• Latest News

  August 24, 2016

  Rais Magufuli Apokea Hati Za Utambulisho Kutoka Kwa Mabalozi Wa Nchi Mbalimbali Ikulu Jijini Dar

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23 Agosti, 2016 amepokea hati za utambulisho kutoka Mabalozi wanne wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.

  Mabalozi hao ni Mhe. Roberto Mengoni - Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Kim Yong Su - Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea hapa nchini, Mhe. Mohamed Hassan Abdi - Balozi wa Jamhuri ya Somalia hapa nchini na Mhe. Paul Sherlock - Balozi wa Ireland hapa nchini.

  Akizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupokea hati za utambulizo za Mabalozi hao Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itawapa ushirikiano wa kutosha ili kuendeleza na kuuimarisha zaidi uhusiano ulipo kati ya nchi hizo na Tanzania.

  Dkt. Magufuli amewaambia Mabalozi hao kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2012 Tanzania imedhamiria kutekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda, hivyo amezialika nchi zao na sekta binafsi katika nchi hizo kuungana na Tanzania katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na biashara.

  "Naomba kukuhakikishia kuwa Wafanyabiashara watakaokuja kuwekeza ama kufanya biashara, mitaji yao itakuwa salama na Serikali yangu itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha uwekezaji huo unafanikiwa na unanufaisha pande zote mbili" Amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Ireland Mhe. Paul Sherlock.

  Aidha, Rais Magufuli amewashukuru Marais wa nchi zote nne ambazo Mabalozi wake wamewasilisha hati za utambulisho kwake hii leo na amewahakikishia kuwa uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo utadumishwa na kuimarishwa zaidi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

  Gerson Msigwa
  Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
  Dar es Salaam
  23 Agosti, 2016
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Rais Magufuli Apokea Hati Za Utambulisho Kutoka Kwa Mabalozi Wa Nchi Mbalimbali Ikulu Jijini Dar Rating: 5 Reviewed By: 2jiachie
  Scroll to Top