana wameamua kujenga reli ya kisasa ili kubeba mizigo ya kutosha, kununua ndege tatu na mbili zitaingia mwezi ujao na kwamba serikali imetenga Sh bilioni 100 kwa ajili ya kuboresha viwanja vya ndege vya Iringa, Songea na Musoma.
Alizitaja huduma nyingine ambazo serikali imeamua kuboresha ni umeme ambapo mradi wa Kinyerezi II una megawati 240 na Kinyerezi I utaongezewa megawati 185 na pia Kinyerezi III na IV inakuja ili kuongeza usambazaji wa umeme nchini uwe mkubwa.
Alisema bajeti ya maji mwaka huu imeongezwa na pia kwa Dar es Salaam kuna mradi wa maji unakuja, na pia wamepata mkopo wa dola za Marekani milioni 500 (sh trilioni 1.05) kutoka Serikali ya India.
Kwenye sekta ya afya, alisema wametenga Sh trilioni 1.99 na kwamba wametenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya kununulia dawa hospitalini tofauti na mwaka uliopita ambapo ilitengwa Sh bilioni 25.

CHANZO: HABARI LEO

No comments